Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Familia yajifungia ndani siku mbili, nyuki wakitanda kwenye nyumba

Muonekano wa nyuki mdudu ambaye licha ya kuzalisha asali lakini ni hatari kwa usalama wa binadamu.

Muktasari:

  • Nyuki hao wameweka makazi kwenye matundu ya njiwa na wengine kwenye mti uliopo jirani na mlango wa kuingilia ndani.

Morogoro.  Mkazi wa Mtaa wa Bomba la Zambia, Kata ya Kingolwira, Manispaa ya Morogoro, Abina Kiasi (47) na familia yake wamejifungia ndani kwa siku mbili baada ya nyuki kuvamia nyumba na kutengeneza makazi kwenye vibanda vya njiwa na mti ulioko karibu na mlango wa kuingilia ndani.

Akizungumza leo Jumapili Aprili 27, 2025 na Mwananchi kwa simu, Abina amesema kabla ya nyuki hao kuweka makazi, walikuwa na tabia ya kupita eneo hilo tangu Februari mwaka huu bila kuleta usumbufu.

"Awali, walipokuwa wakipita, hawakuwa wakisumbua, lakini safari hii wamevamia kabisa. Walianza kuweka makazi kwenye mti ulioko mbele ya nyumba yangu, kisha wakaingia kwenye matundu ya njiwa wa mwanangu na kuanza kuwashambulia njiwa. Baadhi ya njiwa walikufa na wengine walikimbia na hawajarudi hadi sasa," amesema Abina.

Baada ya nyuki hao kujeruhi mabinti zake wawili, mama huyo amesema aliamua kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, aliyemuelekeza amtafute mfugaji wa nyuki kwa msaada.

"Nilimtafuta huyo mfugaji, naye juzi Aprili 25, alikuja na mavazi maalumu, akaondoa makazi ya nyuki waliokuwa kwenye matundu ya njiwa na kutumia mafuta ya petroli pamoja na kuchoma moto matambaa ili kuwasambaratisha," amesema.

Hata hivyo, amesema jana asubuhi, nyuki hao walirudi tena na kuenea kwenye maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo, hali iliyomlazimu yeye na watoto wake kuendelea kujifungia ndani wakihofia kushambuliwa.

"Tunakosa huduma muhimu kama kwenda chooni na hata kununua chakula. Kesho watoto wanapaswa kwenda shule, lakini hatujui watawezaje kutoka. Riziki yangu pia imesimama kwa sababu siwezi kutoka nje," amesema.

Amesema majirani nao wameingiwa na hofu na wameshindwa kutoa msaada kutokana na wingi wa nyuki hao waliotanda hadi kwenye kuta za nyumba yake.

 "Tupo ndani kitandani, tumejifunika chandarua kujilinda na nyuki wachache waliopenya ndani," amesema.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Aclay Dimoso, amekiri kupokea taarifa hiyo, akisema alijaribu kumtafuta mfugaji wa nyuki ambaye aliwasaidia awali, lakini baada ya nyuki kurudi, alishindwa kuingia karibu na nyumba kwa usalama wake mwenyewe.

"Nimeamua kuwasiliana na watu wa idara ya maliasili ili waje kutoa msaada wa kitaalam," amesema Dimoso.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugojo amesema jeshi hilo limepokea taarifa na linaelekea eneo la tukio likiwa na vifaa vya uokoaji.

"Nyuki ni hatari. Tunapaswa kuwaondoa kwa njia salama bila kusababisha madhara kwa watu waliopo karibu. Sasa tupo njiani kuelekea kumsaidia mama huyo na familia yake," amesema Marugojo.