Mtoto avamiwa na nyuki, afariki dunia

Muktasari:
Mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Nyamirama, Kata ya Rung’abure wilayani Serengeti Mkoa wa Mara amefariki dunia baada ya kushambuliwa na kundi la nyuki wakati akifua nguo kisimani.
Serengeti. Mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Nyamirama, Kata ya Rung’abure wilayani Serengeti Mkoa wa Mara amefariki dunia baada ya kushambuliwa na kundi la nyuki wakati akifua nguo kisimani.
Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Samweli Nyamabere alimtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Timasi Safi (12).
Alisema tukio hilo lilitokea Januari 26 saa kumi jioni na kukimbizwa katika Zahanati ya Nyamirama.
Hata hivyo alisema baada ya hali kuwa mbaya, Safi alihamishiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Nyerere kwa matibabu zaidi, lakini Januari 27 alfajiri alifariki dunia.
Nyamabere alisema Safi, ambaye alikuwa na watoto wenzake walivamiwa na nyuki hao baada ya kuwachokoza katika eneo lenye mzinga.
“Watoto wengine walifanikiwa kukimbia huku wakipiga kelele kuomba msaada, Safi alibaki akihangaika kumnusuru mdogo wake ambaye alikuwa anashambuliwa, alichofanya ni kumlalia ili asiumwe na nyuki, na mashambulizi yakahamia kwake,” alisema Nyamabere.
Ofisa Mtendaji wa kata hiyo, Mniko Kiaga alisema hilo ni tukio la kwanza kutokea katika kata hiyo.
Aliwaomba wananchi kuwanaofuga nyuki kuwaweka katika maeneo ambayo hayafikiwi na watoto na mifugo.