Wajasiriamali Arusha, Dodoma na Dar kunolewa

Arusha. Taasisi ya Kingdom Leadership Network Tanzania (KLNT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Regent cha nchini Marekani, wameungana katika kutoa kozi mbalimbali hapa nchini ikiwemo ya uongozi, biashara na ujasiriamali.
Akizungumza leo kwenye uzinduzi wa Programu ya mafunzo ya maendeleo ya biashara mkoani Arusha jana, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Isaac Mpatwa alisema kituo hicho 'Business Development Center' lengo kuu ni kuwaandaa viongozi bora, wafanyabiashara na wajasiriamali kuanzia kwenye wazo la biashara.
"Programu hii ya ujasiriamali na biashara kwa vitendo itasaidia vijana kuanzia kuboresha wazo la biashara hadi kufungua biashara na kwa wale ambao wana biashara tunawafundisha na kuwawezesha kukuza biashara zao na inaendana na masuala ya kifedha ndiyo maana hapa tupo na taasisi za fedha,"amesema
Mpatwa ambaye pia ni mwanzilishi wa taasisi hiyo, amesema kuwa hadi sasa wameshafikia wajasiriamali zaidi ya 100 ambapo programu hiyo iliyoanzia Dar es Salaam mwaka 2021, Dodoma mwaka jana na mwaka huu Arusha.
"Tumekuja Arusha kukuza na kuendeleza wafanyabiashara kwa ajili ya kubadili uchumi wa wajasiriamali wetu. Januari 27, 2024 kozi zitaanza rasmi katika mikoa hii mitatu kwa muda wa wiki 20 ambapo yatatolewa na wakufunzi wa kimataifa," amefafanua
Mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Regent, Jason Benedict amesema wameamua kushirikiana na KLNT kwa lengo la kusaidia wajasiriamali na jamii iweze kukua kiuchumi zaidi.
Mmoja wa wawezeshaji wa mpango huo, James Mwang'amba amesema programu hiyo ni muhimu na inasaidia kumfundisha mjasiriamali mbinu za jinsi ya kufanya biashara, kupata mitaji na kuongeza masoko na kuwa ni muhimu hasa kwa vijana.