Tulia ashindwa kuimba wimbo wa mbingu, Kikwete akumbuka ‘lifti’ ya Msuya

Muktasari:
- Amesema viongozi waliopo sasa, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan, wana matarajio na dhamira ya kuendelea kuhudumia wananchi, hivyo kuimba wimbo huo kwa sasa kungeweza kuonekana kama ishara ya kutotamani kuendelea na majukumu yao.
Mwanga. Wakati Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akieleza namna alivyoshindwa kuimba wimbo wa “Moyo wangu una furaha ya kwenda mbinguni” katika ibada ya mazishi ya hayati Cleopa Msuya, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, alitumia jukwaa hilo kumkumbuka tukio la mwaka 1990, Msuya alipowasaidia yeye na waziri wake usafiri wa kurudi ofisini, baada ya baraza la mawaziri kuvunjwa wakajikuta hawana usafiri.
Ibada hiyo ya mazishi ilifanyika katika Usharika wa Usangi Kivindu, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakuu wa kitaifa.
Dk Tulia alieleza kuwa hakuweza kuimba wimbo huo kwa sababu ujumbe wake ulihusu utayari wa kwenda mbinguni, jambo ambalo alilihusianisha moja kwa moja na hali ya kisiasa, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
"Niliamua kukaa kimya na kusikiliza kwa makini. Nikasema, nashukuru askofu alituruhusu tusio tayari tusiimbe. Sisi tunaotazamia uchaguzi 2025 hatujaimba, si kwa sababu hatutaki kwenda mbinguni, bali tunaomba kwenda baadaye," alisema Dk Tulia kwa ucheshi uliopokelewa kwa vicheko na tafakari.
Dk Tulia amesema aliathiriwa sana na ujumbe wa wimbo huo ambao ulizungumzia utayari wa kwenda mbinguni. Wimbo huo namba 157, fungu la tatu, kutoka katika kitabu cha ‘Tumwabudu Mungu wetu uliombwa kuimbwa na Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Dk Alex Malasusa.
Hata hivyo, Dk Tulia amesema hakushiriki kuimba wimbo huo na alimshukuru Askofu Malasusa kwa kuelewa na kuruhusu wale ambao hawakuwa tayari, kutouimba.
"Kuna neno unasikia na unajua linakuhusu. Kila mmoja amechukua kile kinachomgusa, lakini mimi nilikaa kimya, nikasikiliza kwa makini sana ule wimbo unaosema ‘mbinguni tunao utayari’. Nikaona siwezi kuimba, kwa sababu sina utayari wa kwenda sasa," alisema Dk Tulia.
"Nashukuru kwa kuturuhusu tusio tayari tusiimbe… Sasa hivi tuna mtazamo na matarajio, tuna Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambaye tunamtarajia, na sisi wengine wenye matarajio pia, hatukuimba."
Kikwete na lifti ya Msuya
Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesimulia tukio la Aprili 12, 1990 siku ambayo Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alivunja Baraza la Mawaziri na hayati Msuya akamsaidie lifti.
"Ni siku ambayo haitafutika kwenye kumbukumbu zangu. Tulifika Ikulu kwa wito maalumu, jambo la ajabu kwa manaibu mawaziri ambao kawaida huwa anahudhurikii vikao vua cabinet (Baraza la Mawaziri), lakini siku hiyo tuliambiwa na sisi twende. Tulipofikia, Mzee Mwinyi alitushukuru kwa huduma yetu na kututaka wote tujiuzulu," alisema Kikwete.
Amesema baada ya mkutano huo, walijikuta hawana usafiri wakaanza kutembea kuondoka Ikulu, kwa kuwa madereva walijua mkutano ungechukua muda mrefu kama kawaida, hivyo waliondoka Ikulu.
"Tulitoka nje tukakuta magari hakuna. Tukatembea kutoka Ikulu hadi karibu na barabara, ndipo tukakubaliana kwenda Wizara ya Fedha iliyokuwa karibu Mzee Msuya akatupatia usafiri.
“Tunashukuru mitandao haikuwepo wakati huo, vinginevyo picha zile zingekuwa historia ya taifa na zingekuwa zinarudiwarudiwa," alikumbuka kwa tabasamu.