Mtoto wa Cleopa Msuya: Baba alitaka kijengwe Chuo Kikuu Mwanga

Muktasari:
- Ameyasema hayo leo Mei 13, 2025 wakati akitoa neno la shukrani katika ibada ya maziko ya baba yake ambayo yanafanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Usangi Kivindu, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Mwanga. Jobu Msuya ambaye ni mtoto wa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu, Cleopa Msuya, ameeleza jinsi ambavyo baba yake alivyowakutanisha katika siku yake ya kuzaliwa mwaka huu na kueleza matumaini yake ya kukumbukwa kupitia ujenzi wa chuo kikuu katika Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Amesema kwamba si kawaida kwa baba yao kusherehekea kumbukizi ya siku yake ya kuzaliwa, lakini mwaka huu, Januari 4, aliwaita pamoja na kueleza kuwa angetamani kusherehekea siku hiyo muhimu akiwa na watoto wake.
Msuya, ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia Mei 7, 2025 kutokana na maradhi ya moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam. Atazikwa leo, Mei 13, 2025, katika makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwake.

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anaongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi hayo yamehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali na chama.
Viongozi wengine walioungana na Rais Samia katika mazishi hayo ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Wengine ni Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Katibu Mkuu wa CCM Dk Emmanuel Nchimbi, makatibu wakuu viongozi, mawaziri mbalimbali, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Camillus Wambura, pamoja na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, John Malecela na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Ameyasema hayo leo Mei 13, wakati akitoa neno la shukrani katika ibada ya maziko ya baba yake ambayo yanafanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Usangi Kivindu, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

"Nawashukuru kwa kujumika nasi leo na kutufariji, nilipata habari za msiba wa baba saa 11 saa za Japani Mei 7 nikiwa kazini inilichukua muda kutoka ofisini hadi nyumbani, na kutoka kule mpaka huku ilikuwa ni safari ndefu,"amesema Jobu.
"Baba yetu yeye ni mtoto wa tano katika familia ya Mzee David alikuwa kiongozi wa familia kwa sababu yeye ndiye alibakia kama mwanafamilia," amesema Jobu.
Katika siku hiyo ya sherehe yake ya kuzaliwa alipanga ni nani anataka aje na nani mchungaji, nani afike katika sherehe hizo na ikawa hivyo.
"Januari 4, mwaka huu ilikuwa ‘birthday’ (Siku ya kuzaliwa) yake baba, baba yetu alikuwa hapendi kufanyiwa 'birthday' lakini akaagiza nataka kufanya, akaagiza ni mchungaji gani aje afanye sala bahati nzuri ilifanyika vizuri sana," amesema mtoto huyo wa Msuya.

"Baada ya 'birthday' kupita alisema nia yake ni kijengwe chuo kikuu Mwanga cha 'Brain power by Technology’ au IT, lakini akasisitiza sana benki ambayo alikuwa mwasisi wake ambayo ni Hakika Mwanga Benki kwamba tuikuze iwe kama Benki ya NMB au CRDB," amesema.
Akizungumzia mambo aliyojifunza kwa baba yake amesema kubwa ni namna alivyowafundisha kupambana na kujitafutia wenyewe.

"Katika miaka 54 tuliyoishi na baba jambo kubwa ambalo nimejifunza kwa baba ni kupambana na kujitafutia wenyewe, mimi binafsi sikumbuki kama baba amewahi kunipa hata senti moja, alitusisitiza tupambane wenyewe na kujitafutia wenyewe ila hakusita kuwa mshauri mkubwa na tulipata muda wa kuchambua changamoto tulizopata lakini pesa zake alikuwa hatoi." amesema Job.