Msuya aagwa, viongozi wa dini waonya rafu za uchaguzi

Askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya katika viwanja wa CD Msuya vilivyopo Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Ibada ya kuuaga mwili wa Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya imefanyika Mwanga, Kilimanjaro, ambako viongozi wa dini wametumia jukwaa hilo kuonya dhidi ya rafu kwenye uchaguzi mkuu ujao. Wataka wananchi kukataa rushwa ya uchaguzi na kuiga uadilifu wa Msuya.
Mwanga. Wakati mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya, ukiagwa katika viwanja vya CD Msuya, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, viongozi wa dini wameonya rafu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Wamesema viongozi wazuri ni wale wanaochaguliwa na wananchi, na si wale wanaogawa fedha chafu kipindi cha uchaguzi ili kupata nafasi.
Msuya ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia Mei 7 mwaka huu kwa ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salaam na anatarajiwa kuzikwa kesho Mei 13, 2025.
Mamia ya wananchi, viongozi mbalimbali wa Serikali na chama wamejitokeza katika viwanja hivyo kuaga mwili wa kiongozi huyo.
Akihubiri katika ibada maalumu ya kuaga mwili wa Msuya uwanjani hapo, Askofu Mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mwanga, Dk Daniel Mono, amewataka Watanzania kuiga mfano wa Msuya kwa kuwa alikuwa ni kiongozi aliyependwa na wananchi kutokana na kutanguliza maslahi yao na Taifa.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa katika viwanja vya CD Msuya, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro
"Tuseme kweli na kukataa uongo, hasa tukikataa watu wanaogawa fedha chafu kipindi hiki cha uchaguzi. Baba huyu (Cleopa Msuya) mimi ninaamini hata angeamua kuwa mbunge wa maisha angekuwa, kwa sababu alipendwa, lakini kwa sababu alijua saa ya kupanda jukwaani na saa ya kushuka, alijiongeza," amesema Dk Mono.
Amesema katika nafasi yake hakuweza kugawia watu fedha ili awe mbunge na kipindi hiki amewaonya wana-Mwanga na Watanzania wote wakatae watu wanaonunua kura, kataeni, hawafai.
Amesema mtu apewe nafasi kwa sifa yake njema, kwa bidii yake, kwa moyo wake, hata akimtazamwa usoni afanane na anachokisema, hata mienendo yake.
"Mzee wetu alipendwa kwa sababu kazi zake zilikuwa njema. Waswahili wanasema chema chajiuza lakini kibaya kinajitembeza, msikubali kuhongwa hongwa, tusiuze uhuru wetu na dhamana yetu ya kupiga kura kwa sababu ya chakula cha siku moja. Dhamiri yako ikutume kufanya maamuzi sahihi," amesema.
Aidha, ametumia pia nafasi hiyo kuwataka viongozi wote kumuenzi Msuya kwa kuweka mbele maslahi ya wananchi na Taifa na kutosheka na mishahara wanayopewa.
Amesema kila mwenye nafasi ya uongozi na anayefikiria kuwa kiongozi, aweke maslahi ya wananchi mbele badala ya maslahi yake. "Tutamuenzi kwa kuweka maslahi ya Taifa na wananchi mbele badala ya maslahi yetu binafsi na tutosheke na mishahara tunayopewa," amesema Dk Mono.
Ameongeza kuwa watu wanaomtegemea Mungu bila kulewa nafasi na elimu walizo nazo, vyeo, heshima zisababisha wakasahau ibada, wajifunze kwa Msuya pamoja na nafasi kubwa aliyokuwa nayo lakini alimtukuza Mungu.
Aidha, amewataka kumuenzi kwa kuendeleza umoja na mshikamano na kamwe wasikubali kubaguliwa kwa sababu yoyote ile.
"Tuna sababu ya kumshukuru Mungu kwa kutupa baba Cleopa Msuya. Familia mshukuruni Mungu kwa kuwapa baba bora, aliyewalea na kuwafikisha hapa mlipo, Wilaya ya Mwanga ambayo alitumika kwa ubunifu na akapendwa na kupendeka, lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sote tumshukuru Mungu kwa ajili ya mtu huyu ambaye alikuwa kiongozi bora na wa kuigwa."
Akimzungumzia marehemu Msuya, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, amesema mzee Msuya ameacha alama zisizofutika na kwamba hazihitaji mtu kuvaa miwani kutazama.
"Niwashukuru wote mliofika hapa kwa ajili ya utumishi wake uliotukuka. Baba Askofu Mteule amesema mengi katika mahubiri yake, sitaki kuyapunguza uzito, lakini itoshe niseme katika utumishi wa umma hivi sasa kuna makundi mawili nitapata nini, nitaacha nini. Mzee wetu ameacha alama ambazo hazihitaji kuvaa miwani kutazama ama kuchunguza," amesema Bagonza.
Aidha, amesema katika uongozi wake ameitumikia Serikali yake na wananchi vya kutosha, hivyo ni wakati wake wa kurudi kwa Mwenyezi Mungu.
"Tunaposoma Zaburi ya 103:5, mzee wetu aliyelala hapa mbele yetu Mwenyezi Mungu amemshibisha vyema uzee wake. Mzee ametusindikiza vya kutosha, amesindikiza Serikali, Kanisa na waumini wote wa dini zote, amesindikiza Chama cha Mapinduzi. Ni wakati wake kurudi ili tuzoee kuwa peke yetu," amesema Bagonza.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amesema atamkumbuka Msuya kwa kuwa alipenda kusema kweli hata katika mazingira magumu.
"Msuya ni mzee mmoja ambaye ameacha mambo mazuri. Moja nililompendea, alikuwa akipenda kusema ukweli hata katika mazingira magumu. Sisi wapambe ambao hatukuwa kama tutapata nafasi, tulikuwa tukichota busara zake," amesema Pinda.
Aidha, amesema Msuya aliiheshimisha Wilaya ya Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla kutokana na uzalendo wake.
Kuhusu viongozi wa dini kuwaasa kuwakataa wanaogawa pesa ili wapate nafasi za ubunge, Pinda amesema tuwapime kwa kazi na si kwa kugawa pesa.
"Viongozi wetu wametuasa tuwakatae wanaogawa pesa ili waje watuhudumie. Tutakupima kwa kazi uliyofanya. Huu ni ujumbe mzuri kwa ambao wapo katika ndoto ya kuchukua nafasi za ubunge," amesema Pinda.
Aidha, amewataka Watanzania kushikamana na kuungana kwa pamoja kuliombea Taifa na kuwashukuru viongozi wa dini kwa namna ambavyo wameendelea kuliombea Taifa.
Naye Mbunge wa Mwanga, Joseph Thadayo, amesema watamkumbuka Msuya kwa kuwa hakuwa mchoyo wa maarifa.

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akiaga mwili wa Cleopa viwanja vya CD Msuya
"Mzee hakuwa mchoyo wa maarifa yake. Alitushirikisha, alitujenga, alisisitiza umoja. Naamini kabisa tutaenda vizuri, mtuombee ili tusitikisike," amesema Thadayo.
Baada ya shughuli za kuaga mwili kumalizika katika viwanja vya CD Msuya, mwili utapelekwa Usangi kijijini kwake ili kutoa fursa kwa wananchi wa eneo hilo kuaga kabla ya kupelekwa nyumbani kwake ambako utalala.