Mwili wa Cleopa Msuya wapokewa KIA, kuagwa Mwanga

Muktasari:
- Cleopa Msuya ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia Mei 7, 2025 kwa ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es salaam na atazikwa kesho Mei 13, 2025.
Hai. Mwili wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya umewasili leo Mei 12, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kupokelewa na viongozi wa mbalimbali wa Serikali .
Msuya ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia Mei 7, 2025 kwa ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es salaam na atazikwa kesho Mei 13, 2025.
Mwili huo ambao umebebwa na ndege ya shirika la ndege la Air Tanzania, umetua katika uwanja huo saa 8:20 asubuhi ambapo baada ya kushushwa kwenye ndege, umebebwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuingizwa kwenye gari maalumu la jeshi hilo.
Baada ya kupokelewa kwa mwili huo na viongozi wa Serikali, wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, msafara utaelekea Wilaya ya Mwanga katika viwanja vya CD Msuya ambapo wananchi watapata fursa ya kuaga.

Baadaye, mwili utapelekwa katika uwanja wa Shule ya Sekondari Kilaweni Usangi kijijini kwake ambapo pia wananchi wa maeneo hayo watapata fursa ya kuaga na kisha utapelekwa nyumbani kwake kwa ajili ya taratibu za maziko.
Mbali na Lukuvi, yupo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hamza Juma, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (Suki) na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Rabia Hamid na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu.

Wengine ni wabunge wa Mkoa wa Kilimanjaro, akiwemo Saashisha Mafuwe, Mbunge wa Hai, David Mathayo, Mbunge wa Same Mashariki na viongozi wengine.
Mazishi ya Msuya hapo kesho Mei 13, 2025 yanatarajiwa kuongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.