Mzee Msuya anavyokumbukwa kama kiraka cha nyakati ngumu

Muktasari:
- Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya (94) atakumbukwa kama kiongozi aliyerejesha matumaini ya nchi katika nyakati ngumu. Mwili wake utazikwa kijijini kwake.
Dar es Salaam. Umahiri wa uongozi katika nyakati ngumu kiuchumi, ni moja kati ya sifa nyingi zitakazokumbukwa daima katika utumishi wa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya (94) kwa nafasi mbalimbali alizohudumu.
Kwa mujibu wa viongozi mbalimbali wa Serikali, Mzee Msuya ndiye kiongozi aliyeteuliwa kuiongoza Wizara ya Fedha baada ya athari za vita vya Kagera na akafanikiwa kuimarisha uchumi uliokuwa umetetereka.

Ukiacha utumishi wa umma, kwa upande wa familia, nyadhifa alizokuwa nazo, hazikuwa turufu kwa wanawe kupata kila walichokitaka, badala yake wanasema aliwataka wajitafutie vya kwao na kuwapiga marufuku kulitumia jina lake kupata chochote.
Maelezo hayo kuhusu Mzee Msuya yanakuja siku chache baada taarifa za kifo chake kilichotokea Mei 7, 2025 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo yaliyomsumbua kwa miaka kadhaa.

Wakizungumza leo Jumapili, Mei 11, 2025 katika hafla ya kutoa heshima za mwisho kitaifa kwa Mzee Msuya, viongozi hao wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wamemtaja kuwa kiongozi aliyekuwa jasiri, anayelipenda Taifa lake na alitangulisha masilahi ya nchi. Rais Samia hakuzungumza chochote.
Mzee Malecela
Katika salamu zake za pole, Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela amesema amemfahamu Mzee Msuya kwa zaidi ya nusu karne wakifanya kazi pamoja katika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali na amejifunza mengi kutoka kwake.
Amesema amejifunza uongozi, kutanguliza mbele maslahi ya Taifa badala ya binafsi na alikuwa mtulivu, asiye na papara, mwenye hekima na alisikiliza kwa makini kabla hajazungumza.
“Kila alipozungumza alizungumza maneno ya busara na yenye mashiko katika kipindi cha utumishi wake, alishika nyadhifa kubwa na katika zote alijipambanua kwa umahiri wa kupanga sera, udhibiti wa matumizi ya rasilimali na usimamizi wa uchumi wa Taifa,” amesema.
Amesema alifanya naye kazi kwa karibu hasa katika kipindi kigumu cha uchumi na walilazimika kuchukua hatua ngumu kwa ajili ya ustawi wa Taifa.
“Mzee Msuya alikuwa mtu jasiri na mwenye maono, hakushinikizwa na maneno ya ndani na hata nje, alisimamia misingi ya haki, uwajibikaji na uwazi na alithamini mashirikiano ya kitaifa,” amesema.
Ameeleza Mzee Msuya alishiriki siasa za nchi kikamilifu kupitia Tanu na Chama cha Mapinduzi (CCM) na wakati wote alihimiza siasa za hoja, maadili na heshima na alikuwa daraja la kizazi cha waasisi na viongozi wapya.

“Tanzania imepoteza hazina, tuliobaki tunabeba wajibu wa kuendeleza misingi aliyoisimamia na aliyoiamini. Tunapoomboleza leo na kwenda kumzika katika nyumba yake ya milele tumuenzi kwa vitendo vya kuwa waadilifu, wanyenyekevu na wenye kuzingatia na kuliweka Taifa mbele,” amesema.
Alichokisema Dk Mpango
Kwa upande wa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema baada ya kustaafu kwake, Mzee Msuya alikuwa kisima cha maarifa na busara na amewahi kumwona kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali.
Dk Mpango amesema Msuya aliendelea kufuatilia utatuzi wa changamoto za wananchi wenzake wa Mwanga ingawa tayari alishastaafu utumishi wa umma. Miongoni mwa changamoto ni mradi wa maji wa Same-Mwanga ambao ulichukua muda mrefu kukamilika na Mzee Msuya kuwa sehemu ya walioshiriki hafla ya uzinduzi wake.
“Familia ya marehemu, natambua msiba huu ni pigo kubwa kwenu, lakini farijikeni kwa kuwa Mzee Msuya ataendelea kutambuliwa kuwa kiongozi wa pekee aliyefanya kazi nzuri,” amesema.
Ameitaka familia kuhakikisha inakamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha maisha yake kwa kuwa mwenyewe aliwahi kumdokeza kuhusu kuanza kwa kazi hiyo.
Maelezo ya familia
Akizungumza kwa niaba ya familia, mtoto wake, Joyce Msuya amesema licha ya utumishi wa Mzee Msuya enzi za uhai wake, hakuacha familia iache kwenda kanisani kila Jumapili na alichukia jina lake kutumika na mwanawe yeyote kupata chochote.
Joyce amesema Mzee Msuya alipenda wanawe wote wapitie jeshini na hakutaka wapangwe katika eneo la karibu na atakapokuwa yeye.
Kwa mujibu wa Joyce, Mzee Msuya hakuwa anawapa fedha, badala yake aliwataka wajitafutie, huku nyakati za likizo za masomo, aliwaruhusu wafanyakazi wote kwenda likizo, ili watoto ndio wafanye kazi za nyumbani.
“Kabla hajaenda kazini baba alikuwa anauliza kwamba tumeenda Azania Front na kujiunga na kwaya. Tunashukuru pia wajukuu alionao wanamfahamu na kumpenda babu yao,” amesema.
Amesema hakupenda, ubabaishaji, uongo, dharau na majivuno na aliipenda familia yake zaidi ya alivyojipenda yeye binafsi, ndiyo sababu kila alipowasiliana na wanawe aliuliza hali za wajukuu zake.
“Nilipata nafasi ya kuongea na baba saa 14 kabla sijapata taarifa kuwa amefariki, alikuwa ananiuliza wajukuu zangu wanaendelea, wewe unaendeleaje, umekula na hata ukimuuliza kuhusu hali yake hakuwa anajijali yeye zaidi ya kujali familia,” anasema.
‘Tunaendelea kunufaika’
Kwa upande wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema wanaofanya kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu wanaendelea kunufaika na juhudi za utumishi wa Mzee Msuya kwa kila alichokifanya alipokuwa na wadhifa huo.
“Natoa pole kwa watumishi wa umma na wote walioguswa na msiba huu, tumepoteza kiongozi aliyekuwa anatushauri na aliyetuhimiza kufanya kazi kwa bidii,” amesema.
Amesema tayari maandalizi kwa ajili ya maziko yake Usangi mkoani Kilimanjaro, yamefanyika kama ilivyoelekezwa na atazikwa katika hali nzuri.
Majaliwa amesema kesho Jumatatu, Mei 12, 2025 wakazi wa Mwanga watapata nafasi ya kumuaga na jioni mwili wake utasafirishwa hadi kijijini kwao Usangi kwa ajili ya maziko.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amesema Tanzania imepoteza kiongozi mahiri aliyejitolea kwa uzalendo kuwatumikia wananchi.
Katika nyadhifa zake, amesema Mzee Msuya alikuwa muumini wa umoja wa kitaifa na muungano na aliwatumikia Watanzania wote kwa unyenyekevu.
“Tutamkumbuka kwa umakini wake wa kuitumikia Tanzania katika uchumi, katikati ya athari za vita vya Kagera na madhara mengine,” amesema.
Namna bora ya kumuenzi Mzee Msuya, amesema ni kuyaendeleza maono ya kudumisha umoja na mshikamano, kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo ili kuhakikisha nchi inapiga hatua.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema alielekezwa kuwatembelea viongozi wakuu wastaafu kupata maarifa ya ujenzi wa chama hicho na miongoni mwao alimtembelea Jaji Joseph Warioba.
Amesema katika maongezi yao, Warioba alimwelezea Msuya kuwa kiongozi aliyepewa nafasi ngumu katika nyakati ngumu na ndiye kiongozi aliyekuwa na moyo wa pekee na alikuwa na mawazo ya kujenga.
“Alinisihi nitakapokwenda kwake nimuulize maswali mengi na niende na shajara kwa ajili ya kuandika nisipoteze chochote. Kwa bahati mbaya sikubahatika kwenda kwake na nitarudi kwa Mzee Warioba akaniambie,” amesema.
Huyu ndiye Msuya
Akisoma wasifu wa marehemu, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi amesema Msuya alizaliwa Januari 4, mwaka 1931, katika Kata ya Usangi mkoani Kilimanjaro. Ni mtoto wa tano kati ya tisa wa Mzee Msuya.

Alisoma katika Shule ya Msingi Nakivindu mkoani Kilimanjaro 1942, kisha akajiunga na Shule ya Usangi 1943 na baadaye mwaka 1949 alihitimu Sekondari ya Old Moshi, kabla ya kwenda Tabora kwa kidato cha tano na sita.
Mwaka 1955 alijiunga na Elimu ya Juu katika Chuo Kikuu cha Makerere akisoma Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Historia, Siasa, Sayansi na Jiografia.
Mwaka 1956 alianza utumishi wa umma kwa nafasi ya Ofisa Maendeleo ya Jamii hadi mwaka 1961 na baadaye akawa Naibu Kamishna wa Maendeleo ya Jamii hadi mwaka 1964.
Mwaka 1965 Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, 67 Wizara ya Ardhi Makazi na Maendeleo ya Maji, mwaka 1970 Uchumi na Mipango.
Mwaka 1972 alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Hazina na baadaye 1975 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Mwanga na kuteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.
Mwaka 1980 alikuwa Waziri wa Fedha hadi 1983 alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu hadi 1985 aliporejea tena wadhifa wake wa Waziri wa Fedha.
Mwaka 1985-1990 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango na 1990-1994 aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, kisha 1994-95 alikuwa Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu.
Mwaka 1995 hadi 2000 alikuwa Mbunge wa Mwanga na Oktoba 29, 2000 alitangaza kung’atuka ubunge wa Mwanga akastaafu utumishi wa umma na siasa.
Tangu mwaka 1964 hadi mwaka 1977 alikuwa mwanachama hai wa TANU na akawa mwanachama wa CCM na ni miongoni mwa waasisi.
Msuya amecha watoto sita na wajukuu 10, amefariki kwa ugonjwa wa moyo ambao alikuwa akitibiwa katika hospitali mbalimbali ikiwamo ya Mzena, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na nchini Uingereza tangu 2022.