Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uhamiaji watinga Tusiime kuchunguza madai ya walimu wasio na vibali

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Shule ya Tusiime, Albert Katagira amekana madai yaliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, akisema ni taarifa za uzushi zinazolenga kuhujumu biashara yake.

Dar es Salaam. Maofisa uhamiaji wamekwenda katika Shule ya Tusiime iliyopo Tabata, Dar es Salaam kuchunguza madai kuwa imeajiri walimu zaidi ya 30 kutoka nje ya Tanzania bila vibali vya kazi, kinyume cha Sheria ya Kudhibiti Ajira za Wageni ya mwaka 2015.

Taarifa za kuwapo hali hiyo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii wiki iliyopita zikieleza mbali na kuajiri wageni, walimu wazawa walikuwa wamewekwa kando na kupewa notisi ya kusitisha mikataba yao, suala ambalo uongozi wa shule hiyo ulikanusha.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle awali alisema ndiyo kwanza anasikia, wangefuatilia na kufanyia kazi.

“Nimeipokea taarifa, nitaiwasilisha sasa hivi na tutaanza kuifanyia kazi, mtasikia tu,” alisema Mselle.

Siku nne baadaye, Mwananchi lilimtafuta tena Mselle kujua hatua iliyofikiwa, alisema tayari maofisa wa idara hiyo ngazi ya mkoa wamekwenda shuleni hapo.

Kwa mujibu wa Mselle, kati ya Mei 9 au 10, mwaka huu, ndipo maofisa hao walipowasilisha ripoti yao kwa Kamishna wa idara hiyo, hatua itakayofuatiwa na kuiweka hadharani.

"Maofisa ngazi ya mkoa walikwenda shuleni na nafikiri kati ya jana au leo (Ijumaa au jumamosi) wamewasilisha ripoti yao kwa Kamishna, kitakachofuata ni kuiweka wazi," amesema Mselle.

Kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha sheria hiyo, kuajiri mgeni bila kibali halali ni kosa la jinai linaloweza kupelekea faini ya hadi Sh10 milioni au kifungo cha hadi miaka miwili, au vyote kwa pamoja.

Sheria ya Uendelezaji wa Ajira kwa Raia ya mwaka 1999, inasema Kamishna wa Kazi lazima ajiridhishe kuwa jitihada zote zimefanyika kupata mtaalamu wa ndani kwa nafasi hiyo kabla ya kuidhinisha ombi la kibali cha kazi kwa mgeni.


Kinacholalamikiwa

Baada ya taarifa hizo kusambaa mtandaoni, Mwananchi lilimpata mmoja wa walimu wa shule hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliyeeleza walimu waliopo kutoka nje ni zaidi ya 30 na ana uhakika hawana vibali vya kufanya kazi nchini.

Amesema uhakika wake unatokana na wanayoshuhudia kila maofisa wa uhamiaji wanapotembelea shuleni hapo, kwani walimu hao hujificha, hivyo wao (uhamiaji) huongea na uongozi na kutoweka.

Hatua hiyo amesema inasababisha walimu waliopo nchini wasipangiwe vipindi na kuwekwa tayari kuondoshwa.

Amesema ajira za walimu kutoka Uganda zimekuwapo kwa muda mrefu, lakini kwa sasa wameongezeka.

"Kwa sasa walimu hao wameongezeka na kuna mpango wa kuwaondoa kazini wazawa wote ili wabaki wao," kilieleza chanzo hicho cha habari.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa shule hiyo, Albert Katagira alikana madai hayo akisema kile kinachosambazwa katika mitandao ya kijamii ni taarifa za uzushi zinazolenga kuhujumu biashara yake.

Katika shule hiyo, alisema walimu kutoka nje ya Tanzania hawazidi saba na wote wana vibali halali vya kufanya kazi nchini kwa mujibu wa sheria.

“Nipo kwenye sekta hii ya elimu na biashara ya shule kwa zaidi ya miaka 20, najua taratibu zote. Kila ninapoleta walimu kutoka nje ya Tanzania lazima nifuate taratibu,” alisema Katagira.

Alisema kila kinachoelezwa dhidi ya shule hiyo ni nia ovu ya washindani wake wa kibiashara, wanaolenga kuathiri soko alilonalo.

Katagira alisema uamuzi wa kuajiri baadhi ya walimu kutoka nje ni kwa sababu wana ushindani unaoendana na mabadiliko ya mtalaa, ukilinganisha na baadhi ya waliopo nchini.

“Jambo la kujadili ni ubora wa walimu wetu, sina maana kwamba wote wabaya, hapana, lakini wenzetu wametuzidi, wana ushindani mzuri sana,” amesema.

Amesema si mara ya kwanza shule yake kuzushiwa taarifa mbaya, iliwahi kuhusishwa na tukio la kubakwa kwa mwanafunzi, jambo alilodai lilikuwa la uongo.

"Hizi biashara zina ushindani, mtu akikuona unafanya vizuri ataleta tu chokochoko zake ilimradi akuharibie mimi najua utaratibu wa kuajiri na sheria za nchi. Siwezi kufanya kosa hilo," amesema.