Treni ya Mwakyembe yapata ajali, chanzo chatajwa

Muktasari:
- Katika ajali hiyo watu saba walijeruhiwa, hata hivyo walipata msaada wa haraka kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Dar es Salaam. Treni ya abiria katika jiji la Dar es Salaam, inayofanya safari zake kati ya Kariakoo na Pugu, imepata ajali huku sababu ikitajwa kuwa ni mabehewa matatu kuacha njia.
Katika ajali hiyo, watu saba walijeruhiwa na kupelekwa hospitali ya Amana, hata hivyo walipata msaada wa haraka kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Mei 13, 2025, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi amesema ajali hiyo imetokea leo saa 11 jioni kati ya eneo la Kamata ikielekea Machinga Complex.
“Ni kweli ajali hiyo imetokea leo saa 11 jioni wakati treni hiyo ikiwa inaelekea Pugu, na ni baada ya mabehewa matatu katika treni hiyo kuacha njia.
“Hata hivyo, tunashukuru hakuna behewa lililoanguka zaidi ya kuinama na tayari waliokuwa ndani ya treni hiyo wameokolewa wakiwemo majeruhi saba,” amesema Kamanda Mabusi.
Amesema wanashukuru waliwahi mapema katika eneo hilo la ajali na kuwaokoa majeruhi hao na kwa kuwa hakukuwa na purukushani, waliokuwa kwenye mabehewa mengine walitoka salama.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, Bryceson Kiwelu, amekiri kupokea majeruhi 10 waliotokana na ajali hiyo kati yao wanane ni wanawake na wawili ni wanaume.
Akielezea kuhusu hali zao , Kiwelu amesema wamepata majeraha madogo madogo na hakuna aliyepata mvunjiko wowote.
“Ni kweli muda wa jioni tulipokea majeruhi wa ajali ya treni, ambao wote wanaendelea vizuri hadi sasa huku baadhi yao tukitarajia kuwaruhusu leo hiihii,”amesema Mganga huyo.
Taarifa ya TRC imesema ajali hiyo ilihusisha mabehewa 12 yaliyobeba abiria 1,200, wataalamu wa shirika na timu ya afya ya shirika, walifika na kutoa msaada wa huduma ya kwanza ambapo majeruhi 10 wakiwemo wanaume wanane na wanawake walikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Amani kwa matibabu zaidi.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Fredy Mwanjala, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano imesema chanzo cha ajali hiyo ambayo imesababisha mabehewa sita kuathirika bado hakijafahamika na shirika litatoa taarifa zaidi.
“Kufuatia ajali hiyo, shirika linauarifu umma huduma ya usafiri wa treni ya mjini kwenda Pugu, utaendelea kesho kama kawaida,” amesema Mwanjala.