Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tira yaomba kurahakishwa bima ya lazima, sera ya kitaifa ya bima

Muktasari:

  • Hatua hiyo itasaidia kupanua soko na kuwezesha kuunda mipango ya bima inayojengwa kwa mahitaji maalum.

Arusha. Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) imehimiza Serikali kuharakisha uanzishwaji wa Sera ya Taifa ya Bima, ikisema mfumo huo utawezesha sekta mbalimbali kuandaa mipango ya bima inayofaa mali na huduma na hivyo kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mamlaka hiyo pia imesisitiza umuhimu wa kuharakisha uandaaji wa kanuni zitakazoweka bima ya lazima kwa vivuko, majengo ya biashara na bidhaa zinazoingizwa nchini, kanuni hizo zitasaidia kuongeza mapato ya bima na kutoa ulinzi mkubwa kwa wananchi wakati wa majanga.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Bima, Dk Baghayo Saqware, Ijumaa Juni 20, katika Maadhimisho ya Siku ya Bima Tanzania yaliyoratibiwa na Taasisi ya Bima Tanzania (IIT) kwa kushirikiana na Tira na wadau wengine, huku zaidi ya washiriki 400 wakihudhiria.

“Kuwepo kwa sera ya kitaifa ya bima kutasaidia kupanua soko na kuwezesha kuunda mipango ya bima inayojengwa kwa mahitaji maalum. Hivyo, tunahimiza serikali kushughulikia suala hili,” amesema.

Saqware amesema ingawa Sheria ya Fedha ya mwaka 2022 ina masharti ya bima ya lazima kwa majengo ya biashara, bidhaa zinazoingizwa, na meli, bado kanuni za utekelezaji hazijafanyiwa kazi.

Amesema umuhimu wa kumaliza mchakato huo kusaidia ukuaji wa soko na kuongeza mapato.

Akijibu hoja hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar na Balozi wa Bima, Zena Said, ameahidi kuwasilisha suala hilo kwa Katibu Mkuu Kiongozi ili kuharakisha mchakato na kuhakikisha sera ya kitaifa pamoja na kanuni za bima ya lazima zinaendeshwa.

“Haya ni mambo muhimu kwa serikali kufikia malengo ya 2030 katika sekta ya bima,” amesema Zena.

Akizungumzia utendaji wa sekta kwa miaka minne iliyopita, Dk Saqware amesema takwimu zinaonyesha ongezeko la mapato ya bima, kuongezeka kwa watoa huduma, ukuaji wa ajira, na kuongezeka kwa bidhaa za bima zinazokidhi mahitaji ya watu wengi ikiwamo wakulima, wavuvi, wafanyabiashara wadogo, na wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi.

“Ukuaji huu unaonyesha juhudi za Tira na wadau zinaendelea kuzaa matunda. Kupitia usimamizi mzuri, elimu kwa umma, na uvumbuzi wa bidhaa za bima, tumefanikisha kuwafikia wananchi wengi na kuimarisha imani yao,” amesema.

Amesema idadi ya watoa huduma za bima imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi 2,208 mwaka jana, ongezeko la asilimia 122.4 kwa miaka minne, sawa na asilimia 22.1 kwa mwaka.

Idadi ya walionufaika na huduma za bima imeongezeka kutoka milioni 14.2 mwaka 2021 hadi milioni 25.9 mwaka jana, ongezeko la asilimia 82.4 kwa miaka minne, sawa na asilimia 22.2 kwa mwaka.

Kwa upande wake, Zena amepongeza juhudi za Tira na wadau lakini akasisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia, kukuza rasilimali watu na kueneza bima ya afya na kilimo kwa kuwa hilo litasaidia sekta hiyo kuwa sehemu ya ajenda ya serikali ya kuinua uchumi kupitia sekta ya fedha.

Ameongeza kuwa bima haijatambuliwa vya kutosha kutokana na matumizi duni ya teknolojia na elimu hafifu kwa wananchi, akisema elimu bora itawafanya wananchi kununua bidhaa mbalimbali za bima.

“Nasisitiza umuhimu wa kuimarisha jitihada za kusimamia sekta ya bima na kuendeleza wataalamu wa bima. Hili ni jukumu la serikali na sekta binafsi.

“Tunahitaji wataalamu wenye ujuzi wa kutosha ili kusaidia kukuza na upatikanaji wa bidhaa za bima. Niwaombe pia wabunge kutumia nafasi yao kuelimisha vijijini ili wananchi waweze kuelewa vyema.”
Katika hotuba yake, Mwakilishi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara amesema kwa kushirikiana na serikali na sekta ya bima, UNDP inasaidia kuanzisha bima ya kilimo ili kuimarisha uwezo wa wakulima wadogo.

Licha ya ahadi hizi, bima bado haijatumiwa kikamilifu duniani na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kiwango cha ueneaji ni chini ya asilimia 3, UNDP imejitolea kushirikiana na serikali na sekta ya bima Tanzania kuwekeza katika mustakabali mzuri wa nchi.

“Tanzania iko kwenye takriban asilimia 2.01 ya Pato la pato la taifa. Sekta imeonyesha ukuaji mzuri kwa malipo ya bima kufikia Sh1.4 trilioni mwaka jana, lakini bado kuna mapengo katika maeneo kama kilimo, afya, na bima ndogo,” amesema.