Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vyanzo vinane kuchangia bima kwa wote VVU/Ukimwi

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026, jijini Dodoma leo Juni 12, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Serikali imesema fedha itakayopatikana itapelekwa kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote.

Dar es Salaam. Serikali katika mwaka 2025/2026 imependekeza kuanzisha vyanzo vya mapato vinane kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kugharimia bima ya afya kwa wote.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh586.4 bilioni.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Juni 12, 2025 na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alipowasilisha bungeni, mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/2026.

Amesema hatua hiyo inatokana na mabadiliko ya kisera yanayoendelea duniani ambayo yamesababisha wadau muhimu wa maendeleo kupunguza misaada iliyokuwa inatolewa kwa ajili ya huduma za afya, ikiwamo kukabiliana na kudhibiti magonjwa mbalimbali hususan Ukimwi.

Dk Mwigulu amesema Serikali inapendekeza kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato ili kupunguza nakisi ya kibajeti iliyotokana na kupungua kwa misaada kwa kufanya marekebisho katika sheria mbalimbali.

“Inapendekezwa asilimia 70 ya mapato yatakayoongezeka ipelekwe kwenye Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) na asilimia 30 ipelekwe kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa Wote,” amesema.

Amesema Serikali inapendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ili kuongeza ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kilevi vinavyozalishwa na vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi.

Waziri amesema Sh20 kwa lita kwa bia zinazotambulika kwa heading 22.03, Sh30 kwa lita kwa mvinyo unaotambulika kwa heading 22.04, 22.05, na 22.06. Vilevile Sh50 kwa lita kwa pombe kali na vinywaji vingine vinavyotambulika kwa heading 22.08.

Eneo lingine amesema ni kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ili kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye huduma za mawasiliano ya kielektroniki kutoka asilimia 17 hadi asilimia 17.5.

“Kufanya marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220 ili kutoza kiasi cha Sh10 kwa kila lita ya mafuta ya petroli, dizeli na ya taa. Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Madini, Sura 123 ili kutoza kiwango cha asilimia 0.1 kwenye thamani ya soko ya madini,” amesema.

Dk Mwigulu ametaja eneo jingine la chanzo cha fedha ni kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura 41 ili kuongeza kiwango cha kodi kwenye zawadi ya ushindi kwenye michezo ya kubashiri matokeo kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 na kwenye michezo ya kasino ya ardhini kutoka asilimia 12 hadi asilimia 15.

Pia kutoza magari na mashine zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kwa Sh50,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini (CC) kati ya 0 -1000, Sh100,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini kuanzia 1001-1500, Sh150,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini kuanzia 1501-2500, Sh200,000 kwa magari yenye ukubwa wa injini kuanzia 2501 na zaidi.

Amesema Sh250,000 kwa mashine (excavators, bulldozers, fork lifts) zenye heading 84.29 na 84.27.

“Pia kutoza Sh500 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya treni na kutoza Sh1,000 kwa kila tiketi inayotolewa na mtoa huduma za usafirishaji kwa njia ya anga,” amesema.