Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vifurushi bima ya afya viangaliwe upya

Kauli ya Waziri Jenista Mhagama kuwa Serikali inaanza rasmi utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni hatua muhimu na ya matumaini kwa wananchi.

Kauli hiyo aliyoitoa wakati akihitimisha mjadala makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2025/26, ililenga  kujibu mjadala kutoka kwa wabunge kuhusu gharama za vifurushi vya bima ya afya, hususan zinazohusu matibabu ya figo na magonjwa yasiyoambukiza.

Mjadala huo, ulionyesha wazi kwamba bado kuna changamoto kubwa kwenye upangaji wa gharama hizo na upatikanaji wa huduma kwa Watanzania wa kipato cha chini.

Ni kweli, kama walivyosema baadhi ya wabunge kwamba magonjwa yasiyoambukiza ni “bomu linalosubiri kulipuka” katika mfumo wa afya kutokana na ukubwa wa gharama za matibabu yake.

Na ndiyo maana Serikali inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata kinga ya matibabu kupitia mfumo wa bima ya afya kwa wote. Lakini katika hali halisi ya uchumi wa wananchi wengi, hasa waishio vijijini na katika sekta isiyo rasmi, utekelezaji wa mpango huu unahitaji umakini mkubwa katika kupanga gharama na aina ya vifurushi vitakavyotolewa.

Kauli za baadhi ya wabunge ziligusa kiini cha tatizo: haiwezekani kuwalinganisha matajiri wenye uwezo wa kulipa bima ya afya kwa urahisi na wananchi wa kawaida wanaopambana na hali ngumu ya maisha.

Mjadala huu haupaswi kupuuzwa, bali uwe chachu ya kurejea upya upangaji wa vifurushi vya bima kwa mtazamo wa usawa na uhalisia wa maisha ya Watanzania walio wengi.

Ni jambo lisilopingika kuwa huduma bora za afya zinahitaji fedha nyingi. Lakini mfumo wa bima ya afya haupaswi kuwa mzigo kwa mwananchi bali msaada wa kumkinga na gharama kubwa zisizotarajiwa za matibabu.

Dawa nyingi ni ghali, ndiyo, lakini pia tunaweza kupunguza gharama hizo kwa kudhibiti ununuzi holela, kuboresha manunuzi ya pamoja na kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma katika sekta ya afya.

Serikali kupitia Wizara ya Afya inapaswa kutoa uhakika kuwa vifurushi vya bima ya afya kwa wote vitapangwa kwa kuzingatia kipato cha kila kundi la jamii.

Wananchi walio katika sekta isiyo rasmi na wale wa kipato cha chini wanahitaji kifurushi chenye gharama nafuu lakini chenye huduma za msingi na muhimu, hasa kwa magonjwa sugu kama kisukari, shinikizo la damu na maradhi ya figo na mengineyo.

Hili linawezekana kama Serikali itashirikiana na wadau wa maendeleo, sekta binafsi na mashirika ya kijamii kuwekeza katika mfuko wa pamoja wa bima kwa wote.

Ni vyema wananchi wakaelimishwa zaidi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya, lakini elimu hiyo iende sambamba na uhalisia wa uwezo wao wa kuchangia. Ufanisi wa mpango huu hautapimwa kwa idadi ya waliojiunga tu, bali kwa kiasi ambacho watu wa kawaida wanaweza kupata huduma bora bila kuelemewa na mzigo wa gharama.

Ni matumaini yetu kuwa ahadi ya Serikali ya kupunguza vifo na kuweka wananchi salama itatimia kwa kuhakikisha kwamba vifurushi vya bima ya afya vinakuwa jumuishi, vinazingatia hali halisi ya Watanzania na vinatolewa kwa gharama ambazo mwananchi wa kawaida anaweza kuzimudu. Hapo ndipo dhana ya “Bima ya Afya kwa Wote” itakapopata maana halisi.