Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NHIF yazindua vifurushi vipya vya bima ya afya kwa watoto

Waziri wa Afya Jenista Mhagama (wa pili kulia) wakati wa akizindua vifurushi vipya vya Bima ya Afya ya NHIF jijini Dodoma

Muktasari:

  • Serikali imetaka ushirikishwaji wa wadau kupata vifurushi vya Bima ya Afya kwa Wote (UHC) visivyo na malalamiko, huku Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) umefuta vifurushi vya zamani na kuanzisha vipya vya Serengeti Afya na Ngorongoro Afya.

Dodoma. Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), umezindua vifurushi vipya vya bima ya afya, huku ikifuta vifurushi vya Najali, Timiza na Wekeza na kuanzisha vifurushi vipya vya Ngorongoro na Serengeti.

Kwa mujibu wa mfuko huo, maboresho hayo yanalenga kumwezesha mtu binafsi pamoja na familia yake kujiunga na mfuko na kunufaika na huduma kadiri ya umri pamoja na idadi ya wanufaika.

Maelezo ya utaratibu wa kujisajili yanaonyesha kuwa kifurushi cha Ngorongoro Afya kina jumla ya huduma 445, huku gharama ya kujiunga ikianzia Sh240,000 kwa mnufaika mmoja kwa mwaka.

Kwa upande wa kifurushi cha Serengeti Afya kina jumla ya huduma 1,815 na gharama yake inaanzia Sh660,000 kwa mnufaika kwa mwaka.

Kuhusu Toto Afya Kadi, watakaosajiliwa kwa makundi watachangia Sh50,400 kwa mwaka na endapo atasajiliwa peke yake kwa mwaka atakuwa akichangia Sh150,000 kwa mwaka.

Hata hivyo, vifurushi hivyo vya Toto Afya Kadi kwa mtoto atakayejiunga kwa hiari (peke yake), vimegawanywa katika makundi matatu na chaguo la kwanza mnufaika anatakiwa kuchangia Sh658,000, chaguo la pili Sh237,000 na la tatu ambalo ni la mwisho ni Sh150,000.

Akizindua mifumo na vifurushi vya Mfuko leo Jumanne, Desemba 17, 2024, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama ameagiza NHIF kuwashirikisha wadau wote ili kupata maoni ya vifurushi visivyo na malalamiko ambavyo vitakwenda kwenye Bima ya Afya kwa Wote (UHC).

Waziri Mhagama amesema anatambua kuwa mfuko huo uko katika hatua ya kuja na vifurushi mbalimbali ili kuwezesha wananchi kujiunga kupitia Sheria ya UHC.

“Tuhakikishe tunashirikisha wadau wote muhimu ili kupata maoni ya makundi yote na kupata vifurushi vitakavyokwenda kwenye Bima ya Afya kwa Wote ambavyo havina malalamiko na vifurushi vitakavyosaidia sekta ya afya kusimama vizuri,” amesema Mhagama.

Aidha, amesema awali NHIF ilikuwa imegubikwa na changamoto nyingi, ikiwamo ucheleweshaji wa huduma kwa wananchi na malipo na kubwa ilikuwa udanganyifu, lakini sasa changamoto hizo zitaenda kumalizwa kupitia mifumo mipya itakayotumika na hivyo kusaidia mfuko kuchukua taswira mpya.

Hivyo, ametoa rai kwa uongozi wa mfuko huo kuhakikisha unafanya maboresho ya mifumo mara kwa mara kwa kuzingata mazingira halisi waliyonayo na kuendelea kubuni namna bora za kufanya tathimini na ufuatiliaji wa wigo wa wanachama kujiunga na mfuko.

Kuhusu mifumo ya kidijitali, Mhagama amesema kwa kiasi kikubwa itasaidia kuondokana na uchakataji na uwasilishaji madai, huku asilimia 80 ya vituo vikiunganishwa kudhibiti udanganyifu kwa watoa huduma na wanaopewa huduma.

“Mifumo itutengenezee mazingira mazuri kuelekea Bima ya Afya kwa Wote, wadau wote washirikishwe ili kupata maoni ya makundi yote na vifurushi visivyo na malalamiko,”amesema.

Kwa upande wa Toto Afya Kadi iliyozinduliwa leo, Mhagama ameupongeza mfuko huo kwa mabadiliko ya muda mfupi, ikiwemo kutekeleza agizo hilo kwa vitendo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka amesema mifumo hiyo imejengwa na wataalamu wa ndani kwa gharama ya Sh445 milioni, ikiwa ni tofauti ya Sh3.5 bilioni kama ingejengwa na wataalamu kutoka nje ya nchi.

Amesema mifumo hiyo itawezesha wanachama kujisajili bila kufika ofisini, kupata namba ya kulipia michango na kuangalia matumizi ya kadi yake.

Akitolea mfano mtoto atakayelipiwa bima kwa Sh50,400,  atapata kifurushi cha Sh400,000 na akienda kutibiwa anaweza kukiona kiasi kilichobaki kupitia ujumbe mfupi wa maneno (SMS), atakayotumiwa katika simu.

Pia amesema mfumo wa uchakataji wa madai umerahisisha kazi hiyo kutoka kuchakata madai 800 kwa siku hadi 1,000 kwa dakika 40, hatua itakayoondoa ucheleweshaji wa madai kwa watoa huduma na kuongeza ufanisi.

Kuhusu Kadi ya Toto Afya, amesema sasa huduma zitatolewa kwa watoto walio katika makundi na mtoto mmoja mmoja tofauti na awali ilikuwa ikitolewa katika makundi pakee.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu ameshauri NHIF kuangalia suala la malipo kwa watoa huduma.

Amesema baadhi yao walikuwa wanalalamika mapato yao yameshuka, wanashindwa hata kuwalipa watumishi wao wanaofanya kazi katika saa za ziada.

“Tunashauri maeneo ya kubadili vifurushi yaliyolalamikiwa yaangaliwe zitolewe gharama zinazokidhi pande mbili za hospitali binafsi na za Serikali,”amesema Kingu.