Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SMZ yakusanya Sh53 bilioni bima ya afya kwa wageni

Wageni kutoka mataifa mbalimbali wakiwa kwenye foleni kukaguliwa bima ya afya ya lazima kwa wageni baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ilianzisha mpango wa bima za safari kwa wageni wote wanaoingia Zanzibar, ambayo imeanza rasmi Oktoba mosi 2024.

Unguja. Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ikikusanya Dola za Marekani milioni 20.034 sawa na Sh53.270 bilioni kutokana na bima ya lazima za safari kwa wageni wote wanaoingia Zanzibar, zimetumika Dola za Marekani 1,591 milioni sawa na Sh4.127 bilioni pekee kati ya fedha hizo kutoa huduma iliyokusudiwa.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ilianzisha mpango wa bima za safari kwa wageni wote wanaoingia Zanzibar, ambayo imeanza rasmi Oktoba mosi 2024.

Lengo kuu la uanzishwaji wa bima ya Dola za Marekani 44 sawa na Sh116, 880 ni kutoa fidia kwa majanga yatakayowapata wageni ikiwemo ajali, kifo na upotevu wa nyaraka mbali mbali pale wanapokuwa katika visiwa vya Zanzibar.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Juma Makungu Juma ameeleza kwamba fedha hizo zimekusanywa tangu Oktoba mosi hadi Machi 31 na zilizotumika kwa kipindi hicho cha miezi sita ni kwa ajili ya kuwagharamia huduma mbalimbali wageni waliopatwa na majanga wakiwa Zanzibar.
Amesema lengo la uanzishwaji wa bima ni kutoa fidia endapo majanga yatatokea, hivyo bima hiyo imetumia gharama za madai mbalimbali yatokanayo na wageni kwa kipindi hicho.

Katika kikao cha 14 cha mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi cha Mei 22, 2025, Mwakilishi wa Kiembesamaki Suleiman Haroub Suleiman, aliuliza swali la nyongeza linalotokana na swali la msingi kuhusiana na tozo ya Dola za Marekani 44 kwa kila mgeni anayeingia Zanzibar.

Mwakilishi huyo alitaka kujua mpaka sasa hivi kuna kiasi gani kimetumika katika bima hiyo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya aliahidi kulijibu swali hilo kwa njia ya maandishi.

Hata hivyo, katika majibu ya yaliyotolewa siku hiyo Mei 22 katika mkutano huo wa Baraza la Wawakilishi Naibu Waziri alikuwa ameeleza kwamba bima hiyo tayari imekusanya Dola za Marekani 6 milioni (Sh16 bilioni).

Akijibu swali hilo kupitia taarifa ya Spika Juni 6, 2025, Naibu waziri Makungu amesema kuanzia Oktoba mosi hadi 31 Machi 2025, bima hii imefanikiwa kukusanya mapato ya Dola za Marekani 20 milioni sawa na Sh53.270 bilioni.

“Kwa kuwa lengo kuu la uanzishwaji wa bima ni kutoa fidia endapo majanga yatatokea, bima hii imetumia gharama za madai mbalimbali yatokanayo na wageni kuanzia Oktoba mosi hadi kufikia Machi 31, 2025 ni Dola za Marekani 1.591 milioni sawa na Sh4.127 bilioni yaliyohusisha matibabu,”

Amesema pia fedha hizo zimetumika kupeleka wagonjwa nchi za jirani kwa matibabu zaidi, kurudisha wageni na maiti nchini kwao, usumbufu katika safari ikiwemo kupotea kwa hati ya kusafiri, kuachwa na ndege, kubadilisha tiketi ya kusafiri kutokana na hali ya ugonjwa na mengineyo,” amesema

Mathalani, ametaja gharama zilizotumika ni pamoja na kurudishwa nyumbani raia wa Hungary waliovunjika miguu wakati wanaelekea uwanja wa ndege na kulazwa Hospitali ya Lumumba na baadaye kupitia Shirika la Bima la Zanzibar, lilikodi Air Ambulance iliyotokea nchini Morocco na kuwarudisha nyumbani kwao.

Vilevile, imetumika kugharamia wageni raia wa Ufaransa, Ujerumani na Kenya waliofariki wakiwa nchini walisafirishwa na kurejeshwa nchini kwao.

Hata hivyo bima hiyo ya Dola za Marekani 44 sawa na Sh116,880, imepunguzwa hadi kufikia Dola za Marekani 22 sawa na Sh58,440 kwa wageni wanaotoka nchi za Afrika Mashariki.