Madaktari wataka mwelekeo bima kwa wote, Serikali yatoa agizo

Muktasari:
- Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameliagiza kongamano la kitaifa la tiba kuja na mawazo mtambuka, yatakayoiwezesha Serikali kutekeleza kwa ufanisi mpango wa bima ya afya kwa wote.
Arusha. Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimeitaka Serikali kutekeleza kwa umakini Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ili kuwe na ubora wa huduma za afya kwa Watanzania wote katika upatikanaji, unafuu na uendelevu.
Kauli hiyo imekuja zikiwa zimepita siku saba, tangu mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2025/2026 kuanzisha vyanzo vya mapato vinane kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Ukimwi na kugharamia bima ya afya kwa wote.
Hatua hiyo itajwa kuwa inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh586 bilioni.
MAT imesema suala la bima ya afya kwa wote wanalipa kipaumbele, kama changamoto ambayo imeanza kupatiwa ufumbuzi.

Akizungumza katika kongamano la kitaifa la tiba linalokwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya chama hicho, leo Jumatano, Juni 18, 2025, Rais wa MAT, Dk Mugisha Nkoronko amepongeza kuona sheria ya bima ya afya kwa wote imepitishwa na utekelezaji umeanza kwa hatua za awali.
Amesisitiza kuwa bado kuna kazi kubwa mbele ya kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kikamilifu na kwa ufanisi.
"Changamoto itakuwa ni kuongeza uelewa kwa umma juu ya umuhimu wa kujiunga na bima, kuandikisha wananchi walio sekta isiyo rasmi, na kuhakikisha kuwa watoa huduma wanapata malipo stahiki kwa huduma wanazotoa kupitia mifumo ya bima bila urasimu mwingi.

"Tunatoa wito kwa wadau wote Serikali, sekta binafsi, mashirika ya bima na hata sisi watoa huduma tushirikiane kwa karibu ili lengo la bima ya afya kwa kila Mtanzania lifikiwe. Hili litasaidia kupunguza mzigo wa gharama kwa wagonjwa mmojammoja na familia, na pia litahakikisha upatikanaji endelevu wa fedha za kuendesha vituo vya kutolea huduma za afya, na hivyo kuboresha ubora wa huduma zenyewe," amesema Mugisha.
Akijibu hoja hiyo katika hotuba yake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amelitaka kongamano hilo kujadili namna bora ya kutoa huduma za afya.
"Tupeni ushauri wenu wa namna ya kutekeleza jukumu hili. Tumieni vema lengo la kukutana hapa, mwisho katika kuboresha huduma za afya nchini ninyi ni kipaumbele katika sekta ya afya," ameagiza.
Pamoja na agizo hilo, Majaliwa amesema sekta ya afya itaendelea kuwa kipaumbele muhimu, ndiyo maana wamefanya maboresho makubwa ikiwemo upatikanaji wa dawa.
Amesema Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa afya na mpaka sasa imeajiri watumishi 48,633 wa sekta ya afya na kufanya idadi ya watumishi wa sekta kufikia 177,711,ambayo imewezesha kupunguza uhaba wa watumishi wa sekta hiyo kutoka asilimia 64 hadi 55.
Akizungumzia mafanikio ya sekta hiyo amesema Serikali imeongeza idadi ya vituo vya afya kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi vituo 12,846 sawa na ongezeko la vituo 4,297 ambalo limewezesha asilimia 80 ya wananchi kupata huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano.
"Mpango wa Serikali ni kufikia asilimia 95 ya wananchi ifikapo mwaka 2030 watakaopata huduma karibu na makazi yao, Serikali pia imeanzisha huduma za mkoba za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi, ili kusogeza huduma hizo karibu na zaidi ya wananchi 154,015 wameweza kupata huduma za madaktari bingwa katika kambi mbalimbali," amesema.
Kuhusu hali ya upatikanaji wa vifaatiba na dawa, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa vifaa, vifaatiba, dawa na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za afya.

"Serikali imeimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya muhimu za kipaumbele 382 kutoka asilimia 58 mpaka asilimia 87 pamoja na kuongezeka kwa viwanda vya dawa, vifaa na vifaatiba kutoka 23 hadi 92.
"Ongezeko hilo la viwanda limepunguza uagizaji wa dawa, vifaa na vifaatiba kutoka nje ya nchi kwa asilimia 20 na kuongeza urahisi wa upatikanaji wa bidhaa hizo pamoja na kuipunguzia Serikali mahitaji na matumizi ya fedha za kigeni, kwa ajili ya kuagiza dawa nje ya nchi," amesema.
Awali, Rais wa MAT amegusia changamoto walizonazo akitaja uwepo wa Wizara ya Tamisemi na afya kuwa mgawanyo wa majukumu yake unasumbua, akisema MAT inashauri kuwe na muundo utakaowezesha zisomane.
"Tutengeneze wizara mbili zisomane, leo hii daktari aliyeajiriwa Tamisemi na Wizara ya Afya wanapata mishahara tofauti na wote walisoma chuo kimoja, wana elimu sawa na utendaji pia unafanana."
Pia ameshauri uwekezaji ufanyike katika eneo la watumishi wa afya ili kuondoa upungufu uliopo wa asilimia 55.
Awali, akitoa salamu zake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema mkoa huo umekuwa unashirikiana vema na madaktari na kila mwaka ambapo wamekuwa wakitoa matibabu bure kwa wananchi wasio na uwezo na mwaka jana walihudumia wagonjwa 32,000 kwa siku saba.
"Wananchi wasio na pesa walikuwa wanaishia njiani kwenye vipimo, hawana hela za dawa. Sasa tumeshirikiana na wenzetu MSD (Bohari ya Dawa), tunafanya matibabu bure kuanzia Juni 23 mpaka 29, 2025 tuna madaktari bingwa na tumeshapata dawa kuhakikisha hakuna itakayopelea na tumejipanga kuhakikisha hakuna atakayekosa huduma," amesema Makonda.