Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tira yabeba ajenda ya bima ya afya kwa wote

Muktasari:

  • Vipindi vya elimu vinafanyika kila siku kwenye Maonyesho ya Sabasaba ili kuwasaidia wananchi kuelewa vyema masuala ya bima na namna ya kujilinda dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Dar es Salaam. Wakati kampuni 40 chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (Tira) zikishiriki Maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) mkazo mkubwa umewekwa kuhamasisha umma kuhusu Bima ya Afya kwa Wote (UHI).

Vipindi vya elimu vinafanyika kila siku kwenye maonyesho hayo ili kuwasaidia wananchi kuelewa vyema masuala ya bima na namna ya kujilinda dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ambayo imesainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni inalenga kufanya bima ya afya kuwa ya lazima na inayopatikana kwa wote.

Akizungumza katika maonyesho hayo leo Jumamosi,  Julai 5, 2025, Meneja wa Tira Kanda ya Mashariki, Zakharia Muyengi amesema ajenda ya bima ya afya kwa wote ni jambo linalopaswa kupewa nguvu zaidi.

“Sheria ya bima ya afya kwa wote imeshapitishwa na tunafanya kazi kwa karibu na kampuni za bima kuitekeleza,” amesema Muyengi.

“Wakati wa maonyesho haya, kampuni shiriki zinatoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kunufaika na mipango mipya ya bima ya afya.”

 Muyengi amewahamasisha wananchi wenye malalamiko kuhusu huduma za bima kutembelea mabanda ya maonyesho kwa ushauri na msaada, akibainisha kuwa uelewa wa umma kuhusu bima bado ni mdogo.

Amesema kampeni zinazoendelea za uhamasishaji zitasaidia kuongeza uelewa na matumizi ya bima.

Takwimu kutoka Tira zinaonesha kuna ukuaji mkubwa wa sekta ya bima, idadi ya watoa huduma imeongezeka kutoka 993 mwaka 2021 hadi 2,208 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 122.4 kwa kipindi cha miaka minne, ikiwa na wastani wa ongezeko la kila mwaka la asilimia 22.1.

Vivyo hivyo, idadi ya Watanzania walioko kwenye mfumo wa bima imeongezeka kutoka milioni 14.2 mwaka 2021 hadi milioni 25.9 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 82.4 na wastani wa asilimia 22.2 kwa mwaka.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa ICEA Lion, Jared Awando amempongeza Rais Samia kwa kusaini sheria ya bima ya afya kwa wote akisema kuwa hatua hiyo itaongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya Watanzania walioko kwenye mfumo wa bima ya afya.

“Kampuni za bima zinazotoa huduma za afya zimejipanga vizuri na zina dhamira ya kuhakikisha ajenda ya hii inawafikia wananchi wengi iwezekanavyo,” amesema Awando.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima  ya  Afya(NHIF) Mkoa wa Kinondoni, Rafael Malaba ameweka wazi kuwa NHIF tayari imezindua vifurushi mbalimbali vya bima kwa ajili ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.

“Utekelezaji tayari umeanza, tumeandaa vifurushi mbalimbali vinavyolenga makundi tofauti ya jamii,” amesema Malaba.