Mtaalamu ashauri ruzuku iwepo kushughulikia bima ya afya kwa wote

Muktasari:
- Rais Samia Suluhu Hassan alitia saini katika Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na kuwa sheria kamili baada ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Desemba Mosi, 2023.
Dar es Salaam. Licha ya serikali kubainisha vyanzo nane vya tozo kuchangia bima ya afya kwa wote kwa wasio na uwezo, mtaalamu ameshauri kuwa ili mfuko uwe na uhimilivu, itengeneze njia ya wengi kuingia kwenye mfumo na kuwa na ruzuku ya mfuko kwa kuweka kodi mahususi zitakazoenda moja kwa moja kwenye matibabu.
Hatua hiyo itasaidia mifumo ya mafao ya bima yaani Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), kuuboresha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na bima za watu wasiojiweza ambazo zitasimamiwa na Mamlaka ya usimamizi wa bima TIRA.
Hayo yamesemwa leo na mtaalamu wa hisabati za bima na fedha, kutoka Idara ya Hisabati UDSM, Dk Agnella Mandia wakati akiwasilisha mada yake kwenye kongamano la kitaifa kuhusu uendeshaji wa bima ya afya Tanzania.
Dk Mandia amesema kutokana na mfumo wa bima unaoendeshwa na mfumo wa wengi kuwachangia wachache, hata wataalamu wanapotengeneza bei za vifurushi vya bima, jinsi watu wanavyokuwa wengi ndivyo vifurushi vinavyozidi kuwa nafuu.
“Ili tusiumize mfuko na uwe ustahimilivu, lakini pia wananchi wengi waweze kuweka malipo ni kutengeneza njia ya watu wengi zaidi kuingizwa kwenye mfumo, hii inaweza kufikiwa kwa Serikali kuweka ruzuku katika mfuko, kwa kuweka kodi mahususi ambazo zitaenda moja kwa moja kwenye matibabu,” amesema.
Amesema Serikali ikiweka mifumo ya bima ambayo inatoa ruzuku kwa maana uchangiaji wa wananchi utakua mdogo hivyo tutafika lengo la kila mwananchi kuwa na bima.
“Kinyume na hivyo namba hazidanganyi kwa maana kama tutakuwa na wachangiaji wachache na hakuna mfumo wa kujazia wale wachache, basi shirika litashindwa kuwa stahimilivu kwa maana watu watashindwa kuchangia, mahitaji yatakuwa makubwa kwa watu sambamba na uchangiaji,” amesema Dk Mandia.
Hata hivyo Dk Mandia amesema serikali kuweka vyanzo nane kuchangia katika bima kwa wasio na uwezo, ni mwanzo mzuri kama vyanzo vyote vikifikia malengo yake, tutakua na fedha itaingia ya kutosha ili wananchi waweza kupata huduma.
Amesema changamoto hayo bado ni mapendekezo, utekelezaji unategemea utayari wa wananchi kutoa kodi ili Serikali ipate hivyo vyanzo na kupeleka fedha hizo.
Akizungumzia viwango vya uchangiaji, Dk Mandia amesema gharama za matibabu ni juu na hicho si kitu cha kuficha kuanzia vifaa, gharama za kusomesha wataalamu, dawa kwa ujumla gharama za sekta ya afya ziko juu.
“Kwahiyo nikiwa mtaalamu natarajia kwamba Serikali haitaweka vifurushi vya juu ili wananchi wasiweze kuchangia, lakini mwisho wa siku mzizi wa tatizo upo kwenye uchangiaji, wananchi wanataka kupata hivi vifurushi lakini Serikali pia inahitaji kuwa na uwezo wa kuendesha vituo vya afya na kutoa matibabu.
“Tukienda kwenye kanuni za kihesabu, kuwa watu wengi wachangie wachache watibiwe tunaongeza wigo wa uchangiaji na pale ambapo itashindikana kabisa wananchi kuchangia, basi serikali itasaidia kuweka ruzuku kwa vyanzo vinginevyo, tutafikia uchangiaji utapungua yaani ada ya bima na kila mtu atakuwa na uwezo wa kupata huduma,” amesema.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Idara ya Hisabati, lilijadili mada isemayo, ‘Mabadiliko ya mfumo wa bima ya afya Tanzania na fursa za taaluma ya hesabu ya bima’.
Akizungumza kwenye mdahalo huo mkuu wa kitengo cha udhibiti majanga NHIF, Rose Temba amesema ili kuingia katika bima ya afya kwa wote lazima muundo wa NHIF uboreshwe na hiyo ndiyo sababu ya kuja na Muswada wa marekebisho ya sheria.
Amesema lengo ni kuoanisha sheria mbili ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023 na ya NHIF ili ziwezi kusomana kwa kuwa maeneo mengi zilikuwa zinakinzana.
“Ukiangalia sheria inayokuja imeongeza wigo kutoka kwa wazazi na watoto kama wategemezi, mpaka kujumuisha ndugu wa damu chini ya miaka 21, pia inafanyiwa marekebisho ili kumtambua Tira kama mdhibiti,” amesema.
Mkurugenzi wa Sera, Tafiti na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Dk Tumainiel Macha amesema hatua za awali za utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote umeshaanza na kwamba idara ya hisabati ya bima ni sekta muhimu ili kuhakikisha mfuko huo unasimama.
Amesema katika idadi ya watu milioni 62 nchini ni asilimia 8 pekee ndiyo wenye bima ya afya, hivyo mfumo unaokuja sheria inamlazimisha kila mtu awe katika mfumo wa bima na kwa kuwa kila sekta itatakiwa kuingia, hisabati ya bima ni muhimu.
“Serikali imeangalia huo mfumo unawezaje kufanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu kuangalia mabadiliko ya kimfumo, sheria imeweka wazi kwa wasio na uwezo lazima agharamiwe na serikali. Hivyo utekelezaji umeanza na tayari NHIF na TIRA wameanza kufanya marekebisho ya sheria,” amesema.
Mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati amesema uwepo wa bima ya afya ni muhimu, kwnai mpaka sasa asilimia 9 inayokusanywa kutoka katika mifuko ya bima ndiyo inayohudumia sekta ya afya.
“Tunategemea tuendako tutakuwa na mfuko mkubwa zaidi utakaosaidia wananchi kwa wingi, Tanzania fedha nyingi zinazotibu wagonjwa wa msamaha zinatokana na mapato ya bima. Tunategemea itakuwa fursa kwetu kuendeleza huduma na tunategemea kuwa mfuko utakua mkubwa zaidi,” amesema Dk Osati ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya tafiti za magonjwa ya binadamu- Nimr.
Katika mahojiano maalum maalum yaliyofanywa na Gazeti hili wiki jana na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka alibainisha mwelekeo wa bima ya afya kwa wote utakavyokuwa, huku ukitaja gharama kwa kaya moja ya watu sita itakuwa Sh150,000 sawa na Sh25,000 kwa kila mwanakaya kwa mwaka.
Kifurushi hicho chenye huduma 277, imeeleza kuwa kiongozi wa kaya ataweza kulipia kwa mkupuo au kupitia kampuni ya simu kwa kuanza na Sh14,000 na kisha mtumuaji atakatwa kidogo kidogo mpaka atakapokamilisha Sh150,000 ya kifurushi cha kaya.