Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tathmini ya taasisi Wizara ya Nishati zamkuna Dk Biteko

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewapongeza watendaji wa Wizara ya Nishati na taasisi zake akisema zinaendelea kuimarisha utendaji kazi.

Amesema kwa hatua hiyo, zinaifanya sekta ya nishati kuwa na matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Dk Biteko ametoa pongezi hizo baada ya kufanyika kwa tathmini ya utendaji kazi iliyofanywa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini katika Wizara ya Nishati na kuonesha katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2024/2025, utendaji kazi  wa wizara na taasisi zake umeimarika kwa zaidi ya asilimia 95.

Katika kikao cha nne cha tathmini ya utendaji kazi wa wizara hiyo na taasisi zake kilichofanyika jijini Dodoma leo Jumatano Juni 4, 2025, Dk Biteko amesema tathmini hiyo inasaidia kujiimarisha na hasa ikizingatiwa kuwa sekta hiyo, ina umuhimu mkubwa kiuchumi na kijamii.

“Sekta hii ni muhimu sana nchini kwa kuwa ni ya huduma na sekta ya uchumi hivyo ikilegalega italeta malalamiko, ningependa kuona inaendelea kuwa na matokeo mazuri kwa wananchi,” amesema.

Hata hivyo, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuendelea na kasi ya ukarabati wa miundombinu ya umeme pamoja na kutafuta vyanzo vipya vya umeme.

Aidha, ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kasi iliyofanya ya kuhakikisha vijiji na vitongoji vyote vinapata umeme.

Akizungumzia nishati safi ya kupikia, Dk Biteko amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hususan, REA, TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania) na Tanesco, kuunganisha nguvu katika kutekeleza ajenda hiyo.

Amesema ikiwa ni kutimiza lengo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha wananchi wanahama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi kwenda kwenye nishati safi ya kupikia.

“Nikipongeze kitengo hiki cha ufuatiliaji na tathmini katika Wizara ya Nishati  kwa kutekeleza jukumu lenu kwa ufanisi, nawakumbusha  watendaji wa wizara na taasisi zake hatua hii ya tathmini inapaswa kuwa endelevu kutokana na umuhimu wake katika kuboresha utendaji kazi wenu,” amesisitiza.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amezitaka taasisi zote kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia ili lengo la Serikali la kufikisha asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034 litimie.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema kikao hicho ni cha nne tangu vianze kufanyika.

Amesema tangu kuanza kazi ya kupima utendaji kazi wa wizara na taasisi, wanashuhudia ufanisi hasa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na mipango ya wizara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini  ya Utendaji wa Serikali, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kutekeleza miongozo iliyowekwa na ofisi hiyo ya ufuatiliaji na tathmini.

Amesema wizara hiyo imetekeleza miongozo iliyowekwa kwa asilimia 100 huku akimpongeza Dk Biteko kwa dhamira yake ya dhati katika kusimamia utendaji kazi wa Serikali, hasa sekta ya nishati ambayo anaisimamia.