Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Biteko: Matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka

Muktasari:

  • Kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Dodoma. Naibu Waziri Mkuu Dk Doto Biteko amezindua mkakati wa Taifa wa mawasiliano wa nishati safi ya kupikia  pamoja na kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji na uelimishaji matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuongeza uelewa wa wananchi.

Kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Akizindua mkakati huo wa mawasiliano jijini Dodoma, leo Juni 2, 2025, Dk Biteko ameagiza kuwa mkakati huo usiishie kukaa kwenye makabati bali utekelezwe katika ngazi zote za Serikali hadi ngazi ya mtaa bila kusahau sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kuutekeleza.

Katika uzinduzi huo, Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara namba moja wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi akisema tangu azindue mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024-2034) Mei 8, 2024 matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6 hadi 16.

“Katika kuthibitisha jinsi anavyolipa umuhimu suala hili la nishati safi ya kupikia, mheshimiwa Rais pia ameunda kitengo ambacho kina jukumu maalumu la kusimamia ajenda ya nishati safi ya kupikia na kwa kupitia kitengo hiki Serikali itaendelea na shughuli mbalimbali ikiwamo kubuni na kusimamia miradi, pia kusimamia kampeni zote za kitaifa za uelimishaji na uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia,” amesema Dk Biteko

Dk Biteko ameeleza kuwa, matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia yanaendelea kuathiri afya na maisha ya watumiaji wengi hasa kina mama na watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Amesema taarifa zinaonesha kuwa, watu bilioni 2.1 sawa na asilimia 24.7 ya watu wote duniani hawana nishati safi ya kupikia.

Kati yao watu milioni 990 sawa asilimia 47.1 ya wanaotumia nishati isiyo salama wanatoka barani Afrika.

Ameeleza kuwa, Afrika inalazimika kufunga mkanda katika safari ndefu ya kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo kwa upande wa Tanzania kila taasisi inapaswa kutambua na kutekeleza jukumu lake kikamilifu.

Dk Biteko amewasisitiza wadau wote wanaohusika na nishati safi ya kupikia kuhakikisha wanaandaa na kutekeleza kampeni zinazolenga makundi maalumu katika jamii, kukuza uelewa wa umma kuhusu njia za ufadhili na gharama nafuu, kuhakikisha ujumbe thabiti wenye kueleweka unafika kwa wadau wote na kuendeleza na kuimarisha njia za mawasiliano za kuaminika.

Katika hatua nyingine, ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia kitengo cha tathmini na ufuatiliaji kufanya tathmini katika kila robo mwaka ili kujipima juu ya utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amempongeza Rais Samia kwa kuendelea  kuonesha kuwa nishati safi ya kupikia si suala la maneno bali ni vitendo na ndio maana anatambulika duniani kama kinara wa nishati safi ya kupikia.

Amesema kuwa suala la nishati safi ya kupikia ni kipaumbele cha Mkoa wa Dodoma na  juhudi  mbalimbali zinachukuliwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia akitoa mfano kuwa, kwa Mkoa wa Dodoma kwa sasa tayari magereza tisa yanatumia nishati safi ya kupikia, shule za Veta tatu na shule tisa za bweni huku kazi ya uhamasishaji ikiendelea.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema katika kipindi cha miaka minne sekta ya nishati imekuwa mashuhuri kwa masuala mbalimbali kubwa likiwa ni nishati safi ya kupikia na kueleza kuwa nguvu ya ushawishi ya Rais  Samia imefanya ajenda ya nishati safi ya kupikia kukubalika ndani na nje ya nchi, hivyo kutoa hakikisho la usalama wa afya za wananchi na mazingira pia.

Ameongeza kuwa mkakati wa mawasiliano wa nishati safi ya kupikia uliozinduliwa utaongeza kasi za programu za nishati safi ya kupikia na kuleta mapinduzi ya kuhama kutoka matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kwenda kwenye nishati safi ya kupikia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuzinduliwa kwa mkakati wa Taifa wa mawasiliano wa nishati safi ya kupikia ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Ameeleza kuwa mkakati huo umeandaliwa na  Wizara ya Wizara ya Nishati  kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) na unaongozwa na kauli mbiu ya kitaifa isemayo “Nishati Safi ya Kupikia, Okoa Maisha na Mazingira.”

Amesema lengo kuu la mkakati ni kuongeza uelewa wa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na malengo na kuandaa kutekeleza kampeni maalumu za uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuhakikisha ujumbe wenye lengo la pamoja unafika kwa wadau wote pamoja na kuendeleza na kuimarisha njia za mawasiliano.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo amempongeza Rais  Samia kwa kuanzisha gurudumu la nishati safi ya kupikia, pia amempongeza Dk Biteko kwa jinsi anavyoongoza wizara na kutoa ushirikiano kwa kamati hiyo.

 Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Rodney Thadeus amesema kuwa wizara hiyo itahakikisha mkakati wa mawasiliano uliozinduliwa unatekelezwa kwa mafanikio kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na wadau wengine vikiwemo vyombo vya habari.

Mshauri wa Rais ( Nishati Safi ya Kupikia na Maendeleo ya Jamii) Angellah Kairuki amepongeza juhudi za Serikali katika kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia huku kielelezo mojawapo kikiwa ni uzinduzi wa mkakati wa mawasiliano ambao ni muhimu katika kufikisha ujumbe kwa umma kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Lamine Diallo, Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali kutoka Umoja wa Ulaya ( EU), ameipongeza Wizara ya Nishati kwa tukio hilo muhimu la kuzindua mkakati wa mawasiliano wa nishati safi ya kupikia na kusema kuwa inaonesha kwa vitendo juhudi za Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia nishati safi ya kupikia.