Dk Biteko: Marathoni ni fursa kiuchumi kwa wafanyabiashara

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk, Dotto Biteko (kulia) akiwa ameambatana na Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya mjini, Dk Tulia Ackson (katikati) na msanii wa Bongo Fleva, Nassib Abdul maarufu Diamond Platnumz wakati wa mbio za Mbeya Tulia Marathon 2025 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Picha na Hawa Mathias.
Muktasari:
- Dk Biteko amesema uwepo wa mbio Betika Mbeya Tulia Marathon ni fursa kubwa kwa wafanya bishara, huku akihamasisha umoja na ushirikiano kupitia mashindano hayo.
Mbeya. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dk Dotto Biteko amesema uwepo wa mashindano ya mbio za Betika Mbeya Tulia Marathon 2025 unachangia kukuza fursa za kiuchumi kwa wafanyabiashara Mkoa wa Mbeya.
Dk Biteko, ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Mei 10, 2025 alipokuwa mgeni rasmi wakati wa kufunga mashindano hayo yaliyoanza jana Mei 9, 2025.
Mbali na kufungua mashindano ya mbio hizo, Biteko ameshiriki mbio za kilometa tano akiongozwa na mwenyeji wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa mjini, Dk. Tulia Ackson sambamba na viongozi wa chama na serikali.
Amesema uwepo wa mbio hizo ni fursa kubwa kwa wafanya bishara, huku akihamasisha umoja na ushirikiano kupitia mashindano hayo.

"Kuna watu waliibeza, lakini leo ulizeni wafanya bishara wa Mbeya, fursa wanazopata kupitia mashindano ya Tulia Marathoni? Niwatake kuwa wamoja, lakini pia tunaona kuna mwitikio mkubwa wa ushiriki," amesema.
Wakati huohuo, Dk Biteko, amempongeza Spika Tulia kwa kuandaa mashindano hayo kila mwaka sambamba na kumpatia msanii wa vichekesho, Bosi kimaro kitita cha Sh5 milioni.
"Hongera sana msanii wetu Kimaro kwa mchango wako wa sadaka kwa Wanambeya kuunga mkono mashindano ya mbio za Tulia Marathon kila mwaka," amesema Dk Biteko.
Katika hatua nyingine, Biteko amesema wanamuombea Dk Tulia kuendelea na kazi hiyo kwa kuendelea kuongoza jimbo la Mbeya.
"Mlishafanya huko nyuma na sisi wabunge tulivyofika bungeni kwa Mbunge wenu tulimfanya kuwa Spika. Lakini alipokwenda duniani Mheshimiwa Rais alisema nileteeni mwanangu wa Mbeya,” amesema Biteko.
Kauli ya Dk Tulia
Kwa upande wake Spika wa Dk. Tulia amesema hizo ni mbio za kipekee nchini na ndio maana zimefanyika kwa siku mbili ambapo leo Mei 10, 2020 wameanzia kilometa 42.

"Kwanza niwashukuru wadau kwa kuungana nasi katika nia njema ya kuboresha miundombinu ya elimu na afya lakini tuishukuru serikali kwa kuboresha sekta ya afya nchini," amesema.
Dk Tulia amesema katika kuunga mkono jitihada za serikali kwa mwaka huu, wametoa bima za afya kwa wananchi 9,000, na kuwezesha mahitaji kwa watoto kutoka kaya maskini zikiwepo sare za shule na madaftari.
"Nimeanza kuwashukuru wananchi. Walijiandikisha kushiriki mbio hizi kwani ni sehemu ya mchango wa kusaidia watoto mazingira magumu kupata vifaa vya shule kama sare na madaftari," amesema.
Katika hatua nyingine amesema wanagusa kaya za wazee wasiojiweza kwa kuwajengea makazi bora na mahitaji mengine kama chakula na mavazi.
Dk Tulia amesema kupitia mashindano hayo wamejitokeza wadhamini mbalimbali ikiwepo kampuni ya Betika na Wasaf na Taasisi mbalimbali za kifedha.
Mashindano hayo yameshirikisha mbio za uwanjani za mita 1,500-800-400-200-100 na mita 50 kwa watoto kwa mbio za uwanjani, huku kwa mbio za barabarani ilianzia mita 42.
Naibu Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema msimu huu mashindano yamekuwa na mwamko mkubwa wa ushiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini.
"Binafsi nimekimbia kilometa tano, lakini pia nimewezesha vijana zaidi ya 27 kushiriki mashindano hayo,” amesema Mahundi.