Dk Biteko akerwa kasi ya watoto wa mitaani, wazazi kukwepa majukumu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiwa amembeba na kusalimiana na mwanafunzi wa Shule ya msingi Wounder Kid Academy mara baada ya kuwasili katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia iliyofanyika leo Mei 24, 2025 katika Ukumbi wa Rocky City Mall jijini Mwanza
Muktasari:
- Dk Biteko amesema jambo hilo ni aibu kwa wazazi kwani wanapaswa kuvumiliana kujenga familia imara, wakishindwa kulea vizuri watoto wanajiandalia upweke uzeeni.
Mwanza. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amesema kasi ya ongezeko la watoto wa mtaani nchini linatokana na wazazi kushindwa kuwajibika kwa kutelekeza watoto wao, kukwepa malezi na kutothamini umuhimu wa mtoto, huku akiwataka wazazi kila mmoja kumlea mtoto wake na kuacha visingizio vya kubanwa na majukumu mengi.
Dk Biteko ameyasema hayo leo Mei 24, 2025 jijini Mwanza wakati akizungumza katika Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Familia, alipomwakilisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, yaliyofanyika Ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza.
Wito huo wa Dk Biteko umekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda kutoa takwimu mbalimbali za mashauri 3,534 yaliyopokelewa na idara ya ustawi wa jamii mkoani Mwanza kwa mwaka 2024/2025 yakiwemo 1,586 ya matunzo ya watoto, 980 ya ndoa na 770 ya matunzo kwa watoto waliozaliwa nje ya ndoa.
Dk Biteko amesema jambo hilo ni aibu kwa wazazi kwani wanapaswa kuvumiliana kujenga familia imara kwani wakishindwa kulea vizuri watoto wanajiandalia upweke uzeeni.
"Nimemsikia Mkuu wa Mkoa wakati anazungumza juu ya changamoto tulizonazo za kuwa na watoto wanaoitwa wa mtaani ambao kwa kweli hakuna mtaa unaozaa mtoto bali ni watoto wa watu ambao wazazi wao wameacha wajibu wao kwa namna moja au nyingine," amesema.
Amewataka wazazi hususan watumishi wa umma kuacha visingizio vya kubanwa na majukumu na kushindwa kutenga muda wa kukaa na watoto wao ili kuwarithisha tamaduni nzuri.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ( Mwenye tai nyekundu) akiwa na viongozi wa dini, wakionesha nakala za mwongozo wa malezi kwa watoto wadogo ulioandaliwa kwa ushirikiano wa viongozi wa dini na kuzinduliwa ikiwa ni sehemu maadhimisho ya siku ya familia.
“Kila mwanafamilia achukue nafasi yake ya kulea watoto wake, inawezekana tuna kazi nyingi za kufanya lakini ni muhimu kutenga muda hata kama ni kidogo kukaa na watoto ili kuwarithisha mila na desturi tunazozifahamu. Tunawajibika kwa namna moja au nyingine kwa kila mtoto ama mwanafamilia tuliyenaye kumpa malezi ili na yeye kesho awe na familia iliyo bora na kujenga taifa imara,” amesema.
Ameongeza kuwa; “Wakati mwingine tunaweza kulaumiana ni nani mbaya hili si muhimu kwa sasa ni wajibu wa jamii yote kujua kwamba familia ni msingi wa jamii yoyote, tuvumiliane tujenge familia imara.”
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema katika mwaka 2024/2025 idara ya ustawi wa jamii ilipokea mashauri 3,534 ikiwemo migogoro 980 ya ndoa, jambo linaloashiria uwepo wa migogoro hiyo umekuwa na madhara makubwa katika malezi na makuzi ya watoto ambao wengi huishia mitaani.
Amesema mkoa huo unao watoto wa mitaani zaidi ya 1,000 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa waliozikimbia familia zao kutokana na migogoro ya ndoa, ambapo mkoa huo umeshazindua mkakati maalumu wa malezi na makuzi ambao unaeleza namna ya kudhibiti ukuaji wa watoto wa mitaani ili wasiwe tishio miaka ijayo.
“Mwaka 2023/2024 tulipokea mashauri 1,586 yanayohusiana na matunzo ya watoto, migogoro 770 ilihusu matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa. Wito wangu tuendelee kupunguza hili suala la kuzaa nje ya ndoa kwa sababu dini zinakataza na ukiacha hata hii migogoro haitakuwepo,” amesema Mtanda.
Mtanda amesema watumishi wa umma wana changamoto za malezi na makuzi ya watoto wao kwani wamewekeza nguvu nyingi kwenye mafunzo na semina za ofisini kwao kuliko watoto wao.
“Miongoni mwa changamoto za malezi na makuzi pia watumishi kujisahau, wengi wana semina nyingi za lishe, malezi na makuzi kwahiyo wanasahau kulea na kushiriki katika malezi na matunzo ya watoto wanawaachia wasichana wa kazi kwa asilimia kubwa, kwahiyo kazi yao ni kutembea tu na fimbo na kufanya ufuatiliaji kwa mbali,” amesema Mtanda na kuongeza;
“Pamoja na semina na mikutano mingi ambayo tunaenda tusisahau malezi na makuzi tufuatilie familia zetu na malezi yetu, tusipofanya hivi tunajiandaa kuwa wapweke tutakapokuwa wazee kwa sababu hakutakuwa na muunganiko baina yetu na watoto wetu na hawatajua kwamba sisi tulibanwa na shughuli za lishe kule Dodoma.”
Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis amesema maadhimisho hayo yanalenga kutathmini nafasi ya familia katika malezi ya watoto ambao ndio msingi wa familia yeyote na Taifa kwa ujumla.
“Akina mama na akina baba washirikiane kwa pamoja kulea watoto ili wawe na malezi bora, wapate elimu na huduma zingine muhimu kwao,” amesema Mwanaidi.
Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, John Jingu John Jingu amesema mkutano huo umeazimia mambo matano ambayo ni kueneza vituo vya malezi na makuzi ya watoto kote nchini, kwani kwa sasa vilivyopo ni 4,178, pia kuimarisha huduma za utambuzi za mapema za watoto wenye changamoto mbalimbali hususan watoto wenye ulemavu ukiwemo ulemavu wa mtindio wa ubongo ili kuwasaidia kupata huduma za mapema.
“Mengine ni kukuza matumizi ya Tehama katika kuimarisha masuala ya malezi na makuzi ya watoto ili kuwasaidia wazazi na watoto kushirikiana, kuimarisha ushirikiano na taasisi za dini na za kimila ili kuimarisha malezi na makuzi kwa kuzingatia tamaduni zetu zilizo chanya na zile ambazo ni hatarishi tunaachana nazo. Tano, ni kuongeza idadi ya watoa huduma za malezi na makuzi ya watoto ngazi ya jamii wenye uwezo,” amesema Jingu.
Akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Laximi Bhawan amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuweka mikakati ya kusaidia malezi ya watoto.
Aidha, pamoja na Maadhimisho hayo, Dk Biteko amezindua miongozo ya afua za utekelezaji wa malezi na matunzo ya watoto na familia, kutambua mchango wa wadau kwenye malezi na ustawi wa familia na kuzindua kampeni ya malezi kwa mtoto.