Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali imefungua milango kusaidia watu watakaoshindwa kulea watoto

Muktasari:

  • Waziri Dk Gwajima amesema kuwa mpango huo utasaidia kupunguza vitendo vya hasira vinavyowasababisha baadhi ya wazazi kuwatupa au kuwatelekeza watoto mitaani.

Dodoma. Serikali imefungua milango kwa Watanzania wanaokabiliwa na changamoto ya kulea watoto wao, ikiwataka kuwapeleka kwa utaratibu maalum ili waweze kupokelewa na kulelewa badala ya kuwatelekeza mitaani au kuwatupa.

Mpango huo unalenga kuwahudumia wanandoa waliofarakana pamoja na wazazi waliotelekezwa na wenza wao katika suala la matunzo ya watoto.

Hata hivyo, mpango huo umeweka ahueni kwa wahusika kwa kuwa wataruhusiwa kurejeshewa watoto wao endapo watathibitisha kuwa wana uwezo na mazingira bora ya kuwalea.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima, ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Mei 8, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia, yatakayofanyika Mei 15, 2025.

Hata hivyo, Waziri ametaja kuwa sharti la msingi ni kwamba watoto hao watapokelewa baada ya uchunguzi kufanyika na Serikali kujiridhisha kuwa wazazi wote wawili wameshindwa kuwalea katika kipindi husika.

Hii ni mara ya kwanza kwa Serikali kutoa kauli hadharani kwamba iko tayari kuwapokea watoto wanaopelekwa kwa hiari na wazazi wao ili watunzwe, ingawa kwa muda mrefu jukumu la kuwatunza watoto waliokutwa katika mazingira magumu limekuwa likitekelezwa na taasisi mbalimbali za ustawi wa jamii.

Dk Gwajima amesema kuwa badala ya baadhi ya watu kuwatelekeza watoto wao wanapokumbwa na migogoro ya kifamilia, ni vyema wakajua kuwa jukumu la malezi linaweza kushirikishwa na Taifa.

“Wanandoa wanaposhindwana, wengine huamua kuwatelekeza watoto wao. Napenda kuwajulisha kuwa Serikali iko tayari kuwapokea watoto hao na kuwapeleka katika makao maalum ya malezi,” amesema Dk Gwajima.

Dk Gwajima ameongeza kuwa hadi sasa, Tanzania ina jumla ya vituo 388 vya kulea watoto, na zaidi ya watu 2,000 wanaojitolea kuwahudumia watoto hao katika vituo hivyo.

Akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani, Waziri amesema yana lengo la kuhamasisha na kuwakumbusha wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa malezi, kwani ni jukumu lisiloepukika kwa kila mzazi au mlezi.

Dk Gwajima, amewaomba viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha malezi bora, akieleza kuwa viongozi hao huishi na jamii kwa karibu na wana nafasi kubwa ya kusikilizwa na kuaminiwa.

Amesema chanzo kikuu cha watoto kutelekezwa ni kupungua kwa upendo na hofu ya Mungu miongoni mwa wanandoa, jambo linalosababisha ndoa kuvunjika na watoto kuishia mitaani.

Kwa mujibu wa Dk Gwajima, Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani yatapendeza zaidi iwapo kila familia itashiriki kwa pamoja na watoto wao ili kujenga utamaduni wa kusikilizana, kupeana muda na kukuza misingi ya malezi bora.