Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UCHAMBUZI WA MJEMA: Enock umekufa kifo cha kikatili, damu yako itumike kuimarisha utawala wa sheria

Mauaji ya kikatili ya kijana Enock Thomas Mhangwa wa mkoani Geita, yanaumiza, yanahuzunisha, yanaudhi na yanatia hasira, lakini ukweli tumefika hapo kama Taifa kwa sababu ya baadhi yetu kutojali wala kuheshimu misingi ya utawala wa sheria.

Yaani tumefikia mahali watu wanaua kijana mdogo kama Enock asiye na hatia na wanapata ujasiri hadi wa kujirekodi hatua kwa hatua wakifanya unyama ule, na wala hili si tukio la kwanza watu kujirekodi wakifanya uhalifu wao.

Tukio hili la Enock ninalifananisha na la mwaka 2000 la mfanyabiashara Jaffar Abubakar, maarufu JJ wa mjini Moshi, alimuua kijana Peter Swai, kwa kumchoma moto kwa kumsingizia kuiba Sh150,000 tukio ambalo halikuwa la kweli.

Kiufupi, shemejiye JJ aitwaye Haruna Yusuph alifika Moshi kwenye harusi ya mdogo wake JJ iliyohudhuriwa na mkuu wa Jeshi la Polisi wakati huo, na maofisa wengine wa juu wa jeshi hilo wakiwamo wakuu wa vikosi na makamanda wa mikoa.

Haruna alifikia katika lodge (nyumba ya kulala wageni) ambayo Peter Swai alikuwa ni meneja, usiku wa sherehe aliutwika sana na aliporudi chumbani aliamua kuficha fedha hizo ndani ya mto alioulalia, lakini asubuhi alipoamka hakukumbuka alikoficha pesa zake.

Akalalamika ameibiwa na kumchukua meneja hadi nyumbani kwa JJ na kueleza mkasa wa kuibiwa, bila kutafakari, JJ alimfunga kamba mikono meneja huyo na kumtuhumu ndiye aliyeiba, kumwagia mafuta na kumlipua akaungua asilimia 75.

Lakini polisi walipokwenda kufanya upekuzi katika chumba hicho, wakakuta zile pesa chini ya mto, lakini haikusaidia kwani Peter alifariki dunia. Mpaka leo JJ na shemejiye wanatafutwa baada ya Mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwao.

Nasema tukio hili halina tofauti na la Enock kwa sababu ukizitizama video zile, licha ya kukana kuhusika na wizi ule wa laptop, hakusikilizwa badala yake watesi wake waligeka waendesha mashitaka na mahakama na kumuhukumu kifo.

Utawala wa sheria ni nini? Kwa lugha ya kawaida kabisa, ni kwamba hakuna mtu aliye juu, au nje ya mamlaka ya sheria, kuanzia Rais wa nchi mpaka mimi mnyonge niliye hapa, kuanzia Dola ya nchi mpaka kaya iliyopo kwenye kijiji kidogo kabisa.

Maana yake kila chombo cha Dola, kila taasisi, kila mtu anawajibika kwa sheria na kuwajibika kwa sheria maana yake kama ni mhalifu mpeleke polisi, wachunguze na kumfikisha mahakamani ili iamue kama kweli ni mwizi ama la na kumwadhibu au kumwachia huru.

Jaji Mkuu wa Uingereza, Sir Edward Coke, kwenye mwaka 1607, aliamua kesi dhidi ya Mfalme wake, James wa Kwanza.

Kesi yenyewe ilihusu uwezo wa mahakama ya kidini kutoa uamuzi wa sheria za dini, badala ya Mfalme kuwa ndiye hakimu katika mahakama hizo.

Kwa mara ya kwanza katika desturi za sheria za Kiingereza, Jaji Mkuu alitamka kwamba Mfalme yuko chini ya sheria. Alisema na alitumia maneno Quod rex non debet esse sub homine, sed sub Deo et lege.

Akiwa na maana kwamba Mfalme hayuko chini ya mamlaka yoyote, ila tu mamlaka ya Mungu na ya sheria. Mfalme James alighadhabika sana kusikia kwamba yuko chini ya sheria na akatamka kwamba huo ulikuwa uhaini, na papo hapo akamfukuza kazi Jali Mkuu Coke.

Baadaye, mwaka 1628, Bunge la Uingereza lilipitisha muswada wa kuunga mkono msimamo wa Jaji Coke na kuanzia hapo Uingereza na sasa karibu nchi zote duniani zimekuwa zikishika mtazamo huo kwamba hakuna binadamu au taasisi yoyote iliyo juu ya sheria.

Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu linatahadharisha kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, uonevu na ukandamizaji ambayo hutokea pale ambapo hakuna utawala wa sheria.

Watawala wasipoheshimu sheria na kuzizingatia katika kila hatua, uamuzi wanaochukua, basi kama tangazo la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa linavyosema, fujo na maasi ya raia huwa ndio matokeo ya dhambi hii.

Hatusemi kwamba Tanzania tumefika huko, la hasha, lakini tukiacha utaratibu huu uendelee ambapo baadhi ya viongozi na wananchi wanatenda mambo nje ya sheria na wanaangaliwa tu au wanakingiwa kifua ni jambo la hatari sana.

Hivi kiongozi anatamba kabisa kuwa katika uchaguzi mkuu 2020 yeye ndio alikuwa ‘anaua’ watu porini ili CCM ishinde, au anatamka kuwa ushindi hautegemei sanduku la kura, lakini wote hawa hawakuwahi kushtakiwa kwa uchochezi.

Upungufu wa hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahalifu umesababisha watu kuamua kujichukulia sheria mikononi mwao na "kuwaadhibu" wale wanaotuhumiwa kwa uhalifu... tusiwafikishe Watanzania huko.

Tunaona mchana kweupe kibaka akichomwa moto na watu wanaoitwa wenye hasira kali. Hakuna anayeshangaa! Hakuna anayekemea, hakuna anayekataza. Watu kuumizana na hata kuuana kwa madai ya ardhi au fedha ni jambo la kawaida.

Kwa nini? Kwa vile madai yanapoletwa mahakamani yanachelewa sana kutolewa uamuzi, au kwa vile uamuzi wa madai unapatikana kinyume na haki na kinyume na sheria na baadhi ya maamuzi hayaakisi uhalisia wa tukio lenyewe.

Uimarishwaji wa utawala wa sheria utatokana pia na sheria zenyewe. Kwa maneno rahisi, sheria nazo lazima zifuate ‘sheria’. Sheria kandamizi hazina uhalali wa kisheria. Sheria zinazokiuka Katiba ya nchi hazina uhalali wa kisheria.

Kwa hiyo hatujachelewa, turudi kwenye misingi ya kuheshimu utawala wa sheria, kwa sababu sheria ni kama msumeno hukata mbele na nyuma bila woga na wote mnaoona matendo mabaya mnakaa kimya nanyi ni wahalifu.

Kifungu cha 22 cha Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2022 kiko wazi kabisa, kwamba kama unaona tukio la kihalifu linatokea unakaa kimya, huzuii wala kutoa taarifa tena wakati mwingine unashabikia, nawe ni mhalifu kama aliyelitenda.

Yaani unachukua video kijana mdogo anapigwa hadi anakufa? Hii roho ya kinyama hivi tunaitoa wapi?

Tungekuwa tunajali na kuheshimu misingi ya utawala wa sheria, leo hii muuza madini yule wa Nachingwea, Mussa Hamis angekuwa hai na kama tungejali utawala wa sheria, leo hii mzee Ally Mohamed Kibao wa Tanga angekuwa hai.

Lakini tungekuwa tunajali na kuheshimu utawala wa sheria, leo hii naamini tungejua Deusdedith Soka na wenzake na Mdude Nyagali, walitekwa na kupotezwa na genge gani la uhalifu na Polisi wangetupa mrejesho wa upelelezi.

Nasema kama tungekuwa tunajali na kuheshimu kikamilifu utawala wa sheria, wale watu waliokamatwa kwa tuhuma za kuteka na kukata watu masikio kule Jimbo la Vunjo uchaguzi mkuu wa 2020, tungekuwa tumewaona wakiwa gerezani.

Tungekuwa tunajali na vyombo vyetu vya Dola kama Polisi wote wangetekeleza majukumu yao ndani ya sheria na ndani ya Kanuni za Utendaji wa Polisi (PGO), na mahakama zikatoa hukumu za haki, watu wasingejichukulia sheria mkononi.

Mauaji ya Enock yanayodaiwa kufanywa na wale waliopewa dhamana ya kusimamia ofisi za umma, hayana tofauti na mauaji ya Mussa kule Nachingwea, wala hayana tofauti na mauaji yaliyofanywa na Christopher Bageni na wenzake.

Tusipozinduka usingizini, utawala wa sheria utazidi kutepeta kwa sababu tunapoelekea nchi yetu inaelekea kuwa na kundi ambalo linaweza kufanya chochote na lisiwajibishwe kwa kisingizio cha ‘watu wasiojulikana’.

Damu ya Enock isiyo na hatia isaidie kufufua na kuimarisha utawala wa sheria, kwamba kila mtu ajue hayuko juu ya sheria na kwamba ni mahakama pekee ndicho chombo cha kupima nani mwenye haki, tusijichukulie sheria mkononi.