Tanzania, India kushirikiana kuinua sekta za habari, filamu

Muktasari:
- Profesa Kabudi amekutana kwa mazungumzo na Waziri wa Nchi, Wizara ya Habari na Utangazaji wa India, Dk Roganathan Murugan.
Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema mkutano wa kwanza wa kimataifa wa masuala ya habari, filamu na burudani (Waves) umeifungulia Tanzania fursa katika kuendeleza sekta za habari, filamu na burudani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 3, 2025 na wizara hiyo, mkutano huo unaendelea jijini Mumbai, India.
Profesa Kabudi ameeleza fursa hizo baada ya kikao na Waziri wa Nchi, Wizara ya Habari na Utangazaji wa India, Dk Roganathan Murugan.
Mawaziri hao wamekubaliana kufufua upya idhaa ya Kiswahili ya Shirikia la Utangazaji la India la All India Radio kwa kushirkiana na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Hatua hiyo inalenga kukifanya Kiswahili kitangazwe na redio hiyo ya India, hivyo kuwezesha kisikike tena katika Bara Hindi na sehemu zingine duniani ambako redio hiyo inasikika.
“Pamoja na hayo, tumekubaliana kuanza kuwa na ushirikiano wa kiufundi na All Radio India, hasa katika mitambo mipya ya utangazaji redio ya kidijitali ya DRM 30+ wenzetu wa India wapo mbali, tumetembelea maonyesho tumeona jinsi gani India wamekwenda mbali katika teknolojia ya utangazaji na urushaji wa matangazo,” amesema.
Ametaja maeneo mengine ya ushirikiano kuwa ni utengenezaji wa filamu kwa kuangalia jinsi gani mataifa hayo yaweza kushirikiana kuzitengeneza, maudhui ya filamu na kuzisambaza za Tanzania nchini India na za India kuendelea kununuliwa na kutumiwa nchini.

Profesa Kabudi amesema eneo lingine ambalo Tanzania inahitaji kulitumia ili kuhakikisha soko lake la filamu linasambaa India ni kuweka maneno ya tafsiri ya Kihindi na Gujirati kwenye filamu zinazotengenezwa Tanzania ziweze kuuzika katika taifa hilo.
Pia kuangalia taasisi mpya ya India inajihusisha na sanaa bunifu itakavyoweza kuchukua wanafunzi kutoka Tanzania.
“Chuo hicho ni kipya na kinasisitiza matumizi ya teknolojia kuendana na mazingira ya nchi ambazo zinahitaji teknolojia hiyo,” amesema.
Waziri amesema kuna umuhimu wa wasanii wa Tanzania kutumia fursa hiyo ya mafunzo na tafiti katika kuimarisha na kuboresha kazi za sanaa.
Amemueleza Dk Murugan kuhusu uzuri wa Tanzania, akiwakaribisha watengeneza filamu kutoka India kutumia maeneo ya kimkakati nchini kama vile Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro na Zanzibar kurekodi filamu.
Pia amewaalika watu mashuhuri nchini humo wakiwamo waigizaji na watengeneza filamu kutembelea Tanzania kuangalia maeneo watakayoshirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania.
“Tumewakaribisha katika maonyesho yetu ya filamu ya kila mwaka ya Zanzibar International Film Festival (ZIFF) na Sinema Zetu. Wao wametualika katika maonyesho yao ya sinema yanayofanyika mwishoni mwa Novemba,” amesema.
Waziri na ujumbe wake walitembelea eneo maarufu la Bollywood ambalo hutumika kutengeneza filamu.