Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Takukuru kuwafikisha kortini ‘wanaohujumu’ miradi

Mkuu wa Takukuru Wilaya ya Kinondoni, Ismail Seleman akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, imesema mara baada ya uchunguzi kukamilika, itawafikisha mahakamani, watuhumiwa ubadhirifu miradi ya maendeleo wilaya za Ubungo na Kinondoni.

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, imesema mara baada ya uchunguzi kukamilika, itawafikisha mahakamani, watuhumiwa ubadhirifu miradi ya maendeleo wilaya za Ubungo na Kinondoni.

Kauli hii inatokana na taasisi hiyo kubaini mapungufu katika miradi tisa ya maendeleo yenye thamani ya Sh 72 bilioni katika wilaya hizo.

Mapungufu hayo ni kutokana na wasimamizi kutofuata kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa kwenye mikataba.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 16, 2023 jijini Dar es Salaam Mkuu wa Takukuru mkoa huo, Ismail Seleman, amesema wanaendelea na uchunguzi baada ya kubaini mapungufu katika miradi hiyo.

Amesema msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Mabwepande wenye thamani ya Sh268 milioni, hakuwa na sifa wala vigezo, kama ilivyoainishwa kwenye mwongozo wa ujenzi, na kwamba mradi kufanywa chini ya kiwango.

"Tumebaini miradi mingi haifuati miongozo yake hivyo tunafuatilia kwa karibu na uchunguzi ukikamilika tutawafikisha sehemu husika," amesema Seleman.

Pia Selamani amesema kutokamilika kwa ujenzi wa madarasa 12 ya Shule ya Sekondari Boko, wenye thamani ya Sh650 milioni, umesababishwa na ucheleweshwaji wa fedha kutoka kwenye vyanzo vya mradi ambao ulitakiwa kukamilika Desemba 2021.

 "Tumemshauri msimamizi kufuatilia kwenye vyanzo vya fedha ili ujenzi ukamilike na madarasa yaanze kutumika ili kupunguza uhaba wa madarasa," amesema.

Kwa upande mwingine, bosi huyo wa Takukuru Kinondoni, amezungumzia ujenzi wa mabweni matano ya shule ya Wasichana Wilaya ya Ubungo, wenye thamani ya Sh3 bilioni, kutokukamilika kutokana na mkandarasi wa kwanza kusaini mkataba wa bweni moja badala ya matano.

"Menejimenti imeshindwa kuwajibika ipasavyo katika usimamizi wa mradi huu na kupelekea kujengwa kwa mabweni matatu badala ya matano ufuatiliaji unaendelea kuhakikisha mradi unakamilika kwa kuzingatia thamani ya fedha," amesema Selemani.

Hata hivyo, Selemani amesema kupanda kwa bei ya baadhi ya vifaa vya ujenzi umesababisha uchelewaji wa malipo ya mafundi katika mradi wa ujenzi wa sekondari Msakuzi wenye thamani ya Sh470 milioni.

Na mapungufu katika ujenzi wa madarasa matatu ya shule ya Sekondari Yusuph Makamba wenye thamani ya Sh60 milioni ulitokana na kukosekana kwa kamati ya mapokezi na manunuzi.

"Kulikuwa na kamati ya ujenzi ambayo ilisimamia na kufanya manunuzi wa vifaa na mapokezi jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya mwongozo wa ujenzi wa miradi ambayo yameainisha majukumu ya kamati hizo," amesema.

Miradi mingine ni ya barabara ambazo zinafanyiwa matengenezo ikiwepo Vijana, Posta Matembo, Midizini, Mbezi Makabe, Millenia ya tatu na King'ongo.

Amesema mkandarasi amelipwa Sh341 milioni tofauti na kiasi kilichoandikwa katika mkataba alioingia ambao ulikuwa wa Sh346 milioni hivyo kubaki Sh6.4 milioni ambazo hazikutumika katika mradi huo.

"Tumeomba ufafanuzi kutoka kwa Tarura juu ya kiasi hicho kilichobaki na kimetumika vipi," amesema.