Takukuru yabaini ‘madudu’ Kinondoni

Naibu Mkuu wa Takukuru wilaya ya Kinondoni, Elizabeth Mokiwa
Muktasari:
- Takukuru imebaini kucheleweshwa kwa mradi wa ujenzi wa jengo la Manispaa ya Kinondoni pamoja na Shule ya Sekondari Godwin Gondwe, yaanza uchunguzi.
Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imesema imebaini ucheleweshwaji wa ujenzi wa jengo la utawala la Manisapaa ya Kinondoni.
Akizungumza leo na waandishi wa habari wakati akitoa ripoti ya miezi mitatu ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kupitia programu ya Takukuru Rafiki, Naibu Mkuu wa Takukuru Kinondoni Elizabeth Mokiwa amesema Taasisi yake inafuatilia kwa karibu.
Akielezea ripoti hiyo amesema mradi wa jengo la Utawala la Manispaa ya Kinondoni wenye thamani ya Sh3.2 bilioni umechelewa kwa miezi minne zaidi tofauti na mkataba unavyojieleza, huku kukiongezeka kwa kazi zingine ambazo hazikuwepo kwenye mkataba.
"Ufuatiliaji unaendelea kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha," amesema Mokiwa.
Akizungumzia matokeo mengine ya ripoti hiyo amesema imebainika kutokuwepo kwa uwazi na ushirikishwaji kwa wadau katika matumizi ya fedha zinazotokana na ushuru na tozo za masoko.
Hivyo Takukuru wametaka kila soko Mkoa wa Kinondoni kuwa na menejimenti yake ambayo itatoa elimu kwa wadau wa masoko na kuwepo kwa uwazi wa matumizi yatokanayo na ushuru wa soko.
Pia amesema kuna uwezekano wa kufanyika kwa vitendo vya rushwa kwa viwango vya juu katika usafirishaji wa mazao ya misitu katika vizuizi vya ukaguzi wa mazao.
"Tumekubaliana kufanya kikao cha pamoja na uongozi wa serikali za mitaa na wakala wa misitu ili kujadili matokeo ya uchambuzi na kuweka maazimio ya pamoja ya kuziba mianya ya rushwa na changamoto nyingine zilizobainika," amesema Mokiwa.