Takukuru, DCEA zaunganisha nguvu

Muktasari:
- Takukuru, DCEA zaunganisha nguvu kupambana na rushwa na dawa za kulevya kwa kutoa elimu kuanzia ngazi za shule za msingi hadi vyuo vikuu wakilenga kuzuia watu wasijihusishe na makosa hayo kuliko kusubiri kuwakamata.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya taasisi hizo katika kuzuia vitendo vya rushwa na dawa za kulevya kupitia klabu za zilizopo shule za msingi, sekondari na vyuoni.
Taasisi hizo kwa pamoja zimekubaliana kutumia rasilimali walizonazo kuwahamasisha wanafunzi, vijana na jamii kwa ujumla kutoshiriki vitendo vya rushwa na biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na mambo hayo.
Akizungumza baada ya kuingia makubaliano hayo Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema ushirikiano baina ya taasisi hiyo utawezesha rasilimali chache kutumika kutatua changamoto mbili kubwa zilizopo kwenye jamii.
Amesema makosa yanayoshughulikiwa na taasisi hizo ni ya kupangwa na vita dhidi ya makosa hayo yana upinzani mkubwa kwenye jamii kwa kuwa yanaleta faida kwa wanayoyatekelezea.
“Nimefurahi tumeunganisha nguvu tutatumia rasilimali chache kushughulika na changamoto kubwa mbili tulizonazo kwenye jamii. Ushirikiano huu utawezesha elimu kutolewa, vijana watajengewa hali ya uzalendo na kuijenga jamii kuchukia matendo ya rushwa na dawa za kulevya hivyo kuibua chachu ya maendeleo kwa Taifa.
“Mamlaka yetu inaahidi kushirikiana kikamilifu katika kuisimamia na kuimarisha vita dhidi ya rushwa na dawa za kulevya na tutaendelea kushirikiana kuhakikisha jamii inaelewa madhara ya rushwa na dawa za kulevya,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Mkurugenzi wa Takukuru, Kamishna Salum Hamdun amesema ushirikiano wa taasisi hizo unalenga kuwekeza nguvu kubwa katika kuzuia kuliko kukamata kwa kuwa hatua ya ukamataji huwa inakuja pale nguvu ya kuzuia inaposhindikana.
‘‘Tuna matarajio makubwa baaada ya kusaini makubaliano haya kwani nguvu yetu ya kudhibiti dawa za kulevya na rushwa itaongezeka na kufanya jamii ya Watanzania kuwa salama,’’ amesema Hamduni.