Takukuru, GGML washirikiana kudhibiti rushwa

Katibu Tawala Mkoa wa Geita Mohamed akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa kupinga vitendo vya rushwa lililoandaliwa na mgodi wa GGML kwa kushirikiana na Takukuru
Muktasari:
- Kongamano hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Takukuru na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), likiwa na lengo la kujadili mbinu bora za kuzuia na kupambana na rushwa, hasa katika maeneo yanayozunguka migodi na sekta nyingine mbalimbali.
Geita. Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema kuwa rushwa ni janga linalodhoofisha haki, maendeleo na usawa katika jamii na kusababisha kuzorota kwa huduma za kijamii, kushindwa kwa ukuaji wa uchumi, pamoja na kuathiri mazingira ya uwekezaji.
Akizungumza leo, Mei 14, 2025, wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa mapambano dhidi ya rushwa lililoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML), Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati amesema kuwa maeneo yenye viashiria vya rushwa hurudisha nyuma juhudi za maendeleo na kuathiri ustawi wa jamii kwa ujumla.
Amesema vita dhidi ya rushwa si jukumu la Takukuru pekee bali ni la kila Mtanzania hivyo ni wajibu wa wananchi kwa pamoja kushirikiana kuitokomeza.
“Rushwa inaathiri huduma, inaua haki, inaua usawa na inaua maendeleo. Tusiposhirikiana kuikomesha, tutabaki kulalamika bila mafanikio. Tuwe wakweli na wazi, tushirikiane kugundua, kuzuia na kuchukua hatua,” amesema Gombati.
Amesema yapo malalamiko yanayotolewa na wananchi wanaoomba kazi au zabuni kwenye mgodi, lakini mengi yanatokana na wao kutoelewa taratibu za uendeshaji wa shughuli za migodi.
Amesema kupitia warsha hiyo, wananchi watapewa elimu ya mchakato wa ajira, utoaji zabuni na namna bora ya kushiriki bila kutoa rushwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Duran Archery amesema rushwa siyo tishio tu kwa biashara bali pia kwa ustawi wa jamii nzima.
“Hupunguza imani ya wananchi kwa taasisi, huvuruga maendeleo,hatuwezi kufanikisha mapambano haya bila kushirikiana,” amesema.

Archery amesema GGML kwa kushirikiana na Takukuru wamepanga kufanya mikutano 28 ya ngazi ya vijiji na mitaa pamoja na vipindi vya redio ili kupeleka elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa na hatua za kuikabili.
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, James Ruge amesema kuwa kongamano hilo limewakutanisha wadau kutoka taasisi za Serikali, mahakama, benki, viongozi wa dini na mashirika ya kiraia ili kujenga mikakati ya pamoja ya kuzuia na kudhibiti rushwa.
Amesema lengo li kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika ujenzi wa mfumo usio na rushwa na kwamba katika kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka huu taasisi hiyo imekusudia kukomesha dalili na vitendo vyote vya rushwa kwa washiriki.
“Katika kampeni hii tunashirikiana na GGML kwa kuwa wao wanatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya CSR na sisi kwenye eneo hilo tunahusika kwenye ukaguzi kuhakikisha utekelezaji wa miradi unaenda sambamba na thamani ya fedha iliyotolewa kutekeleza mradi,” amesema Ruge.