Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chadema yataka hatua madai vigogo kuhongwa na Acacia

Dodoma. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemwangukia Rais Samia Suluhu Hassan, kikiomba awachukulie hatua za kisheria watendaji wa Serikali waliotajwa kwenye baruapepe wakihusishwa na madai ya rushwa kutoka iliyokuwa kampuni ya uchimbaji dhahabu nchini ya Acacia.

Pia wameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria maofisa na watendaji waliohusishwa.

Mkurugenzi wa Takukuru, Salum Hamduni alipotafutwa na Mwananchi jana kuhusu madai hayo ya Chadema alisema: “Kwa kweli sina majibu ya moja kwa moja kwa sasa na Takukuru inashughulika na mambo mengi sana, mitandao ya kijamii ni moja ya vyanzo vya taarifa, kwa hiyo sina jibu la moja kwa moja”.

Hata hivyo, alisema atafuatilia taarifa hizo.

Madai hayo yalitolewa jana na msemaji wa sekta ya nishati na madini wa Chadema, John Heche alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa akionyesha nyaraka hizo (baruapepe).

Heche, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alipoulizwa iwapo wataziwasilisha nyaraka hizo Takukuru, alisema, “Nyaraka hizi zipo kila sehemu. Takukuru ni jukumu lao kuzichukua na kuzifanyia kazi.”

Alisema: “Jinai haifi, Chadema tunasubiri tukiingia madarakani tutazianzisha hizi kesi za jinai hata kama watakuwa wamestaafu. Tutawafuata hukohuko”.

Heche alidai baruapepe hizo zinathibitisha kuwapo kwa mtandao mkubwa wa kihalifu uliowahusisha baadhi ya viongozi na watendaji serikalini.

“Mtandao huo haramu unafanikisha wizi mkubwa wa dhahabu mgodini Nyamongo, huku wananchi wa eneo hilo wakisingiziwa kuwa ndio wezi na kuuawa au kujeruhiwa na walinzi wa mgodi,” alisema na kuongeza:

“Kwa sababu ya wizi uliokuwa unafanywa na mtandao huo, Barrick Gold (Kampuni iliyonunua hisa za Acacia) ililazimika kuajiri kampuni ya masuala ya kiusalama ya ‘Europe Conflict and Security Consulting Ltd’ ili kuchunguza kilichokuwa kinaendelea mgodini Nyamongo. Kampuni hiyo ilitoa taarifa ya uchunguzi wake Novemba 17, 2017.”

Alidai mtandao huo ndio uliohusika pia kutayarisha taarifa za kughushi za uthamini wa ardhi kwa ajili ya ulipaji wa fidia, na kusababisha mgodi kushindwa kuwalipa wananchi fidia kutokana na ughali wa ardhi.

Heche alidai baruapepe hizo zinathibitisha, Mgodi wa North Mara na Serikali ya Tanzania ilikuwa inapata hasara ya takribani Dola 31.6 milioni kila mwaka.

Alisisitiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watendaji serikalini na wanasiasa wanaotajwa kwenye nyaraka (Mwananchi haijazithibitisha) kuhusishwa na madai ya rushwa kutoka Acacia.

Septemba mwaka huu gazeti hili liliandika habari iliyokuwa na kichwa cha habari “Siri madai vigogo kuhongwa na kampuni Acacia zavuja”, iliyoeleza madai ya tuhuma za rushwa dhidi ya kikosi kazi cha Tanzania kilichokuwa kikifanya kazi kwenye maeneo ya migodi iliyokuwa chini ya Kampuni ya Acacia.

Acacia ndiyo kampuni iliyokuwa ikimiliki migodi mitatu mikubwa ya dhahabu (Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara), kabla ya kununuliwa na kampuni ya Barrick.


Hali ilivyo

Septemba mwaka huu ndipo baruapepe hizo zilipovuja zikieleza tuhuma za rushwa kwa kikosi kazi cha Tanzania kilichokuwa kikihudumu maeneo ya migodi iliyokuwa chini ya kampuni ya Acacia.

Kikosi kazi (NTF) kinachozungumzwa ni kile ambacho huundwa na Rais, mara nyingi kikijumuisha maofisa wa Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa, kazi zake zikijumuisha kupambana na uhalifu mkubwa kama vile ugaidi na ufisadi na mkuu wake huripoti moja kwa moja kwa Rais wa nchi.

NTF kazi yake ni kulinda miundombinu nyeti ya Serikali na ya sekta binafsi nchini na katika sakata hili inaelezwa kuwa kilihusika na kutoa huduma kwa Acacia, ambapo kulingana na mahitaji ya kampuni hiyo, NFT ilikuwa na vitengo vitano, kila kimoja kikiwa na maofisa watatu mpaka saba.

Baruapepe zilizovuja kwa mara ya kwanza zilichapishwa katika mtandao wa habari wa The Globe and Mail, zinaeleza kuwa kuanzia mwaka 2008 hadi 2015 kampuni ya Acacia ilikuwa ikitumia hadi Dola za Marekani 1.2 milioni (Sh3 bilioni) kwa mwaka kwa ajili ya kulipa na kuhudumia NTF, jambo ambalo baadhi ya watendaji ndani ya kampuni hiyo walilitafsiri kama rushwa.

Mwananchi lilipomtafuta Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Eliezer Feleshi kuzungumzia suala hilo hakupatikana kwa njia ya simu na alipotafutwa Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniphace Luhende kwa ajili ya ufafanuzi alijibu kwa ufupi kuwa jambo hilo haliwahusu.