Stendi mabasi ya Kusini yaanza kwa ubovu wa miundombinu

Baadhi ya mabasi yakiwa katika stendi ya mikoa ya Kusini iliyohamishiwa Kijichi kutoka Mbagala jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Stendi ya mabasi ya mikoa ya Kusini iliyohamishiwa Kijichi kutoka Mbagala jijini Dar es Salaam, imeanza kazi kwa malalamiko ya miundombinu mibovu inayosababisha magari kunasa.
Dar es Salaam. Licha ya wadau wakiwemo madereva ma wamiliki wa mabasi kuridhishwa na uamuzi wa stendi ya mabasi ya mikoa ya Kusini kuhamishiwa Kijichi, kikwazo kikubwa kimekuwa miundombinu ya eneo la stendi.
Mwananchi imefika alfajiri ya leo Jumatano Oktoba 19 kwenye stendi hiyo iliyoanza kufanya kazi Oktoba 17 na kushuhudia baadhi ya mabasi yakihangaika kujinasua baada ya kunasa kwenye mchanga katika eneo hilo la stendi.
Hali hiyo ilisababisha wakati mwingine abiria kushuka chini wakisubiri gari linasuliwe kwenye mchanga ndipo safari ianze, hili lilisababisha kuchelewa kuanza kwa safari.
Pamoja na stendi hiyo kuwa na eneo kubwa la kuegesha magari kwa ajili ya kubeba abiria, eneo hilo halijashindiliwa hali inayosababisha magari kunasa kwenye mchanga.
Sadiki Yasin ni mmoja wa madereva aliyelalamikia hali hiyo akieleza kuwa itasababisha magari mabasi kuharibika.
“Hawa wanataka kututia hasara gari ikishanasa namna hii shughuli yake ya kuitoa unaweza ukitoka hapo ukaishia gereji sasa mambo yakiwa hivi kila siku si magari yatakufa?” amelalama Yasin.
Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa madereva wa mabasi kanda ya Kusini, Said Abdallah amesema changamoto hiyo ndogo imekuwa kikwazo kikubwa kwao hivyo kuiomba halmashauri kuitatua kwa haraka.
Amesema kwa kiasi kikubwa wameridhishwa na stendi hiuo kutokana na ukubwa wake ikilinganishwa na ilivyokuwa Mbagala na Temeke.
“Hapa vitu vingi vipo vizuri eneo ni kubwa, ulinzi na usalama wa kutosha, huduma za kijamii zipo changamoto ni hili eneo la stendi halijawekwa vizuri mchanga mwingi matokeo yake mabasi yananasa inatupa shida madereva.
“Hapa kuna stendi mbili, ya mabasi na daladala ambayo ni ndogo lakini kutokana na hali ilivyo magariyanakimbilia upande wa daladala kwa sababu kuko vizuri lakini hakutoshi mengine yanabaki upande wa pili ambako mchanga mwingi yananasa,” amesema Abdallah.
Oktoba 15 wakati wa uzinduzi wa stendi hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke Elihuruma Mabelya alisema halmashauri inazifahamu changamoto zote za stendi hiyo na inazifanyia kazi.
“Tunafahamu kuna vitu haviko sawa vyote vitarekebishwa ila tunachotaka kwa sasa stendi ianze, maboresho na marekebisho yataendelea mkiwa mnafanya kazi,” amesema Mabelya.