Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT-Wazalendo yataka hatua za wazi waliotajwa ripoti ya CAG

Kiongozi mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu akizungumza na wanahabari wakati wakifanya uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali (CAG) leo Jumamosi ya Mei 10, 2025.

Muktasari:

  • ACT-Wazalendo imesema uchambuzi wa ripoti za CAG kwa miaka minne kuanzia 2020/21 hadi 2023/24 umeonyesha kuwapo hoja zinazojirudia.

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimetaka hatua za wazi kuchukuliwa kwa wote waliotajwa kuhusika katika ubadhirifu na kuisababishia Serikali hasara kama ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilivyoeleza.

Pasipo kufanya hivyo, imeelezwa wananchi wataona ripoti ya CAG hutolewa kila mwaka kwa kutimiza wajibu na si kwa ajili ya kufunua uovu uliojificha na kuuchukulia hatua.

Aprili 16, 2025 ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2024 iliwasilishwa bungeni jijini Dodoma. Awali ilikabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwa Machi.

Akizungumza katika mkutano kuchambua ripoti ya CAG uliofanyika leo Jumamosi Mei 10, 2025, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu amesema uchambuzi wa ripoti hizo kwa miaka minne kuanzia 2020/21 hadi 2023/24 umeonyesha kuwapo hoja zinazojirudia.

Semu ameeleza hayo baada ya kufanyika uchambuzi katika maeneo 10 ambayo ni ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma, ucheleweshwaji na kutelekezwa kwa miradi ya maendeleo, kasi ya kuongezeka kwa deni la Taifa na madai ya wazabuni na wakandarasi yenye thamani ya Sh4.5 trilioni.

Mengine yaliyochambuliwa ni malimbikizo ya wafanyakazi na pensheni, usimamizi mbovu wa mashirika ya umma, hasara ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), hatari ya upigaji wa Sh262.34 bilioni za CSR za mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ukosefu wa mabasi ya mwendokasi umeleta adha ya usafiri Dar es Salaam na uwekezaji kiduchu kwenye miundombinu ya barabara.

Kuhusu ubadhirifu kwa miaka yote minne, amesema CAG ameibua hoja zenye jumla ya thamani ya Sh7.72 trilioni. Akieleza fedha hizo huenda zimepotea, kuliwa au zimetumika bila tija kwa Watanzania walio wengi.

Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo, Isihaka Mchinjita

Semu amesema kama fedha hizo zingesimamiwa vizuri, kama nchi ingepunguza kasi ya mwenendo wa deni la Taifa na kuondokana na mikopo umiza.

“Watanzania wanataka kuona hatua zikichukuliwa dhidi ya ubadhirifu unaotolewa taarifa na CAG, lakini hakuna yeyote aliyechukuliwa hatua. Kwa miaka minne tumekutana na hoja za kutelekezwa au kusuasua kwa miradi ya afya, maji na barabara nchini, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya uzembe huu,” amesema Semu.

Amesema 2025 ni mwaka wa uchaguzi mkuu, hivyo watatumia ripoti za CAG kuwaonyesha kwamba wamechoka kuona fedha za umma zinaenda kuwanufaisha watu wachache, kuona miradi inaendelea kulala huku deni la Taifa linaendelea kupaa.

“Ni wakati sasa kuipa dhamana ACT-Wazalendo ili ihakikishe kila shilingi inayokusanywa inatumika kutoa huduma bora za jamii, ijenge uchumi imara wenye kuzalisha ajira nyingi,” amesema.

Awali, Waziri Mkuu Kivuli wa chama hicho, Isihaka Mchinjita alivitaka vyombo vya habari na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutekeleza wajibu wao wa kiukombozi kuangazia, kumulika na kuweka hadharani vitendo vya ubadhirifu na upotevu wa mapato.

“Tunaisisitiza Serikali ihakikishe mfumo wake wa kielektroniki unafanya kazi kwa wakati wote na maeneo yote na kuweka utaratibu wa kutokuruhusu miamala kufanyika nje ya mifumo,” amesema.

Waziri wa Fedha wa chama hicho, Kiza Mayeye amesema ni wakati sasa CAG kufanya ukaguzi maalumu wa ununuzi wa ndege tangu ulipoanza mwaka 2016 hadi sasa akidai kuna mambo mengi yanafichwa.

Kuhusu fedha za CSR katika mradi wa JNHPP, chama hicho kimewataka wananchi wa Rufiji, Kibiti, Mkuranga, Liwale na maeneo mengine yanayoathiriwa kuwashinikiza madiwani na wabunge wao kuwajibika kusimamia na kuhakikisha Sh262.34 bilioni zinatolewa na kuhudumia jamii husika.

“Tunapinga na kukemea janjajanja zinazofanywa za kutaka kuchepusha fedha hizo na kutaka kuhudumia jamii nyingine, huku zikipuuza na kutokutoa kipaumbele kwa watu wa Rufiji, Kibiti, Mkuranga, Liwale na maeneo mengine yanayoathiriwa na mradi,” amesema Mayeye.

Ametaka Serikali iweke na kutekeleza mipango madhubuti ya dharura na usalama kuwezesha jamii zinazoathiriwa na mradi kukabiliana na madhara na majanga.

Waziri kivuli wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kulthumu Mchuchuli amesema uchambuzi wa ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha 2023/24 umebaini Serikali inatenga fedha kiduchu kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Amesema fedha inayotengwa sehemu kubwa ni kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi na kufanya maboresho ya barabara jambo ambalo linafanya Tanzania kwa zaidi ya miaka 63 tangu uhuru kubaki na barabara zisizopitika au kupitika kwa shida.