Kada Chadema atua CUF, ataka kugombea urais

Muktasari:
- Romanus amesema amekihama Chadema kwa kuwa kilitaka kuua ndoto yake ya kuwania urais wa Tanzania, huku akieleza kuwa alijipanga baada ya kuzunguka nchi nzima kutengeneza mazingira.
Dar es Salaam. Vita vya panzi, furaha ya kunguru. Ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kuanza kuvuna baadhi ya makada wanaokihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku kikisisitiza kwamba milango iko wazi kwa wanachama wengine wanaohitaji kuendeleza mapambano yao katika jukwaa jingine.
Romanus Mapunda, aliyekuwa kada wa Chadema na aliyeingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania uenyekiti kabla ya kujitoa na kumuunga mkono Tundu Lissu katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho, amejiunga rasmi na CUF leo Mei 10, 2025 huku akisisitiza azma ya kutimiza ndoto yake ya kuwania urais wa Tanzania.
Romanus alitangaza kuhama Chadema Mei 7, 2025, siku ambayo mchana wake, waliokuwa wajumbe wa sekretarieti katika uongozi uliopita, wakiongozwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Benson Kigaila walitangaza kukihama chama hicho.

Kada huyo aliyeweka nia ya kugombea urais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema, amepokelewa makao makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam, hafla iliyohudhuriwa na wanachama, huku mgeni rasmi akiwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Othman Dunga.
Akizungumza baada ya kupokewa kwake, Romanus amesema amekihama Chadema kwa kuwa kilitaka kuua ndoto yake ya kuwania urais wa Tanzania na akieleza kuwa alijipanga baada ya kuzunguka nchi nzima kutengeneza mazingira.
“Nimechukua uamuzi huu baada ya kukishauri chama lakini sikuzikilizwa, sasa ukiangalia malengo ya chama chochote ni kushika dola. Baada ya kutafakari kwa kina nimeona bora nije huku ili nipate nafasi ya kugombea urais ili niwatumikie Watanzania,” amesema Romanus.

Amesema kabla ya kuchukua uamuzi wa kujiunga na CUF, alifanya utafiti kwenye vyama vya ACT Wazalendo, Chaumma, lakini moja ya mambo yaliyomvutia kujiunga na chama hicho ni kuwa na sera ya haki sawa kwa wote.
“Vyama vingine havina sera ya haki kwa wote, hiyo unaipata CUF, peke yake lakini pia kinaheshimu Katiba tofauti na vyama vingine midomoni wanasema hiki lakini kwenye utekelezaji unapitia Mbagala,” amesema Romanus.
Romanus amesema haamini katika mbinu ya kuzuia uchaguzi inayofanywa na Chadema, lakini ni muhimu mbinu hiyo ingetumika kushiriki uchaguzi na kuona wagombea wao wanaoshinda wanatangazwa.
“Leo nimekuja CUF, lakini mjiandae kupokea wanachama wengine kama nilivyotangulia kukishauri Chadema nikatukanwa na nimekuja huku lakini kuna wanachama wengi watakuja kujiunga huku, mjipange kuwapokea.
Ameongeza: “Nimejiunga na chama hiki si kuwa mwanaharakati, bali ndoto yangu ya kuutaka urais bado iko palepale nimekuja CUF, na leo nimepokewa kwa kishindo nitatangaza muda ukifika nitachukua fomu ya kugombea nafasi hiyo kupitia CUF,” amesema Romanus.
Baada ya hotuba hiyo, Dunga amemtaka kuwa mtulivu kwani nafasi ya kutia nia ya kugombea urais wa Tanzania ameipata na pazia likifunguliwa Juni 15 hadi 30, 2025 atakiwa huru kuchukua fomu ili atimize ndoto yake.
“Chama chetu hakina pingamizi, ili ugombee uchaguzi wa kiserikali, hata ukijiunga leo unakuwa huru kugombea, lakini chaguzi za ndani zina masharti, lazima upitishwe na vikao vya chama,” amesema Dunga.
Dunga amempatia Romanus kadi pamoja na Katiba ya chama hicho ili akaisome na kuelewa miiko na taratibu za chama hicho.