Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sintofahamu mvutano Serikali, madereva malori Mwanga

Baadhi ya malori ya mchanga yakiwa yameegeshwa pembezoni mwa barabara baada ya madereva wa magari hayo kufanya mgomo wa  kuendelea na kazi kwa madai ya kupandishiwa ushuru kiholela na Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga.Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Zaidi ya madereva 50 wa malori ya mchanga katika wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro wamegoma kuendelea na kazi  kwa muda usiojulikana kwa madai ya kupandishiwa  ushuru kiholela na Halmashauri ya wilaya ya Mwanga.

Mwanga. Zaidi ya madereva 50 wa malori ya mchanga katika Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro wamegoma kuendelea na kazi  kwa muda usiojulikana  kwa madai ya kupandishiwa ushuru kiholela na Halmashauri ya wilaya ya Mwanga.

Madereva hao wamegoma leo asubuhi Juni 12, 2023 kwa madai ya kupandishiwa ushuru kiholela kutoka Sh17,000  waliyokuwa wanalipa  na  sasa kutakiwa kulipa Sh28,000 hadi  Sh40,000 kulingana na ujazo wa gari.

Wamesema hali hiyo imewapelekea kufanya kazi kwa wakati mgumu na kwa hasara kutokana na upandishwaji holela wa ushuru unaofanywa na halmashauri hiyo bila kuwashirikisha wafanyabishara hao wa mchanga.

Mmoja wa madereva hao, Zady Msuya amesema imekuwa ni kawaida kwao kupandishiwa ushuru bila taarifa na halmashauri hiyo na kwamba imefika mahali wamechoka kwa kuwa wanafanya kazi kwa hasara.

"Leo tumeamua kugoma na hatutafanya kazi mpaka hapo jambo hili litakapotiwa suluhu, hatuwezi kufanya kazi kila siku kwa hasara, mwanzoni kabisa tulikuwa tunatozwa ushuru Sh7,000 ambayo ilikuwa inafahamika na kila mfanyabiashara, ikafika mahali tukaongezewa ushuru hadi Sh 14,000 kwa gari moja, baadaye Sh17,000 sasa  cha kushangaza zaidi sasa hivi tumepandishiwa ushuru mpaka Sh28, 000 na wakati mwingine Sh40,000 kama gari limejaa zaidi,"amesema.

Kufuatia mgomo huo ambao umezua  taharuki wilayani humo , Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mwajuma Nasombe amefika katika eneo la Kileo ambapo madereva hao waliweka kambi na akawataka  kuwa watulivu na kwamba kama wana malalamiko wayafikishe ofisini kwake kesho ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.

Hata hivyo, Mkuu wa wilaya hiyo, Abdallah Mwaipaya alipiga simu, kupitia simu ya Mkurugenzi huo na kuwasikilizishia madereva hao akiwataka madereva hao kuondoka eneo hilo  na kwani  wanazua taharuki ambazo hazina msingi na kuwataka kufika ofisini kwa Mkurugenzi kesho.

"Madereva wote kama mna madai yoyote ambayo mnaona ni ya msingi,  viongozi wenu waje walete malalamiko kwa Mkurugenzi, kesho muende kwake kueleza hayo mnayotaka kueleze na mimi nitakuwepo naomba mtawanyike hapo, "amesema Mwaipaya

Bado simu hiyo ya Mkuu wa Wilaya haikufua dafu huku madereva wakiendelea na msimamo wao jambo lililomfanya Mkurugenzi kutishia kuiita kamati ya ulinzi na usalama.

"Mngekuwa na changamoto mngekuja ofisini kwangu,  nyie mna viongozi wenu, naomba niseme kitu kimoja, kwa sababu kuna watu wanashida ya vurugu naomba niahirishe tuendelee kugoma leo ili niite kamati ya ulinzi na usalama na mimi nitakuwa na walinzi ili tusaidiane, kwasababu naongea na watu wanajaziba zao na wamejipanga kivurugu, Mimi niko radhi kupoteza mapato ya leo na nyie pia mtapoteza kwa sababu tunategemeana hapa,"amesema  Mwajuma

Madereva hao wametakiwa kuchagua viongozi wawakilishi watakaokwenda ofisi ya mkurugenzi kuwasilisha changamoto zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi, huku madereva hao wakitoa angalizo kwamba kero yao isipopatiwa ufumbuzi wataendelea kugoma.