Wabunge walia gharama za kuunganisha umeme

Muktasari:
- Kwa mujibu wa wabunge, wapo wananchi mijini ambao hawana uwezo wa kulipia Sh321,000 kuunganishiwa umeme, lakini wamekuwa wakishuhudia mafanikio makubwa ya watu wa vijijini
Dodoma. Wabunge wameishauri Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kupitia upya mwongozo wa gharama za kuunganisha umeme ili kuweka unafuu kwa wananchi.
Wamesema hayo leo Jumatatu Aprili 28, 2025 wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Mbunge wa Kigoma Mjini, (CCM), Kilumbe Ng’enda amesema Serikali imesaidia watu wa vijijini kuhusu umeme lakini hivi sasa mijini inatengeneza tabaka.

Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ngenda akichangia katika makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 leo Jumatatu Aprili 28, 2025 bungeni Dodoma. Picha na Hamis Mniha. Picha na Hamis Mniha
“Wapo wananchi mijini ambao hawana uwezo wa kulipia Sh321,000 kuunganishiwa umeme, lakini wamekuwa wakishuhudia mafanikio makubwa ya watu wa vijijini lakini wao hawana nishati ya umeme,” amesema Ng’enda.
Ameitaka Serikali kuona namna ya kuwapa wakazi wa mijini umeme lakini kwa kulipa kwa awamu badala ya kuwataka kulipa fedha zote kwa mkupuo ndipo waunganishiwe nishati hiyo.
Ng’enda ameungwa mkono na Mbunge Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu akisema: “Huku ni kuwaonea wananchi wa mijini walio na uwezo mdogo wa uchumi, hivyo kuwanyima fursa ya kupata huduma kama hizi za umeme.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, Dk David Mathayo akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, amesema kumekuwa na utofauti wa gharama za kuunganishiwa umeme kwa wananchi waishio vijijini.
Amefafanua kuwa, wateja wa njia moja walio ndani ya mita 30 kutoka kwenye miundombinu ya umeme ni Sh 27,000 na wale walio umbali wa mita 70 kutoka kwenye miundombinu ni Sh515,617.52 na wateja walio umbali wa mita 120 kutoka kwenye miundombinu ni Sh696,669.64.
Amesema kamati ilielezwa kuwa, hali hiyo inatokana na mwongozo kuhusu gharama za kuunganishiwa umeme uliotolewa na Ewura.
“Baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia gharama hizo kuwa ni kubwa, na pia zinaleta utofauti miongoni mwa wananchi waishio vijijini,”amesema Dk Mathayo.

Mbunge wa Nyag'wale (CCM), Hussein Amar akichangia katika makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 leo Jumatatu Aprili 28, 2025 bungeni Dodoma. Picha na Hamis Mniha. Picha na Hamis Mniha
Amesema ili kuondokana na malalamiko hayo na kukuza ustawi kwa wananchi, Ewura ipitie upya mwongozo huo kwa kuwianisha gharama hizo ili kuweka unafuu kwa wananchi wote waishio vijijini.
Katika hatua nyingine, Dk Mathayo amesema uhaba wa maghala ya kuhifadhia mafuta unaifanya nchi kukosa uhakika na usalama wa hifadhi wa mafuta kwa muda mrefu, jambo linaloweza kuwa na athari ikiwamo kupanda kwa bei ya mafuta.
Amesema ili kuondokana na changamoto hiyo, Serikali iongeze kasi ya 41 utekelezaji wa Mradi wa Hifadhi ya Kimkakati ya Mafuta (SPR).
Dk Mathayo amesema mazingira yanayozunguka mita za mafuta (Flow metres) na bomba la mafuta, Kigamboni Dar es Salaam si salama kutokana na ufinyu wa eneo na kuzungukwa na makazi binafsi.
“Kwa kuwa, kuna ongezeko la kiwango cha kushusha na kupakia mafuta katika eneo hilo, shughuli hizo zinahitaji usalama na eneo kubwa zaidi ya lililopo, Serikali iongeze ukubwa wa eneo hilo kwa kutwaa maeneo yanayolizunguka,”amesema Dk Mathayo.
Mbunge wa Nyang’wale (CCM) Hussein Amar amewashauri wasambazaji kupunguza bei ya mitungi na gharama ya kununua gesi kwa kuwa, wananchi wa vijijini kipato chao ni kidogo.
Mbunge wa Kuteuliwa (CCM), Profesa Shukrani Manya ameshauri vyanzo vya umeme viongezwe ili chanzo kimoja kikiathiriwa na mabadiliko ya tabianchi kitumike kingine.

Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga akichangia katika makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 leo Jumatatu Aprili 28, 2025 bungeni Dodoma. Picha na Hamis Mniha. Picha na Hamis Mnih
Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amesema Makete kumekuwa na mvua zikinyesha kwa kiwango kikubwa, hivyo kusababisha transfoma nyingi kuungua mara kwa mara kutokana na radi.
“Tunaiomba Serikali, maeneo haya yenye changamoto hii tuwekeze katika kuweka mitego ya kutegua changamoto hii. Muda mrefu wananchi wanakosa umeme kutokana na kuungua kwa transfoma kutokana na radi nyingi,”amesema Sanga.
Pia, ameishauri Serikali kuja na kampeni ya kutoa elimu ya kuhifadhi umeme kwa kuhakikisha kuna matumizi sahihi ya nishati.