Mpango wa Taifa wa Nishati wapewa kipaumbele 2025/26

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko akisoma hotuba ya utekelezaji wa Makadirio ya bajeti ya wizara ya nishati ya mwaka 2025/26 leo Jumatatu Aprili 28, 2025 bungeni Dodoma. Picha na Hamis Mniha
Muktasari:
- Mpango wa Taifa wa Nishati unalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuwaunganishia wananchi kwenye huduma za nishati zinazotekelezwa
Dodoma. Wizara ya Nishati imetaja vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2025/26, vinavyohusisha kuanza kwa utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Nishati wa mwaka 2025/30.
Mpango huo unalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuwaunganishia wananchi kwenye huduma za nishati zinazotekelezwa.
Mpango huo pia, unalenga kukuza mchango wa nishati jadidifu na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya sekta ya nishati.
Katika mwaka huo wa fedha, wizara inatarajia kuajiri watumishi 1,071, kuwapandisha vyeo 1,901 na kuwahamisha 606 ili kukabiliana na upungufu wa rasilimali watu.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Aprili 28, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alipoliomba Bunge liidhinishe Sh2.24 trilioni huku akisema Sh2.16 zitatumika katika miradi ya maendeleo.
Dk Biteko amesema wizara itaendelea kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme, pamoja na kufikisha gridi ya Taifa mikoa ya Rukwa, Kagera, Lindi na Mtwara.
Pia, itaendeleza juhudi za kuhakikisha umeme wa uhakika kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia matengenezo na ukarabati wa mitambo ya kuzalisha umeme.
Maeneo mengine ya kipaumbele ni usambazaji wa nishati katika vitongoji, maeneo ya migodi, kilimo, viwanda na pampu za maji, pamoja na vituo vya afya, kwa lengo la kuimarisha shughuli za uzalishaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Aidha, wizara itahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034),” amesema Dk Biteko.
Katika sekta ya mafuta na gesi, Dk Biteko amesema wizara itaendelea kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za mafuta vijijini kwa kujenga vituo vya mafuta na kuendeleza miradi ya utafutaji, usambazaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia.
Amesema miradi muhimu inayotarajiwa kutekelezwa ni Mnazi Bay Kaskazini, Eyasi-Wembere na wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG).
“Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) imepanga kuanzisha hifadhi ya kimkakati ya mafuta, andiko la mradi litakamilishwa na kuwasilishwa serikalini mwaka 2025/26,” amesema.
Pia, amesema TPDC itaanza ukarabati wa tenki namba nane kwa kutumia Sh3.89 bilioni ambazo ni fedha za ndani.
Kuhusu usambazaji wa gesi asilia Dodoma, Dk Biteko amesema mradi mkubwa wa kujenga miundombinu ya kusambaza gesi hadi Mji wa Serikali Mtumba pamoja na ununuzi wa vifaa vya usafirishaji kutoka Dar es Salaam na ujenzi wa kituo cha kupokea gesi, utatekelezwa.
Amesema mradi huo utatumia Sh9.65 bilioni ikiwa ni fedha za ndani.
“Katika Mkoa wa Dar es Salaam, TPDC itaunganisha nyumba na taasisi 1,000 kwenye mabomba ya gesi yaliyopo. Pia, kazi za kusambaza gesi katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) na eneo la kibiashara la Mlimani City litaendelezwa kwa shilingi bilioni 8.11,” amesema Dk Biteko.
Akizungumzia ujenzi wa vituo vidogo vitatu vya kujazia gesi asilia vinavyohamishika katika mikoa ya Morogoro na Dodoma, Dk Biteko amesema vitakuwa na uwezo wa kuhudumia magari 300 kwa siku huku Sh8.26 bilioni zikitumika kutekeleza mradi huo.
Naibu waziri mkuu huyo amesema Serikali pia imepanga kuanza mradi wa kuunganisha umeme katika vitongoji 9,009 kwa kujenga miundombinu ya umeme, kufunga transfoma 9,000 na kuwaunganisha wateja wa awali 290,300.
Dk Biteko amesema mradi huo unakadiriwa kugharimu Sh1.39 trilioni, kati ya fedha hizo, Sh350 bilioni ni za ndani na Sh2.26 bilioni zinatoka Serikali ya Norway.