Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Biteko ahitimisha ziara Arusha akisisitiza amani

Muktasari:

  • Dk Biteko ameonya wanaotaka uongozi katika Uchaguzi Mkuu 2025 wasiutafute kanisani au msikitini.

Arusha. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, katika ziara ya siku nne mkoani Arusha pamoja na mambo mengine, amesisitiza amani, akitaka wananchi kutokugawanywa kwa itikadi za dini wala za siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025.

Dk Biteko aliwasili Arusha Aprili 22, 2025, ambako alikagua miradi ya maendeleo ikiwa ni katika kuelekea maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyohitimishwa leo, Aprili 26.

Kiongozi huyo alianza ziara Aprili 23 katika wilaya za Monduli, Longido, Arumeru na Arusha, ambapo amewataka wananchi kutokugawanywa kwa itikadi ya dini wala siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kwa manufaa ya Taifa.

Kila alipopita kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo alitoa wito kwa wananchi kudumisha amani, umoja na kuenzi Muungano.

Wilayani Monduli, Dk Biteko alikagua Shule ya Sekondari Migungani na mradi wa maji katika Kijiji cha Esilalei.

Katika mkutano wa hadhara shuleni hapo, Dk Biteko alizungumzia kuhusu umeme, akisema vijiji vyote vya Wilaya ya Monduli vimeshapata nishati hiyo.

Alisema vitongoji 236, kati ya hivyo 72 vimepata huduma hiyo na vilivyobaki vitapata baada ya uchaguzi mkuu.

Kuhusu utatuzi wa migogoro wilayani humo, ameipongeza wilaya hiyo kwa jitihada za kuitatua ile inayohusu ardhi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kuwataka viongozi kutatua changamoto za wananchi katika maeneo yao.

"Naomba niwapongeze tena uongozi wa Wilaya ya Monduli kwa kuendelea kufanya kazi nzuri hapa wilayani kwa masilahi mapana ya wananchi wa Monduli. Nimejulishwa mmefanya mengi mno, ikiwemo utatuzi wa changamoto na migogoro ya ardhi," amesema.

Aprili 24, 2025, akiwa wilayani Longido, pamoja na masuala mengine aliagiza kufungwa kwa vifaa vya maabara ya kemia na biolojia katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Longido Samia, ili wanafunzi waanze mafunzo kwa vitendo.

Amesema lengo la Serikali ni kuimarisha elimu kwa kujenga maabara na kukuza uzalishaji wa wanasayansi.

Shule hiyo, iliyojengwa kwa zaidi ya Sh4.4 bilioni, tayari imepokea baadhi ya vifaa vya maabara wiki mbili zilizopita, lakini havijafungwa kutokana na kutokamilika kwa ufungaji wa makabati.

Amesema Serikali imewekeza katika elimu, hasa kwa watoto wa kike kwa kujenga miundombinu ya kisasa kama vile maabara, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuzalisha wataalamu wa sayansi nchini.

Ameonya haitakiwi wanafunzi kuendelea kuchora vifaa vya maabara kama vile 'Bunsen burner' badala ya kuvitumia kwa vitendo, jambo alilosema ni mambo ya zamani.

"Maabara zimejengwa vizuri lakini hazijaanza kutumika, nimemuelekeza mkuu wa mkoa na mkurugenzi wa halmashauri kufuatilia jambo hili kwa karibu. Vifaa hivi vimenunuliwa, hatutaki viwepo stoo; watoto waanze kujifunza kwa vitendo," ameagiza

Aprili 25, 2025, Dk Biteko aliendelea na ziara wilayani Arumeru ambako alikagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru na kuhitimisha kwa mkutano wa hadhara katika Stendi ya Soko la Tengeru.

Akizungumza na wananchi kwenye mkutano huo, pamoja na kusisitiza juu ya umuhimu wa kudumisha Muungano, aliwataka wananchi kulinda amani na kuhakikisha uchaguzi hauwagawi.

Amehitimisha ziara leo, Aprili 26, akiwataka wananchi kutambua uchaguzi ni tukio la mara moja na kuna maisha baada ya uchaguzi, hivyo wavumiliane, wastahimiliane, kuthaminiana na kujiona wamoja wanaolenga kuchagua viongozi kwa nia ya maendeleo.

"Kwa tunaotaka uongozi tusitumie tofauti zetu kutafuta kura ukaenda kanisani kwako ama msikitini ukatafuta uhalali wa kanisa au msikiti kutafuta kura, hilo halitafanya Tanzania kuwa bora, itatugawanya," amesema.

Akiwa jijini Arusha akihitimisha ziara, Dk Biteko amekabidhi zawadi kwa washindi wa usafi wa mazingira na kugawa majiko ya nishati safi kwa mama na baba lishe.