Simulizi masaibu ya biashara ya ukahaba-3

Muktasari:
- Kuna dhana kuwa wasichana wote wanaofanya biashara ya kujiuza ni watu wanaopenda hali hiyo. Lakini ukipata wasaa wa kuwasikiliza baadhi yao wanahitaji ushauri wa kisaikolojia au kushikwa mkono ili kuondokamana na biashara hiyo haramu.
Dar es Salaam. Kuna dhana kuwa wasichana wote wanaofanya biashara ya kujiuza ni watu wanaopenda hali hiyo. Lakini ukipata wasaa wa kuwasikiliza baadhi yao wanahitaji ushauri wa kisaikolojia au kushikwa mkono ili kuondokamana na biashara hiyo haramu.
Katika mwendelezo wa makala ya uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa gazeti hili, walipata wasaa wa dakika 45 kuzungumza na Jane (17) zilibadili mtazamo wa hali halisi ilivyo. Ukweli ni kuwa baadhi ya wasichana wanaojiuza, maisha yao yamejaa machungu mengi huku wengi wakikata tamaa ya maisha kiasi cha kuamua kufanya lolote.
Msichana huyu mdogo, licha ya kuwa mrembo, hafanani na maisha aliyoyachagua kuishi anayodai ameyazoea.
Jane amejiingiza kwenye biashara hatarishi ya ukahaba na kushiriki ngono na wanaume zaidi ya watano kwa siku ikiwa ni njia ya kujipatia riziki ili kumudu kuhudumia familia yake.
Haikuwa rahisi kumpata na kumshawishi kuzungumza na gazeti hili kutokana na unyeti wa jambo lenyewe, aina ya maisha anayopitia na namna jamii itakavyomchukulia kila wanapoona sura yake.
“Nimeridhika hivi nilivyo na biashara ninayoifanya (ukahaba) inaniingizia kipato, niliingia huku kusaka pesa zaidi. Nimezoea, siwezi kulala bila kukutana na mtu, nitaumwa. Ni sehemu ya maisha yangu,” anasimulia Jane.
Anasema anafanya biashara hiyo katika madanguro mchana na jioni huweka mitego yake kwenye baa kabla ya usiku kwenda kujirusha katika klabu zinazokesha.
Jane anasema katika kazi hiyo amekutana na mikasa mingi ikiwamo kubakwa, kulawitiwa na wateja wanaomnunua na hata kupigwa na makahaba wenzake kutokana na visa mbalimbali, vikiwamo kumtuhumu kuchukua wanaume zao katika maeneo mapya anayokwenda kufanya biashara hiyo.
Anasimulia kuwa alianza biashara hiyo haramu mwaka 2018 maeneo ya Tandale ‘uwanja wa fisi’ kwa dau la Sh2,000 hadi Sh6,000 kulingana na makubaliano, wakati huo akiwa na umri wa miaka 14.
“Nikiwa na umri wa miaka 12, wazazi wangu walitengana, mama aliondoka na alipotaka kutuchukua baba alimzuia. Nilibaki na mdogo wangu wa miaka miwili na wengine wawili wakubwa. Mimi ni wa kwanza kuzaliwa hivyo nilibeba jukumu kama mama na baba wa familia,” anasimulia Jane.
Hata hivyo, anasema baba yao aliwatunza awali lakini kutokana na tabia zake za ulevi kuna nyakati alishindwa kuhudumia familia na kuisahau.
“Kuna nyakati tulilala njaa, baba anarudi usiku amelewa, nikimwambia hatujala ananipiga. Kutokana na kupewa msaada wa chakula na majirani kuna mpangaji mwenzetu nilizoea kumwita anko siku moja aliniita anipe hela chumbani kwake akanibaka,” anasema.
“Niliumia sana lakini akaniambia niwe nakwenda ananipa hela. Nilizoea huo mchezo baadaye asiponipa wengine wananitongoza na kushiriki nao, nikajikuta nimezoea kuwa na wanaume wengi,” anasema Jane.
Anasema hali ilizidi kuwa mbaya baba yake alivyopotea mwaka 2017, “Aliondoka kama kawaida lakini hajarudi mpaka leo na nilikuwa sifahamu ndugu wala mawasiliano ya mama yangu mzazi, hivyo, nilibeba rasmi jukumu la kulea wadogo zangu.
“Kuna nyakati nahisi baba yangu hayupo hai kwa maana hakuwahi kurudi nyumbani. Tangu hapo maisha yalianza upya, nilitegemea wanaume tofauti kuishi, fedha niliyopewa ni kati ya Sh1,000 mpaka Sh5,000 lakini hazikutosha ilifikia hatua niliacha shule nikiwa darasa la sita wakati huo nina miaka 13,” anasimulia Jane ambaye kwa sasa analea wadogo zake bila msaada wa mtu mwingine.
Anasema akiwa na miaka 14 alishawishiwa na rafiki zake kuna eneo wanapata fedha nyingi kutoka kwa wanaume na hapo ndiyo ikawa mwanzo wake kujiuza kwenye danguro la uwanja wa fisi.
Licha ya mtoto huyo kukidhi baadhi ya mahitaji ya familia yake kutokana na biashara hiyo, lakini anaiweka hatarini afya yake dhidi ya magonjwa ya zinaa ukiwamo ukimwi na athari nyingine za kisaikolojia.
Katika umri alionao Jane, alitakiwa kuwa shule kama walivyo wanafunzi wengine, fursa ambayo ingemwezesha kufanya kazi ya ndoto yake badala ya kuuza utu wake kwa dhiki ya muda mfupi.
Mwanasaikolojia atoa ushauri
Akizungumzia athari anazoweza kuzipata kutokana na aina ya maisha anayoishi, mwanasaikolojia, Modesta Kimonga anasema ngono za mapema kwa watoto yakiwamo matukio ya ubakaji, yanawapunguzia ari ya kujiamini na kuthamini utu wao.
Anasema watoto wengi wanaokutana na kadhia hiyo hupoteza mwelekeo wa maisha na kuona maisha yao hayana thamani yoyote bali wapo ili mradi wana uhakika wa kula siku inayofuata.
“Inawezekana kwa watoto wanaopitia hali hii kubadilika na kuanza kujithamini. Jamii isiwatenge, wazungumze nao na kuwasaidia kwa namna yoyote kuwatoa katika mazingira hatarishi waliyoyachagua wakidhani watapata unafuu wa maisha,” anasema Modesta.
Kauli ya Serikali
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk John Jingu alisema suala la madanguro haliruhusiwi na ni kinyume cha sheria.
Aliwataka wananchi wanapoona madanguro yameanzishwa katika mitaa yao watoe taarifa kwa viongozi wao wa Serikali ya mtaa au polisi ili wachukue hatua mara moja.
“Wananchi watimize wajibu wao wa kutoa taarifa kwa viongozi wao wa mitaa au polisi. Sisi hatuwezi kujua kama sehemu fulani kuna tatizo kama hawajatoa taarifa kwenye mamlaka zinazohusika.
“Kweli hili jambo halikubaliki kwa sababu ni kinyume cha sheria. Kwa hiyo, kila mtu atimize wajibu wake, wananchi wana wajibu wao na sisi Serikali tuna wajibu wetu,” alisema Dk Jingu.
Pia, alisema kama kuna takwimu halisi kuhusu ukubwa wa tatizo hilo, basi anaomba kupata taarifa ili Serikali ione namna ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo pia ni kinyume na maadili ya Kitanzania.
“Kama mna takwimu halisi za haya madanguro basi mtupatie taarifa, lakini kama hali ni ile ninayoijua, basi wananchi wana wajibu wa kutoa taarifa Serikali ya mtaa na polisi,” alisema kiongozi huyo.
Kwa nyakati tofauti, Serikali ilijaribu kukabiliana na makahaba wanaojiuza mitaani, hata hivyo, jitihada hizo hakikuzaa matunda.
Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alijaribu kupambana na makahaba kwenye madanguro yao yaliyopo Mtaa wa Fisi, Manzese, hata hivyo hakufanikiwa kwa kiasi alichotarajia.
Hatua hiyo imetokana na mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahusika, ambapo awali walikuwa wakisimama kandokando mwa barabara nyakati za usiku kama ilivyokuwa mtaa wa Ohia, Dar es Salaam.
Mbinu inayotumiwa kwa sasa na makahaba wengi ni kupangisha vyumba na kuendesha biashara hiyo ambapo, wateja huwafuata tofauti na ilivyokuwa awali.
Pia, makahaba wengine wamejikita katika kuendesha biashara hiyo kidijitali ambapo, huwatumia picha za utupu wateja kupitia simu za mkononi ama mitandao ya kijamii na kuelewana kila kitu kabla ya kukutana.
Hata hivyo, uwepo wa madanguro haya katikati ya makazi ya watu unatajwa kusababisha mmomonyoko wa maadili katika jamii hasa kwa watoto ambao wanajifunza kutokana na wanachokiona.
Viongozi wa dini wametoa rai kwa Serikali kuingilia kati suala hili ili kuwanusuru wananchi na hatari zilizopo ikiwemo kuwa na kizazi ambacho kimepoteza maadili ya Kitanzania.
Polisi yatoa onyo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai alisema mwanaume au mwanamke yoyote anayeishi kwa kutegemea biashara ya ukahaba anakuwa anatenda kosa au kwa mtu anayefanya makazi yake kufanyia biashara hiyo.
Alisema linapotokea hilo jeshi la polisi limekuwa likiwawajibisha kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sharia.
“Tumekuwa tukifanya operesheni mitaani na kuwakamata wameona ni kero kwao, sasa wameona wabidilishe mbinu ingawa kwetu inakuwa ni vigumu kubaini maeneo hayo, tunapopata taarifa huwa tunafuatilia,” alisema Kingai na kuongeza:
“Hawa wanakuwa wanatenda makosa ya kijinai, ni hizi operesheni zetu zimekuwa zikiwasumbua ndio maana wakati mwingine wanabuni njia, mbinu na kufanya biashara hiyo kwa siri.”
Kamanda Kingai alibainisha kuwa jeshi hilo linapopata taarifa ni wapi walipopangisha hufuatilia na kuwakamata kisha kuwafikisha mahakamani ambapo zipo kesi mbalimbali zinazoendelea.