Simbachawene aonya kampuni za simu zinazovujisha siri za wateja wao

Muktasari:
- Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene ameitaka ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuanza kuwachunguza na kuzichukulia hatua baadhi ya kampuni ya simu za mkononi pamoja na watumishi wake wanaovujisha taarifa za miamala ya wateja wao kwa wahalifu wa mitandaoni.
Morogoro. Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene ameitaka ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuanza kuwachunguza na kuzichukulia hatua baadhi ya kampuni ya simu za mkononi pamoja na watumishi wake wanaovujisha taarifa za miamala ya wateja wao kwa wahalifu wa mitandaoni.
Akizungumza jana Jumatano Februari 23 katika mafunzo ya makosa ya mitandao kwa mawakili wa Serikali mjini hapa, Waziri Simbachane amesema anashangazwa kwa kuona baadhi ya wahalifu na taarifa za mteja aliyefanya muamala wa simu.
Waziri Simbachane amesema kuwa kuna uwezekano wa baadhi ya watumishi wa kampuni za simu sio waaminifu kwa kutoa siri za wateja kwa wahalifu na kusababisha wizi katika akaunti zao za fedha za baadhi ya mitandao.
“Kwani inawezekanaje kwa mharifu akajua kwamba mtu fulani amefanya muamala wa kuhamisha fedha kama sio makapuni ya simu yanatoa siri lakini je mharibu anajuaje kama fedha imeingia kwa mtu na kwanini haya makampuni msiyakamate na kundi linaliathirika na wizi huo ni akimama kuibiwa” amesema Waziri Simbachawene.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu amesema baada ya mafunzo hayo wanaimani kuwa mawakili wa Serikali watafanyakazi kwa weledi katika kushughulikia makosa ya kimtandao na kuondoa malalamiko mengi ya wananchi.
Mwakitalu amesema changamoto zilizokuwa zinakwamisha uendeshaji wa kesi za kimtandao ni uelewa mdogo kwa baadhi ya mawakili wa serikali jambo ambalo limesabaisha malalamiko kuwa mengi yakielezwa kwao wasomi hao kutokana na vitendo hivyo kuonekana kuongezeka siku hadi siku.
“Tumekuja Morogoro ili kuwapa uelewa zaidi na mawakili wa serikali wamekuwa wachache na umuhimu wa mafunzo hayo imeilazimu ofisi yetu kusimamisha shughuli ili kuhakikisha mharifu asione kama kuna njia ya kupita kufanikisha uharifu wake,” amesema Mwakitalu.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Makosa ya Kimtandao Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Monica Mbogo amesema kuwa lengo la kufanya mafunzo hayo ni kuhakikisha waendesha mashtaka wanakuwa na uwezo wa kukabiliana na makosa hayo hasa wakati huu ambao teknolojia imekuwa kwa kiasi kikubwa.
Monica amesema sheria ya makosa ya mtandao sio mpya lakini kutokana na sababu za kukua kwa teknolojia mambo mbalimbali yamebadilika ikiwemo uendeshaji wa kesi na ushahidi unao kusanywa na kuwasilishwa vielelezo mahakamani.