Prime
Shahidi muhimu kesi ya Wakenya wanaodaiwa kuua Mtanzania kutotajwa

Muktasari:
- Mauaji hayo yanadaiwa kufanyika Januari 31, 2024 jijini Dar es Salaam kwa watuhumiwa hao kudaiwa kumnyonga Ameir kwa mkanda, kumfunga kwenye mfuko wa Sulphate na kumpakia kwenye boti Mv Zuhura na kumtupa baharini.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imezuia kutajwa majina na mahali anapoishi, shahidi muhimu katika kesi ya mauaji ya Mtanzania Mohamed Ameir inayowakabili raia wawili wa Kenya.
Mauaji hayo yanadaiwa kufanyika Januari 31, 2024 jijini Dar es Salaam kwa watuhumiwa hao kudaiwa kumnyonga Ameir kwa mkanda, kumfunga kwenye mfuko wa Sulphate na kumpakia kwenye boti Mv Zuhura na kumtupa baharini.
Uamuzi wa kuzuia shahidi huyo, familia yake na ndugu wa karibu kutajwa kesi ya mauaji namba PI 1494/2025 umetolewa Juni 22,2025 na Jaji Butamo Phillip wakati akitoa uamuzi wa maombi yaliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Mbali na kutotajwa kwa shahidi huyo muhimu wa Jamhuri, familia yake wala ndugu zake wa karibu na mahali wanapopatikana, lakini Mahakama imezuia kutaja mashahidi wengine muhimu wa Jamhuri bila ruhusa ya Mahakama.
Maombi hayo namba 14230 ya 2025 yalikuwa kati ya DPP dhidi ya washitakiwa hao wawili, Abdulsalam Said Hemed au Dully au Khalifa Mohamed Ahmed na Sadick Salum Said au Captain Sanko aliyekuwa nahodha wa Mv Zuhura.
Katika maombi hayo, DPP aliomba amri ya kutotajwa kwa shahidi huyo muhimu, familia yake na ndugu zake wala kubainisha anuani zao na mahali walipo wakati wote wa usikilizwaji ili kuficha utambulisho wao kwa sababu za kiusalama.
Pia, DPP aliomba Mahakama iamuru kuwa mwenendo wa usikilizwaji wa shauri kwa shahidi huyo muhimu wote ufanyike kwa faragha au kupitia kizimba maalumu ambacho hakitaruhusu kuonekana ili kutoa hakikisho la usalama wake.
Mbali na ombi hilo, DPP aliiomba Mahakama itoe amri kuwa maelezo ya shahidi huyo muhimu ambayo watapewa washitakiwa, mawakili wa utetezi na Mahakama, yafiche maeneo yanayoonesha utambulisho wake na anuani yake.
DPP pia aliomba Mahakama ichukue hatua zozote inazoona zinafaa ikiwamo kuzuia usambazaji na uchapishaji wa ushahidi wa nyaraka au wa mashahidi wengine muhimu unaoonesha utambulisho wao bila kibali cha Mahakama.
Katika ombi la sita, DPP aliomba Mahakama itoe amri ya kuzuia usambazaji na uchapishaji wa taarifa zozote zinazoweza kuonyesha eneo, makazi au mahali walipo mashahidi muhimu wa Jamhuri au ndugu yoyote wa karibu yao.
Sababu kwa nini majina yafichwe
Maombi hayo ya DPP yaliambatana na viapo viwili vya wakili mwandamizi wa Serikali, Rabia Ramadhan na Mkuu wa Upelelezi (RCO) Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kamishna Msaidzi wa Polisi (ACP) Jumanne Amos, kuunga mkono maombi hayo.
Katika usikilizwaji wa maombi hayo ya upande mmoja yaliyosikilizwa chemba kutokana na aina ya maombi, wakili Rabia akisaidiana na wakili mwingine mwandamizi wa Serikali, Mwanahamisi Kilonga walimwakilisha muombaji.
Akijenga hoja kwanini shahidi huyo na mashahidi muhimu wasitajwe bila ruhusa ya Mahakama, wakili Kilonga alisema maombi hayo yanatokana na kesi ya mauaji ya mwaka 2025, iliyopo hatua za awali katika Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni.
Alidai kuwa wajibu maombi wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji; na kulingana na upelelezi uliofanywa na Mkuu wa Upelelezi Temeke, unaonesha wapo washirika katika mauaji hayo ambao bado hawajakamatwa na jitihada za kuwatafuta zinaendelea.
Kulingana na hoja ya DPP, watuhumiwa hao ambao bado hawajakamatwa wanadaiwa kufanya kazi kubwa ya kumtisha shahidi muhimu wa Jamhuri asiweze kufika mahakamani kutoa ushahidi wake kuunga mkono ushahidi wa Jamhuri.
Mauaji yanavyodaiwa kutendeka
Katika hati ya kiapo cha Wakili Rabia na Mkuu wa Upelelezi Temeke, vilikuwa na maudhui yanayofanana na hoja iliyojengwa na wakili Kilonga wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, wakitoa sababu za kwanini maombi hayo ni muhimu yakubaliwe.
Kulingana na viapo hivyo, vinadai kuwa taarifa za kutoweka kwa Mtanzania Mohamed Ameir, zilitolewa Kituo cha Polisi Magomeni, Dar es Salaam na mara moja uchunguzi wa kutoweka kwake ulianza kubaini nini kimejificha.
Januari 31,2024 wakati uchunguzi ukiwa bado unaendelea, matumizi ya kadi ya sim (SIM card) ya Ameir yalihama kutoka kwenye kifaa cha mawasiliano (handset) cha awali na kuonesha inatumiwa na kifaa kingine kilichopo eneo la Kibugumo.
Baada ya kupata taarifa hizo, DPP anadai maofisa wa polisi walikwenda eneo ambalo laini hiyo ilikuwa ikitumika na kufanikiwa kufika katika nyumba aliyokuwepo Yahaya Daud au Ogaa, mkewe Aisha Dinya pamoja na Abdulsalam.
Maofisa wa polisi waliulizia simu waliyokuwa wakiitafuta iliyokuwa mikononi mwa Daud, ambaye hata hivyo alifanikiwa kukimbia na kumwacha mkewe pamoja na mjibu maombi wa kwanza (Abdulsalam) ambaye alikamatwa.
Baada ya kukamatwa, DPP anadai mjibu maombi huyo alihojiwa na kukiri kushiriki mauaji hayo na kumtaja Yahaya Daud au Ogaa na Imran Waziri kuwa ndio wanaodaiwa kumuua Ameir kwa kumnyonga shingo kwa kutumia mkanda.
DPP kupitia viapo vya wawili hao, anadai katika kufanikisha kitendo hicho, watuhumiwa walimziba Ameir mdomo kwa kutumia ‘sole tape’, kumfunga kwenye mfuko wa Sulphate na kisha kuuweka mwili wake kwenye Mv Zuhura.
Baadaye inadaiwa mjibu maombi wa Pili, Sadick Said au Captain Sanko ambaye alikuwa nahodha wa boti hiyo, aliiendesha boti hiyo hadi katikati ya Bahari ya Hindi na kuutupa mwili wa marehemu kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Timu ya makachero wabobezi wa Tanzania walifanya upelelezi wa tukio hilo na kudaiwa kugundua kuwa wajibu maombi hao wawili sio raia wa Tanzania bali Kenya na uchunguzi ulifanikiwa kumtia mbaroni Captain Sanko jijini Tanga.
Mleta maombi anadai, Captain Sanko alikamatwa akiwa katika harakati wa kutoroka kwenda Kenya kupitia mpaka wa Horohoro na kutokana na unyeti na uzito wa tukio hilo, mashahidi wa Jamhuri wamekuwa wakipata vitisho.
Vitisho hivyo kwa mujibu wa DPP, vinadaiwa kufanywa na wajibu maombi kwa kushirikiana na washirika wao ambao bado hawajakamatwa na wapo Tanzania na wanahangaika kupata majina na anuani za shahidi muhimu wa Jamhuri.
Kwa mujibu wa DPP, anadai kuwa taarifa za uhakika za kiintelijensia zimebainisha kuwa, wajibu maombi na washirika wao hao, wanakusudia kutumia mbinu zozote ili kumuua shahidi huyo muhimu pamoja na familia yake ili asitoe ushahidi.
Kupitia viapo hivyo, DPP ameenda mbali na kudai kuwa kulingana na unyeti na uzito wa mashitaka dhidi ya wajibu maombi hasa ikizingatiwa wana mafunzo ya juu ya kijeshi, ni muhimu shahidi huyo na familia yake kulindwa kwa kutotajwa.
Uamuzi wa Jaji
Katika uamuzi wake, Jaji Butamo amesema baada ya kusikiliza hoja za DPP na kuzichambua, sheria inaruhusu maombi hayo kusikilizwa upande mmoja, hivyo maombi hayo yalisikilizwa bila uwepo wa wajibu maombi.
Jaji amesema viapo hivyo viwili, vimetoa taarifa za kutosha kuishawishi Mahakama kutoa amri zinazoombwa kwa ajili ya kumlinda shahidi muhimu.
“Ni muhimu kuelewa kuwa shahidi ni mshirika muhimu katika utoaji wa haki. Ninafahamu kuwa usikilizwaji wa kesi ambao mashahidi hawafichwi utambulisho wao unatoa hakikisho la usikilizwaji wa haki,”amesema.
“Hata hivyo katika mazingira maalumu na ili kutenda haki, ni muhimu kuficha utambulisho wa mashahidi ili kuwalipa. Kwa mfano katika shauri ambalo wapo watuhumiwa hawajakamatwa na wanatoa vitisho kwa mashahidi,” amesema.
“Ifahamike kuficha utambulisho wa shahidi hakuvunji sheria yoyote wakati wa mchakato wa kuhamishia kesi Mahakama Kuu au usikilizwaji wa shauri la msingi. Ni kwa msingi huo Mahakama inaona ipo haja ya kutoa amri zinazoombwa.”
Hivyo, Jaji akatoa amri sita, moja taarifa binafsi na anuani ambazo zinaweza kusababisha shahidi muhimu wa Jamhuri au mahali alipo zinatakiwa zisitajwe katika usikilizaji wa awali na shauri la msingi kwa sababu za kiusalama.
Jaji amesema katika usikilizwaji wa awali wa shauri hilo, shahidi muhimu atatoa ushahidi wake katika kizimba maalumu na tatu sehemu ya maelezo ya shahidi yatakayoonesha utambulisho wake na mahali alipo hayataoneshwa.
Mbali na amri hiyo, Jaji amesema wakati wote wa usikilizwaji wa mchakato wa kuihamishia kesi Mahakama Kuu hadi usikilizwaji kesi ya msingi, jina la shahidi huyo muhimu litatambulika kama P ikifuatiwa na namba na si jina lake.
Jaji pia ameelekeza kuwa usambazaji na uchapishaji wa ushahidi wa nyaraka au ushahidi mwingine wowote ambao utaonesha utambulisho wa mashahidi muhimu hautaruhusiwa wala kuonesha makazi yao au mahali wanapoishi.