Mtoto asimulia alivyojulishwa na msamaria mwema kifo cha baba yake

Muktasari:
- Kufuatia mauaji hayo Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, limeanza kuchunguza tukio la mauaji hayo na kuhakikisha waliohusika kwenye tukio hilo wanakamatwa.
Kilosa. Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamemuua kwa kumpiga risasi mfanyabiashara wa huduma za kifedha, Mana Seleman (50) mkazi wa Kitongoji cha Bombani, Kijiji na Kata ya Dumila, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Juni 22, 2025 wakati marehemu akiwa anarudi nyumbani kwake Kijiji cha Madudu kata ya Kitete baada ya kufunga biashara yake.

Mfanyabiashara wa miamala ya simu na Mkazi wa Kitongoji cha Bombani, Kijiji na Kata ya Dumila, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Mana Seleman (50) enzi za uhai wake.
Akiwa anatembea kwa miguu na begi lake mgongoni lenye vifaa vya kazi, alivamiwa na watu hao waliompiga risasi na kupora begi hilo kisha kutokomea kusikojulikana.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Mtakatifu Joseph Dumila, Dk Seleman Sakoro amesema Mana ameshambuliwa na risasi mbili moja upande wa kushoto juu ya shavu na kutoka upande wa kulia kwenye shingo na kusababisha jeraha kubwa na damu nyingi kuvuja.
Dk Sakoro amesema risasi iliyoingia katikati ya kifua na kutoka upande wa kulia wa mbavu imeharibu pafu la kulia na kusababisha damu nyingi kuvuja ndani ya kifua na hicho ndicho kilichosababisha kifo cha mfanyabiashara huyo.

Mganga mfawidhi kituo cha afya cha Mtakatifu Joseph Dumila Dk. Seleman Sakoro akitoa taarifa baada ya kupokea mwili wa mfanyabiasha wa miamala mkazi wa Dumila Selemani Mana aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia leo Juni 22 na watu wasiojulikana muda mfupi baada ya kufunga eneo lake la biashara. Picha Jackson John.
“Mfanyabiashara huyu alifikishwa hospitalini hapa saa nne usiku akiwa tayari amefariki dunia, uchunguzi umeonyesha alishambuliwa kwa kitu chenye ncha kali kinachofanana na risasi kitu hicho kiliingia upande wa kushoto juu ya shavu na kutoka upande wa kulia kwenye shingo, kikasababisha jeraha kubwa na damu nyingi kuvuja,” amesema Dk Sakoro.
Akisimulia tukio hilo mtoto wa marehemu, Zulfa Mana amesema saa mbili usiku akiwa anatoka dukani alikuta baba yake hayupo alipomuuliza mama yake alimwambia ametoka kaelekea dukani kuchukua begi la vifaa.
Amesema saa nne alipigiwa simu na moja ya wasamaria wema na kuelezwa kuwa baba yake amepigwa risasi na amefariki dunia.
“Jana usiku tulikuwa nyumbani na mama, ilivyofika saa mbili nilienda dukani baada ya kurudi kutoka dukani nikakuta baba hayupo, nilipomuuliza mama aliniambia baba yako ameenda kufuata begi dukani, begi ambalo tunaweka vifaa vyote vya miamala.
“Ilivyofika saa nne kasoro nikapokea simu naambiwa baba yako amepigwa risasi, nikakimbia hadi barabarani nikachukua bodaboda nikaenda hadi dukani nikakuta duka limefungwa, nikazungumza na huyo aliyenipigia simu akaniambia njoo huku maeneo ya Bati la Kona ambapo ni karibu na duka, nilipofika nikamkuta baba amelala chini amefunikwa," amesimulia Zulfa.
Ameiomba Serikali kuhakikisha watu wote waliohusika kufanya mauaji ya baba yake, wanatafutwa na kukamatwa ili sheria ichukue mkondo wake.

Zulfa Mana akisimulia namna qlivyopokea taarifa za kuuawa Kwa baba yake Selemani Mana ambaye ni mfanyabiasha wa huduma za kifedha Dumila aliyeuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika usiku wa kuamkia leo muda mfupi baada ya kufunga eneo lake la biashara. Picha Jackson John.
Mohamed Chilunda, shemeji wa marehemu amesema tukio hilo limewatia hofu kubwa, hasa kwa vile muda mrefu hali ya usalama ilikuwa imetulia.
Kufuatia mauaji hayo Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limeanza kuchunguza tukio la mauaji ya mfanyabiashara huyo.
"Mfanyabiashara huyo ambaye kwa sasa ni marehemu baada ya kufunga kibanda chake cha biashara ya miamala ya fedha akiwa njiani kurejea nyumbani ghafla alivamiwa na mtu huyo na kumpiga risasi, kisha kuchukua mkoba mdogo na kutoweka nao," amesema Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Alex Mkama.
Hivyo amesema kuwa Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa kina, ili kumkamata yeyote ambaye amehusika kwenye tukio hilo.
"Tunawaomba wananchi wema mwenye taarifa za mtu au watu waliohusika na mauaji haya watoe taarifa ili kusaidia kukamilisha uchunguzi kwa haraka," amesema Kamanda Mkama.