Mtuhumiwa wa utekaji wa mtoto apigwa risasi akijaribu kutoroka

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu kukamatwa kwa mtuhumiwa wa wizi wa mtoto. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Mtuhumiwa wa utekeji wa mtoto eneo la Mbezi amepigwa risasi na askari polisi alipojaribu kutoroka akiwa chini ya ulinzi.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inamshikilia Stanley Bulaya, mkazi wa Kata ya Nguruka, wilayani Uvinza, Mkoa wa Kigoma kwa tuhuma za kumteka mtoto wa kiume (8) mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbezi ya jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la utekaji lilifanyika Machi 6, 2025 eneo la Mbezi Luis, Wilaya ya Ubungo, mtoto huyo alipokuwa anaelekea shuleni baada ya kushushwa na baba yake mzazi kwenye kituo cha daladala jirani na anaposoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumapili Machi 9, 2025 Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema siku hiyo mtoto hakurudi nyumbani hadi saa moja jioni wazazi wake walipoanza kumtafuta huku wakiwasiliana na mwalimu aliyepigiwa simu na mtuhumiwa kutaka namba za wazazi.
"Mtuhumiwa alichukua namba ya mwalimu kwenye daftari la mtoto na kuwasiliana na mwalimu akitaka namba za wazazi na alipopatiwa alikuwa anataka pesa tena kwa vitisho, wasipotoa mtoto huyo watamdhuru na kumpotezea maisha yake,"amesema Kamanda Muliro.
Amesema Jeshi la Polisi kwa kutumia wataalamu wake na kuhusisha kamisheni ya kutumia sayansi ya intelejensia, walifanikiwa kufuatilia na jana Machi 8 2025, mtuhumiwa alikamatwa Bagamoyo, mkoani Pwani akiwa na mtoto.

Wazazi wa mtoto aliyeibiwa, Johnson Koranya (kulia) na Modesta Ram wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, baada ya kukabidhiwa mtoto wao na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga
Kamanda Muliro amesema baada ya kukamatwa mtuhumiwa alipelekwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Amesema wakiwa kwenye taratibu za kumuweka mahabusu mtuhumiwa alikurupuka na kufanya jaribio la kutoroka akiwa chini ya ulinzi, jitihada za ulinzi zilifanyika za kumpiga risasi juu za kumtahadharisha lakini alikaidi.
Kamanda Muliro amesema baada ya kukaidi alipigwa risasi ya kwenye paja na kukamatwa tena, kisha kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya.
Mzazi wa mtoto huyo, Johnson Koranya amesema siku hiyo saa nne asubuhi, alitoka nyumbani na mwanaye akimpeleka shuleni na alipofika kituoni alimshusha na yeye kuendelea na safari ya kwenda kwenye kazi zake.
"Nikiwa kwenye shughuli zangu ilipofika saa moja jioni nilipigiwa simu kutoka nyumbani kuwa mtoto hajarudi, ikabidi nimpigie simu mwalimu wake wa darasa na alituambia bora mmenipigia kuna namba ilikuwa inanisumbua sasa hivi," amesema Koranya.
Amesema mwalimu aliwapa namba ya mtuhumiwa kwa sababu alihitaji kuwasiliana na wazazi hao.
Koranya amesema walipopatiwa hiyo namba waliwasiliana naye na aliwaambia mtoto anaye na anachohitaji ni Sh50 milioni.
"Baada ya kutajiwa kiasi hicho ilibidi kwenda kutoa taarifa polisi kituo cha Magufuli kilichopo Mbezi Luis na walisema tuwaachie jeshi lifanye kazi yake, lakini wakati huo nikiendelea kuwasiliana na hao mabwana," amesema.
Amesema kupigwa simu kote huko walihitaji pesa na jibu lake lilikuwa anajitafuta bado hajapata huku wakimtishia akichelewa atapata maiti ya mtoto wake, kama asipotuma kiasi hicho cha pesa.
Hadi kufikia jana amesema alipigiwa simu aende Kigamboni, Kisiwa cha Pemba akachukue maiti yake.
Baada ya kuambiwa hivyo alifunga safari ya kuelekea alipoelekezwa, lakini alipokuwa Kimara alipigiwa simu na Polisi kuwa mtuhumiwa amekamatwa akiwa na mtoto wake.