Sh9 bilioni kusomesha wataalamu hospitali za pembezoni

Muktasari:
- Wizara ya Afya imepatiwa Sh9 bilioni kwa ajili ya mafunzo ya wataalamu bingwa na wabobezi katika fani mbalimbali za sekta hiyo.
Dar es Salaam. Vituo vya afya vya pembezoni nchini sasa vina matumaini ya kuwa na wataalamu bingwa, baada ya madaktari na wauguzi 601 kupata ufadhili wa masomo ya ubingwa na wabobezi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia programu ya ‘Samia Super Specialist.’ Inayofadhiliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Watumishi waliochaguliwa kupata ufadhili katika vyuo vya ndani ya nchi ni 535 sawa na asilimia 89 na huku vyuo vya nje wakienda watumishi 66 sawa na asilimia 11 ya wote waliopata ufadhili huo.
Programu hiyo inalenga kuongeza wataalamu bingwa na wabobezi wa afya ya mama na mtoto ambao ni finyu katika hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Jumatano, Novemba 29, 2023 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wamechukua watalamu wengi zaidi maeneo ya pembezoni ili kuongeza idadi ya watalamu bingwa maeneo hayo.
“Serikali imeboresha miundombinu, tumeweka vifaa tiba vya kisasa ikiwemo CT Scan, MRI, XRay mashine za kisasa, Utrasound lakini bado tuna changamoto za rasilimali watu, pembezoni ndiyo kipaumbele chetu Simiyu, Katavi, Kigoma na maeneo kama hayo,” amesema.
Amesema kati ya waliopata ufadhili huo, wengi wanatoka maeneo ya pembezoni ili wakihitimu na kurudi katika maeneo yao ya kazi, wataalamu waongezeke.
“Wanaotaka kwenda kusoma ubingwa tumewahamasisha sana, kama tayari ni daktari bingwa upo MOI tutampa kipaumbele wa Katavi ambako hakuna wataalamu,” amesema.
Waziri Ummy amesema katika maeneo ambayo programu hiyo imewekeza zaidi ni katika afya ya akili, wataalamu wa saikolojia tiba, wataalamu wa huduma za upandikizaji mimba na upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.
Amesema pia wamepeleka wataalamu wengi katika huduma mpya zilizoanzishwa ikiwemo upandikizaji figo, uloto, upandikizaji wa ini na mimba.
“Mwaka jana wataalamu wa afya walikuwa 439 kwa sasa 601 na hawa tunaenda kusomesha miaka mitatu mpaka sita na tumeweka masharti ukirudi unapaswa kufanya kazi serikalini kwa muda usiozidi miaka mitano.
“Waliopata ufadhili wanapaswa wajaze mikataba hatutalipa ada ya chuo mpaka umejaza mikataba wajifunge kwamba wanakwenda kusoma na wakimaliza wataitumikia Serikali kwa miaka mitano maana wengi wakirudi wanataka kwenda sekta binafsi,” amesema.
Amesema wataalamu wengi watakwenda kusoma kama pea na kama ni upasuaji anakwenda daktari, muuguzi, mtaalamu wa dawa za usingizi na ganzi, mtaalamu wa maabara na mfamasia.
Waziri Ummy amesema wataalamu wa fani ya ubobezi wa upasuaji wa ubongo hawajajitokeza kwa wingi hali inayoashiria kwamba wengi wanaona fani hiyo ni ngumu na inachukua muda mrefu kusoma hivyo akatoa maamuzi.
“Tunataka kufanya maboresho kwamba wataalamu wetu hawa wakirudi walipwe mishahara ya juu kuwatofautisha na wengine kazi yao ni ngumu na wanasoma kwa muda mrefu, hili tutalipepeka kwa Ofisi ya Rais utumishi mpaka sasa tuna mabingwa na wabobezi wa upasuaji ubongo 23 nchi nzima,” amesema.
Amesema lengo jingine la kusomesha wataalamu wengi zaidi ni kuboresha mazingira ili kuzidi kuvutia utalii wa matibabu na kwamba wagonjwa 6,472 kutoka nje ya nchi walitibiwa nchini kwa mwaka 2022/2023 na tangu Julai mpaka Novemba wagonjwa 1,596 wametibiwa.
Mkurugenzi wa mafunzo na rasilimali watu, Wizara ya Afya, Saitori Laizer amesema walipokuwa wakichambua jumla ya maombi ya ufadhili 810 yaliyowasilishwa waliokidhi vigezo walikuwa 601 sawa na asilimia 92 waliooomba walikidhi vigezo.
“Tuliwalenga zaidi wa pembezoni, tunataka kuwapunguzia adha wananchi ya kufuata huduma umbali mrefu tuliangalia zaidi Kigoma, songwe, Katavi tuliwapa kipaumbele ili kuongeza wataalamu bingwa maeneo hayo.
“Vipaumbele vimezingatiwa tuna taaluma zinahitaji ubingwa bobezi wapo wachache sana tumechukua zaidi huko na wanaohitajika katika soko la ajira,” amesema Laizer.