Watoa huduma sekta ya madini waja kivingine

Mwenyekiti wa Kamati ya Masoko na Mawasiliano Chama cha watoa huduma katika sekta ya madini (Tamisa), Dk Sebastian Ndege akuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mei 14, 2025. Picha na Michael Matemanga
Muktasari:
- Sekta ya madini nchini Tanzania ilichangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa (GDP) kwa mwaka 2024
Dar es Salaam. Watoa huduma katika sekta ya madini wameanzisha umoja wao ambao utawawezesha kupeana taarifa na kuongeza ushiriki wa wazawa katika sekta ya madini.
Umoja huo pia unalenga kuhakikisha watoa huduma hao wanakuwa miongoni mwa wanufaika katika Sh3.1 trilioni zinazotumika kila mwaka katika ununuzi wa madini.
Mwamvuli huo uliopewa jina la Tamisa ikiwa ni kifupi cha Watoa Huduma katika Sekta ya Madini unatarajiwa kuzinduliwa Ijumaa ya Mei 16, 2025 na Waziri wa Madini, Antony Mavunde.
Akuzungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Masoko na Mawasiliano (Tamisa), Dk Sebastian Ndege amesema uzinduzi rasmi wa umoja wao utakwenda sambamba na majadiliano ambayo yanalenga kuangalia nafasi ya Watanzania kwenye utoaji huduma katika sekta hiyo.
“Watanzania wana kila sababu ya kushiriki katika sekta ya madini, tunataka kuweka urahisi kwao kuzifikia taarifa mbalimbali, fursa zilizopo zinafahamika kwa wahusika na watu wengine,” amesema.
Dk Ndege amesema uwepo wa umoja pia unalenga kuhakikisha watoa huduma katika sekta ya madini wanaotumika ni wale wenye vigezo na utaalamu badala ya kunufaisha wasiokuwa wabobevu.
“Pia itasaidia kuwanufaisha wanafunzi wetu wanaosoma katika vyuo mbalimbali ili waweze kufanya kile walichokisomea wanapomaliza,” amesema Dk Ndege.
Sheria ya ushiriki wa wazawa katika sekta ya madini Tanzania ilianza kutekelezwa rasmi kupitia marekebisho ya sheria mwaka 2017, ambapo Bunge lilipitisha Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 7) ya mwaka 2017.
Marekebisho haya yalibadili baadhi ya vipengele vya Sheria ya Madini ya mwaka 2010, na kuanzisha hitaji la ushiriki wa Watanzania na kampuni ya Kitanzania katika shughuli za uchimbaji wa madini.
Kufuatia marekebisho hayo, idadi ya Watanzania wanaofanya kazi kwenye migodi imeongezeka, hasa katika sekta ya huduma kama usafirishaji, ulinzi, na uhandisi huku baadhi ya kampuni za Kitanzania zimekuwa kwa kupata zabuni katika sekta ya madini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tamisa, Adrew Kumalila amesema taasisi hiyo ilianzishwa ili kujenga sauti moja ya watoa huduma ambayo wawezesha kushiriki vyema katika kujenga uchumi wa madini.
Amesema kwa sasa zaidi ya Sh3.1 trilioni hutumika katika manunuzi ya madini, hivyo wataangalia sehemu ambayo inakwenda ili na wao waweze kuwa miongoni mwa wanufaika.
“Badala ya kuendelea kulalamika kuwa Wachina wanakuja kuchukua fursa zetu ni vyema tuangalie namna ambayo tunaweza kuzitumia kwa umoja wetu, na hata kwenda mbali kwa kujenga viwanda hapa nchini vya kuongeza thamani ya madini,” amesema Kumalila.
Umoja huu unakwenda kuzinduliwa wakati ambao siku chache zilizopita Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alibainisha kuwa sekta ya madini nchini Tanzania ilichangia asilimia 10.1 ya Pato la Taifa (GDP) kwa mwaka 2024.
“Hii ni hatua kubwa na ya kihistoria kwani imevuka lengo la asilimia 10 lililowekwa kwenye Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026), ambao ulitarajiwa kufikiwa ifikapo mwaka 2026,” alisema Mavunde.