Leseni 95 za madini hatarini kufutwa

Muktasari:
- Leseni 95 za wawekezaji wakubwa na kati ziko hatarini kufutwa kutokana na kutoshindwa kuendelezwa ndani ya miezi 18 tangu kusainiwa kwa mkataba kama sheria inavyotaka.
Dar es Salaam. Huenda kampuni 95 zikapoteza leseni zake za uchimbaji wa madini nchini ndani ya siku saba zijazo, ikiwa zitashindwa kujieleza kwa nini wasifutiwe leseni zao ndani ya siku 30.
Kampuni hizo zilipewa hati ya makosa ambayo inazitaka kujibu hoja za kutofutiwa leseni Aprili 14 mwaka huu, ambazo zinatarajiwa kufikia tamati Mei 13, 2025.
Zilipewa hati hiyo ya makosa kutokana na kushindwa kuendeleza maeneo waliyopewa ndani ya miezi 18 tangu kusainiwa kwa mikataba husika.
Hayo yameelezwa leo, Mei 6, 2025 na Waziri wa Madini, Antony Mavunde alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa juu ya hatua wanazokwenda kuchukua dhidi ya wawekezaji wa sekta hiyo waliokiuka mikataba waliyoingia.
Mavunde amesema Serikali imetoa leseni kwa wawekezaji wa kati na wakubwa, ili kufanya uchimbaji nchini, lakini baadhi yao wamesaini mikataba na hawajaanza kufanya kazi kinyume na sheria.
"Zipo kampuni kubwa zimesaini mikataba hii, lakini hawajaanza utekelezaji wa miradi yao hadi leo. Serikali imetoa hati za makosa kwa wamiliki wa leseni 95 na kuwapa siku 30 ili kama wana hoja ya kujibu kupitia hati hii ya kutokuanza shughuli za uchimbaji madini nchini, walete majibu yao," amesema.
Amesema watakapowasilisha majibu hayo yatapitiwa ili kama wana hoja waondolewe katazo, na kama hawana hoja bila kujali mmiliki wa leseni, itafutwa.
"Leseni hizo mpaka leo hazijaanza kufanyiwa kazi. Kwa mfano, kati ya hizo zote, saba pekee zina mtaji wa Sh15 trilioni zimelala," amesema.
Amesema ni vigumu kuweka mtaji wa Sh15 trilioni kwenye makaratasi wakati kuna Watanzania ambao wanategemea kuanza kwa mradi huo, ili wapate ajira na nchi ipate mapato na uchumi kukua.
Mavunde amesema Tanzania haiwezi kuwa nchi ambayo Serikali inatoa leseni kwa ajili ya kuchochea sekta ya madini kukua, lakini kuna watu wanazichukua na hawazifanyii kazi kwa visingizio kuwa wako kwenye majadiliano na Serikali.
Aliongeza kuwa wapo baadhi ya watu wanaojificha katika suala la mazungumzo na Serikali, huku akisema leseni inapotolewa huwa na masharti nyuma yake, na hakuna sharti linalosema mtu ataanza uchimbaji wa madini akikamilisha mazungumzo na Serikali.
Akifafanua sheria zinazotumika, amesema katika utekelezaji wa ufutaji wa leseni za madini, tume huzingatia matakwa ya kifungu cha 63 cha Sheria ya Madini Sura namba 123 na kanuni zake.
Kabla ya tume kuamua kutoa hati ya makosa kwa mmiliki wa leseni ya utafutaji wa madini au uchimbaji wa madini, hupitia taarifa mbalimbali zilizopo kwenye mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni, taarifa nyingine ambazo huwasilishwa na mmiliki wa leseni pamoja na taarifa za ukaguzi zinazofanywa katika leseni hizo.
Baada ya kujiridhisha kuwa mmiliki wa leseni hajatimiza masharti ya leseni yake na Sheria ya Madini, Tume ya Madini hutoa hati za makosa kwa mmiliki huyo kwa kuainisha mambo ambayo hajafanya kwa mujibu wa sheria, kanuni na masharti ya leseni yake.
"Miongoni mwa makosa hususan kwa wamiliki wa leseni kubwa na wa kati za uchimbaji madini ni pamoja na kutokuanza shughuli za madini na uendelezaji wa leseni hiyo kwa muda ulioanishwa kwa mujibu wa sheria, kinyume na kifungu cha 52 na 47 vya Sheria ya Madini Sura ya 123," amesema.
Sehemu nyingine ni kushindwa kuwasilisha mpango wa uchimbaji madini kinyume na (kanuni ya 208) Kanuni za Mazingira, Afya na Usalama za mwaka 2010 au kushindwa kuandaa na kuwasilisha mpango wa ufungaji mgodi kinyume na kanuni ya 206(1) ya kanuni hizo.
"Pia kushindwa kuwasilisha taarifa za leseni za kila robo mwaka kinyume na kifungu cha 100(1) cha Sheria ya Madini Sura ya 123 na kushindwa kuwasilisha mpango wa ushirikishwaji katika shughuli za madini kinyume na kanuni ya 10 ya Kanuni za Ushirikishwaji katika Shughuli za Madini za mwaka 2018," amesema.
Kuwasilisha taarifa za uongo wakati wa uombaji wa leseni na kubainika, ikiwemo uwezo wa kifedha wa mmiliki wa leseni katika kuendeleza mradi, kinyume na kifungu cha 131(a) cha Sheria ya Madini, Sura ya 123 pia ni kosa linaloweza kufanya mtu afutiwe leseni.
Lakini endapo mmiliki wa leseni atajibu hati ya makosa kwa muda ulioainishwa na kuainisha namna alivyojibu makosa hayo pamoja na uthibitisho wa majibu yake, tume huchambua majibu hayo.
Endapo uchambuzi utabaini majibu hayajitoshelezi kutofuta leseni, hatua ya ufutaji leseni itafuata kwa mujibu wa kifungu cha 63(1) cha Sheria ya Madini, Sura 123.
Kama majibu yanahitaji kufanyiwa uhakiki kwa maana ya kufanya ukaguzi wa eneo kuona yaliyoandikwa ni sahihi, hatua hiyo hufanyika na endapo ikibainika kuwa si sahihi, taratibu za ufutaji zitaendelea na kama itaonekana ni sahihi, tume itaondoa hati ya makosa iliyotolewa.
Kwa kampuni ambazo hazijaanza kazi kwa kuainisha sababu mbalimbali ambazo zimesababisha kutokutekeleza wajibu, hususan kosa la kutokuanza kazi, tume ikiridhika huweza kutoa masharti ya mmiliki wa leseni kuthibitisha kuyatekeleza ili kuondoa hati hizo, wakati tume inaendelea kumsimamia kuona kama kilichoelezwa kinazingatiwa.
"Na kama mmiliki wa leseni ameshindwa kujibu hati iliyotolewa, Tume ya Madini hufuta leseni hiyo," amesema Mavunde.
Akizungumzia suala hilo, mchambuzi wa uchumi na biashara, Dk Balozi Morwa amesema ikiwa njia itakayotumika katika ufutaji wa leseni hizo inajumuisha usikilizwaji wa pande zote ni sahihi.
Hata hivyo, amehoji ikiwa kuna jitihada zozote ambazo zilifanyika kwa wale wawekezaji ambao hawakufanya chochote kwa miaka 10 tangu wapewe leseni, huku akihoji ikiwa wameshafariki dunia.
"Kama njia inayotumika ni sahihi nakubaliana nayo kwa sababu mtu kukaa na eneo miaka 10 si sahihi kwa sababu kuna wengine tumewazuia, huenda walikuwa wanataka hilo eneo ila hawajapewa kwa sababu kuna mtu tayari," amesema Dk Morwa.