Vijana 1,700 wakabidhiwa leseni za kuchimba dhahabu Tarime

Muktasari:
- Akabidhi leseni 100 kwa wachimbaji wadogo zaidi ya 1,700 wilayani Tarime kupitia ushirikiano wa Serikali na Mgodi wa Barrick North Mara, mradi unaolenga kuboresha uchumi wa vijana na mahusiano na jamii.
Tarime. Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo, mkoani Mara, imetoa leseni 100 kwa ajili ya wachimbaji wadogo vijana zaidi ya 1,700 wilayani Tarime, lengo likiwa ni kuimarisha uchumi wa vijana hao pamoja na mahusiano kati ya jamii na mgodi huo.
Mradi huo, ambao umeelezwa kuwa ni wa kwanza kwa ukubwa nchini na barani Afrika, unaohusisha mahusiano mazuri kati ya mgodi na jamii pamoja na kuimarisha uchumi wa vijana, unatarajiwa kuwawezesha wachimbaji wadogo kuboresha shughuli zao na kuongeza uzalishaji wenye tija
Akizungumza wakati wa kukabidhi leseni hizo Nyamongo, leo Jumamosi Mei 3, 2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mradi huo wa wachimbaji vijana wilayani Tarime utatumika kama mradi wa mfano kabla ya kuanza kutekelezwa kwa miradi ya aina hiyo nchini kote.
"Ili mradi ufanikiwe, tayari Benki ya Dunia imeonyesha nia ya kushirikiana nasi katika utekelezaji wake, pia kuna Umoja wa Nchi za Ulaya pamoja na Baraza la Dhahabu la Dunia wameonyesha nia. Hivyo niwahakikishie, mradi wetu utaleta matokeo chanya kama ilivyokusudiwa," amesema Mavunde.

Amesema Serikali itaendelea kusitisha maombi na leseni zinazomilikiwa na watu kwa muda mrefu bila kufanyiwa kazi, ili leseni hizo zigawiwe kwa vijana wazifanyie kazi badala ya maeneo hayo kukaa bila kuzalisha.
Mavunde amesema tayari maombi na leseni 2,648 zimesitishwa na kwamba zitagawiwa kwa vijana kupitia mradi huo, ili nao wawe sehemu ya umiliki na ujenzi wa uchumi imara wa nchi.
Akizungumza kwenye tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema ni ndoto ya mkoa huo kuona panakuwepo na mabilionea vijana kutoka katika eneo la Nyamongo kupitia sekta ya madini.
Amesema ili kufikia ndoto hiyo, ofisi yake itakuwa mlezi wa vijana hao, ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili mradi huo uwe na tija.
"Niombe pia tusiishie kwenye kutoa leseni tu, hebu tutoe na usaidizi wa kitaalamu kwa vijana hawa ili waweze kuchimba kwa tija. Tunataka vijana hawa wamiliki fedha kupitia uchimbaji, na wanaweza kumiliki fedha pale tu watakapopata usimamizi wa kitaalamu," amesema Mtambi.
Mtambi ameongeza kuwa ofisi yake iliongeza nguvu kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, kwani ilitambua kuwa bila vijana kuwa na shughuli zitakazowawezesha kupata vipato hasa kupitia uchimbaji wa madini, changamoto ya ukosefu wa vipato halali kwa vijana wanaotoka kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi ingeendelea kuwepo.

Amewataka vijana hao kwa pamoja kuwa mabalozi wema wa uwekezaji, kwani sera nzuri za uwekezaji ndizo zilizosababisha Mgodi wa Barrick kuachia leseni zake kwa ajili ya mradi huo unaolenga kuwanufaisha vijana.
Meneja Mkuu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko amesema ni furaha ya mgodi huo kuwa sehemu ya mwanzo wa safari ya vijana wanaotoka kwenye vijiji vinavyozunguka mgodi huo kufanya shughuli halali za kiuchimbaji kwa kufuata sheria za nchi.
"Sisi tumetoa leseni nne kati ya hizo za leo na ushirikiano huu utaendelea, kwani ni furaha yetu kuona vijana wetu wanajishughulisha kihalali na shughuli hizi kwa kuzingatia sheria za nchi pamoja na maadili mema. Huu ni mwanzo wa kutengeneza matajiri vijana kupitia sekta ya madini," amesema.
Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Amini Msuya amesema mradi huo utatekelezwa na vijana kupitia vikundi vilivyoundwa kwa mwongozo uliotolewa na Serikali, ambapo kwa awamu ya kwanza jumla ya vikundi 48 vya vijana kutoka wilayani humo vitanufaika.
Amesema vijana hao watafanya uchimbaji wao katika wilaya za Tarime, Butiama na Serengeti, huku ugawaji wa leseni kwa vijana kwa awamu nyingine hivi sasa upo kwenye mchakato wa utekelezaji wake.
Baadhi ya vijana waliopewa leseni hizo wameishukuru Serikali kwa hatua hiyo, wakisema uamuzi huo utasaidia kuimarisha uchumi wa vijana wanaozunguka mgodi na wilaya kwa ujumla.
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukiomba kupata fursa kama hii, hasa ikizingatiwa kuwa sisi shughuli zetu ni uchimbaji wa dhahabu, lakini baada ya uwekezaji wengi wetu tulikosa kazi za kufanya. Kwa hiyo, hatua hii itatusaidia kuwa na shughuli muhimu na halali za kutupatia kipato," amesema Grace Willbert.
"Tumepewa leseni, tunaomba Serikali iendelee kutushika mkono kwani bado tuna changamoto ya mitaji. Tunaomba tuwezeshwe ili uchimbaji huu uwe na tija," amesema Mwita Nyamuhanga.