Watatu mbaroni wakituhumiwa kumuua Scolastica 'gesti'

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza. Picha na Saada Amir.
Muktasari:
- Scolastica ambaye awali hakufahamika, alikutwa amefariki dunia kwenye chumba namba tatu cha gesti ya First and Last iliyopo kata ya Usagara, wilayani Misungwi akiwa amefungwa kitambaa usoni, chanzo cha mauaji hayo kikitajwa ni imani za kishirikina.
Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limewakamata watuhumiwa watatu wa mauaji ya Scolastica Lugalila (40) aliyeuawa Machi 19, 2025 katika nyumba ya kulala wageni ya ‘First and Last Gest’ iliyopo kata ya Usagara, wilayani Misungwi.
Scolastica ambaye awali hakufahamika, alikutwa amefariki dunia kwenye chumba namba tatu cha gesti hiyo huku akiwa amefungwa kitambaa usoni, chanzo cha mauaji hayo kikitajwa ni imani za kishirikina.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Mei 14, 2025 na Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amedai watuhumiwa wa mauaji ya marehemu Scolastica ambaye enzi za uhai wake alikuwa ni mkulima na mkazi wa Nyehunge wilayani Sengerema ni Stephano Manyecha (39) mkazi wa Iwezela Mkoa wa Geita.
Wengine ni Thereza Igabula (39) pamoja na Valentina Igabula (43) wote wakazi wa Nyehunge, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.
“Awali Machi 19, 2025 Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kwa umma juu ya mauaji hayo ambapo, jina la marehemu na wahusika waliotenda mauaji hayo hayakuweza kufahamika, baada ya upelelezi na ufuatiliaji wa kina tumefanikiwa kupata jina la marehemu mbaye ni Scolastica Joseph Lugalila pamoja na watuhumiwa waliohusika katika mauaji hayo,”amedai Mutafungwa.

Mutafungwa ameendelea kudai kuwa, “Chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina kwani inadaiwa watuhumiwa walikuwa wanamtuhumu marehemu anawaroga wasishike mimba. Watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani,”
Mutafungwa amewataka wananchi kuachana na imani za kishirikina na kushirikiana na vyombo vya dola katika kuzuia na kukomesha vitendo vya mauaji yanayotokana na imani hizo potofu.
Mauaji yalivyotokea
Taarifa ya awali ya jeshi hilo ilieleza kuwa, Machi 18, 2025 saa 1 jioni alifika mgeni katika nyumba hiyo aliyejiandikisha kwa jina la Bilal William, mkazi wa Geita akitokea Chato kuelekea Nzega mkoani Tabora.
Mgeni huyo alipewa chumba namba tatu na kuweka mizigo yake, ilipofika saa nne usiku alitoka chumbani akidai anakwenda kutafuta chakula na usiku mkubwa mwanaume huyo alirudi katika nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa na mwanamke (Scolastica).
Inadaiwa ilipofika saa 12:00 asubuhi wakati wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni wakihitaji kufanya usafi ndipo walipokuta mlango wa chumba hicho ukiwa na komeo lililofungwa kwa nje, hali hiyo iliwatia mashaka, hivyo kufungua kufuli hilo na kuingia ndani, ndipo walipomuona marehemu amefungwa usoni kwa kitambaa, akiwa na mikwaruzo usoni huku akiwa mtupu bila mwanaume aliyepangishwa chumba hicho kuwemo.
Tukio lingine
Katika tukio lingine, jeshi hilo linamshikilia mnoa misumeno, Jeremiah Anicent (59) kwa tuhuma za mauaji ya mkazi wa Bupandwa wilayani Sengerema, Mariam Joseph (4) baada ya kumkata kichwani na msumeno wa kukatia mbao uliokuwa kwenye pikipiki yake aliyokuwa akiiendesha.
Mutafungwa amesema tukio hilo limetokea Aprili 28, 2025, saa 1:20 jioni katika kijiji cha Chema, kata Upandwa, Tarafa ya Kahunda wilayani humo ambapo mtuhumiwa alimkata Mariamu kichwani upande wa kushoto na msumeno uliokuwa umefungwa kwenye pikipiki aliyokuwa akiendesha, na kusababisha mtoto huyo kumwaga damu nyingi na kusababisha kifo chake.
“Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na kukabidhiwa ndugu kwa ajili wa mazishi, mtuhumiwa Jeremiah Anicent ameshikiliwa na jeshi hilo kwa uchunguzi na ukikamilika atafikishwa mahakamani kwa hatua nyingine za kisheria. Jeshi la Polisi linatoa wito kwa madereva wanaoendesha pikipiki kuchukua tahadhari wanapobeba mizigo iliyozidi vyombo vyao vya moto ili kuepusha madhara yasiyotarajiwa,”amesema Mutafungwa