Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali kugeukia teknolojia kuharakisha matumizi nishati safi ya kupikia

Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Innocent Luoga,akizungumza leo Jumanne Mei 6,2025 katika kongamano la kwanza la nishati safi ya kupikia Afrika Mashariki,lililofanyika jijini Arusha.

Muktasari:

  • Akizungumza katika kongamano la kwanza kuhusu nishati safi ya kupikia kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, alisema kuwa Serikali inaendelea kupitia sheria, sera na kanuni husika ili kuharakisha utekelezaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Arusha. Serikali imeanza kuangalia teknolojia mbalimbali zinazoweza kupunguza gharama za matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kuharakisha utekelezaji na kufanikisha lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati hiyo ifikapo mwaka 2034.

Kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa kipindi cha miaka 10 (2024–2034), takwimu za sasa zinaonyesha kuwa ni asilimia 16 tu ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia.

Kauli hiyo imetolewa leo, Jumanne Mei 6, 2026, na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, alipokuwa akifungua kongamano la kwanza kuhusu nishati safi ya kupikia kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Amesema kuwa gharama kubwa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia bado ni changamoto kwa baadhi ya kaya, hivyo Serikali imeanza kuchunguza teknolojia zinazoweza kupunguza gharama na kuleta unafuu wa bei, ili kufanikisha malengo na mikakati ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mhandisi huyo ameongeza kuwa Serikali inaendelea kupitia na kuboresha sheria, sera, na kanuni zinazohusika ili kuharakisha na kurahisisha matumizi ya nishati safi.

Amesisitiza kuwa, ili kukabiliana na changamoto ya gharama, Serikali inasambaza mitungi ya gesi kama njia ya kupunguza gharama na kuongeza hamasa ya matumizi ya nishati safi.

Mhandisi huyo amesema kuwa majukwaa mbalimbali ya kitaifa na kimataifa yanaandaliwa ili kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika kutatua changamoto hiyo.

Amesema kuwa duniani kote, takribani watu 2.1 bilioni wanakadiriwa kutotumia nishati safi ya kupikia (kama vile gesi na umeme), badala yake wakitegemea kuni na mkaa. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023 idadi ya watu duniani ni 8.062 bilioni.

Hata hivyo, Tanzania imejipanga kuongeza idadi ya watumiaji wa nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 75 ifikapo mwaka 2030, na asilimia 80 mwaka 2034.

"Lengo la kongamano hili ni kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya nishati safi ya kupikia, ambapo tutaangazia kwa pamoja teknolojia, sheria, kanuni, sera, na kampeni za uhamasishaji ili kuwahamasisha wananchi kuachana na matumizi ya mkaa na kuni na kuelekea kwenye matumizi ya umeme, gesi na nishati safi ya kupikia," amesema.

"Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa kiongozi katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia, na kupitia mkakati wetu wa miaka 10, tutajumuisha utoaji ruzuku, kampeni za kitaifa za uhamasishaji, mikopo nafuu kwa wasambazaji, pamoja na masuala mengine," ameongeza.

Awali, Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa Mfuko wa Maendeleo na Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF), Peter Malika amesema kuwa kongamano hilo lengo lake ni kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi, kukuza matumizi ya teknolojia, na kuboresha sera zinazohusiana.

Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini Tanzania, Lamine Diallo, amesisitiza kuwa Afrika Mashariki, zaidi ya asilimia 90 ya kaya bado zinategemea nishati isiyo salama kama vile kuni na mkaa, ambayo inachangia uchafuzi mkubwa wa hewa.

Naye, Mkurugenzi wa Nishati Mbadala kutoka Wizara ya Nishati na Petroli nchini Kenya, Dk Faith Wandera, amesema kuwa asilimia 34 ya wakazi wa Kenya wanatumia nishati safi ya kupikia na asilimia 75 wanapata umeme.

"Kama Kenya, tumeona umuhimu mkubwa wa matumizi ya nishati safi, hasa katika kuokoa maisha ya watu zaidi ya 26,000 wanaokufa kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa. Huu ni mkutano muhimu kuhakikisha tunaelekea kutatua changamoto ya uelewa wa matumizi ya nishati safi kwa watu wetu," amesema.