Biteko: Vijijini vyote vina umeme, ni zamu ya vitongoji

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege kinachojengwa Manispaa ya Tabora. Picha na Hawa Kimwaga
Muktasari:
- Amesema azma ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora katika sekta mbalimbali za kijamii na kwamba, kwenye umeme, kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa inaendelea.
Tabora. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko amesema hadi sasa vijiji vyote nchini Tanzania vimepata umeme na Serikali inaanza kupeleka umeme katika vitongoji kwa kuanzia na vitongoji 20,000.
Dk Biteko amesema hayo leo Jumamos, Mei 3, 2025, mkoani Tabora baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege cha TCPM, ambacho kina uwezo wa kuzalisha nguzo 120 kwa siku.
Amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho cha TCPM, kinachomilikiwa na Serikali kutakidhi mahitaji ya Mkoa wa Tabora na maeneo mengine ya jirani na kukuza uchumi wa nchi.
“Niwapongeze uongozi wa kampuni ya TCPM na wadau wengine kwa jitihada zenu za kusimamia ujenzi wa kiwanda hiki. Nimejulishwa kuwa utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 73. Ni matumaini yangu kuwa, asilimia iliyobaki mtaikamilisha kwa ufanisi na kwa kuzingatia muda na mahitaji yaliyopo,” amesema Dk Biteko.
Amesisitiza kuwa mahitaji ya umeme yanaongezeka kila mwaka kwa asilimia 10 hadi 15, ukuaji ambao unadhihirisha umuhimu na uhitaji zaidi wa miundombinu ya kisasa, ikiwemo nguzo za zege ambazo ni mbadala wa nguzo za miti.
Dk Biteko amebainisha manufaa ya kiwanda hicho cha nguzo za zege kuwa kitachangia ukuaji wa ajira za moja kwa moja na ajira ambazo hutokana na mnyororo wa thamani.
“Mwaka wa fedha uliopita 2023/2024 usambazaji ulikuwa nguzo 19,368, lakini kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 hadi kufikia Aprili, usambazaji wa nguzo ulifikia 34,181 sawa na ongezeko la asilimia 76, ambayo hii tunaweza kusema ni ukuaji wa ajira ambayo itatengenezwa na sekta hii ya usambazaji wa nguzo za zege,” amesema.

Wananchi wa Tabora wakimsikiliza Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.
Pamoja na hayo, Dk Biteko ameeleza kuwa hadi sasa vijiji vyote vimepata umeme na Serikali inaanza kupeleka umeme katika vitongoji nchi nzima kwa kuanzia na vitongoji 20,000, huku Tabora ikipewa kipaumbele.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema tukio hilo ni muhimu litakalowezesha matumizi ya nguzo ambazo ni imara na za gharama nafuu ikilinganishwa na nguzo za miti.
“Kuna baadhi ya maeneo nguzo za miti zimeshindwa kustahimili, mfano katika maji au dhidi ya moto, lakini nguzo za zege zinadumu muda mrefu na kuna baadhi ya maeneo mkoani Tanga ziliwekwa nguzo za zege na zipo hadi leo, pia zinatunza mazingira,” amesema Mhandisi Mramba.
Meneja Mkuu wa TCPM, Yusuph Kitivo amesema kuwa kiwanda hicho kinamilikiwa na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania kwa asilimia 100.
Amesema tayari nguzo hizo zimeanza kutumika katika mikoa ya Katavi na Tabora na zaidi ya nguzo 80,000 zimeingia Tanesco, na sasa kila wilaya nchini ina nguzo za kampuni hiyo ya zege zilizojengwa na wadau wao.
“Mradi wa kujenga kiwanda hiki ulianza Oktoba 30, 2024, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa uhakika kwa kuwa na nguzo zinazodumu kwa muda mrefu. Umeme wa uhakika unachochea uchumi,” amesema Mhandisi Kitivo.
Amebainisha kuwa gharama ya mradi huo ni Sh6 bilioni, na ujenzi utakamilika kwa viwango vinavyotarajiwa.
“Kukamilika kwa kiwanda hiki kutasaidia ujenzi wa kiwanda kingine mkoani Mbeya na kutakuwa na manufaa makubwa kwa kuongeza pato la Taifa na kuzalisha ajira pamoja na kukuza biashara mtambuka inayotokana na bidhaa hizi,” ameongeza Mhandisi Kitivo.
Aidha, jana baada ya kukikagua Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msongo wa Kilovoti 132/33 kilichopo Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora, Biteko alisema ni lazima Watanzania wapate huduma bora ya umeme, huku akimtaja Rais Samia Suluhu Hassan kuwa kinara katika kusukuma kufikiwa kwa malengo hayo.
Dk Biteko alisema azma ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora katika sekta mbalimbali za kijamii na kwamba, kwenye umeme, kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa inaendelea.
"Tunamshukuru Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) ambaye siku zote anasema wananchi wapate umeme, na naomba nimuahidi kuwa mimi na wenzangu tutafanya kazi kwa kasi unayohitaji ili kuhakikisha wananchi wanapata umeme," alisema Dk Biteko.