Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mradi wa Sh44 bilioni wazinduliwa Tabora

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua mradi wa umeme msongo wa kilovoti 132. Picha na Hawa Kimwaga

Muktasari:

  • Wilaya ya Urambo imekuwa na changamoto ya umeme wa uhakika kwa muda mrefu, lakini siku za hivi karibuni changamoto hiyo imekwisha baada ya kuwashwa msongo wa kilovoti 132.

Tabora. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) kutoa kipaumbele kwa Wilaya ya Urambo katika mpango wa vijiji 28,000 vitakavyopatiwa umeme.

Ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Mei 2, 2025, wakati wa uzinduzi wa kituo cha kupokea, kupooza na kusambaza umeme cha Uhuru, msongo wa kilovoti 132, kilichopo wilayani Urambo, mkoani Tabora.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kumeongeza mapato kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hatua ambayo itazidi kuongezeka kadiri huduma inavyozidi kuunganishwa kwa wananchi.

"Mapato yatazidi kuongezeka, lakini kwa sababu wananchi wa Urambo wamesubiri huduma hii kwa muda mrefu, pia niseme tu kwamba Rea hakikisheni vitongoji vilivyobaki katika wilaya hii vinapata huduma ya umeme," amesema

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesconchini, CPA Renatha Ndege, amesema mradi huo umegharimu Sh44 bilioni na kwa sasa upatikanaji wa umeme mkoani Tabora ni wa kuridhisha, kwani kuna ziada ya megawati 57.

"Kwa sasa, mkoa wa Tabora una umeme wa kutosha na tumeweka mpaka ziada, ili kadiri maendeleo yanavyoongezeka umeme usiwe kikwazo kwao," amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema kukamilika kwa mradi huo kutachochea ukuaji wa uchumi mkoani humo kutokana na uwepo wa umeme wa kutosha.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Saidi Nkumba, amesema uwepo wa umeme wa uhakika ni utekelezaji wa ilani ya chama hicho na kwamba kimejipanga vizuri kwa ajili ya uchaguzi mkuu, kwa kuwa asilimia kubwa ya huduma kwa wananchi ziko vizuri.

"Wananchi wanahitaji huduma za msingi na si maneno, hivyo jitihada za utekelezaji zinaendelea ili kuendelea kuimarisha huduma kwa wananchi wetu wa Tabora," amesema Nkumba.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza na wananchi mara baada ya kuzindua mradi wa umeme msongo wa kilovoti 132. Picha na Hawa Kimwaga

Mbunge wa Urambo, Magret Sitta, amesema vitongoji 126 kati ya vitongoji 259 vya Wilaya ya Urambo havina umeme, huku akiomba wananchi wapunguziwe gharama za kuunganishiwa umeme ili kila nyumba iweze kupata huduma hiyo.

Omari Katirijuma, mkazi wa Wilaya ya Urambo, amesema awali walikuwa hawapati unga kwa wakati kwa ajili ya chakula kutokana na umeme kukatika mara kwa mara, hivyo mashine zilishindwa kufanya kazi vizuri.

"Mwanzo ilikuwa shida san, huwezi kusema nataka unga kwa haraka ukaupata, ni kwa sababu umeme muda wote ulikuwa shida, lakini sasa hivi tunashukuru," amesema Katirijuma.

Dk Biteko yupo mkoani Tabora kwa ziara ya siku mbili akizindua miradi hiyo ya umeme, ambapo leo amezindua mradi wa msongo wa kilovoti 132 wa kilomita 115 kutoka Tabora hadi Urambo, ambao umekamilika.